Viongozi watakiwa kuzingatia maadili


Peter Akaro

Peleja Masesa
TUME ya Utumishi wa Umma imetaka viongozi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma katika utekelezaji majukumu yao ili kuhudumia wananchi ipasavyo.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Peleja Masesa alisema utumishi wa umma una wajibu wa kuleta ustawi kwa wananchi kwa kutekeleza mipango ya Serikali.

Masesa alisema utumishi wa umma unapaswa kukuza uchumi, kutoa huduma kwa jamii na kulinda amani na utulivu, hivyo ni vema watumishi wa umma wakazingatia hilo.

“Kila mtumishi anapoajiriwa hupewa maelekezo ya majukumu ya kazi yake sambamba na miiko ya kazi katika utumishi wa umma.

“Viongozi na watumishi wote wa umma hawana budi kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo hiyo,” alisema.

Alisema katika kuhakikisha maadili ya kazi yanazingatiwa ipasavyo, mamlaka za ajira na nidhamu katika utumishi wa umma zina wajibu wa kuhakikisha kuwa watumishi wote wanafahamu sheria, kanuni, taratibu na miongozo.

“Mwaka 2005 kuliainishwa kanuni za maadili ya utumishi wa umma, na kanuni hizi zimetungwa na waziri wenye dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 34 cha sheria ya utumishi wa umma ya mwaka 2002,” alisema Masesa.

Alisema sheria hiyo imetoa kanuni nane za kuzingatiwa katika utumishi wa umma wa Tanzania.

Kwanza ni kutoa huduma bora, utii kwa Serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa umma, kuheshimu sheria na matumizi sahihi ya taarifa.

Msesa aliongeza kuwa misingi ya uzingatiaji wa maadili unawekwa katika makundi makuu matatu ambayo ni kuzingatia taaluma, uaminifu na kutimiza wajibu.

“Wananchi wana matarajio ya kupata huduma bora kutoka kwa viongozi wa utumishi wa umma waliopewa dhamana ya kuwa katika ofisi kwa lengo la kuleta matumaini na kutatua matatizo yao.

“Ili kukidhi matarajio hayo ya Watanzania na kumudu jukumu la kuwa nguzo muhimu kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu, utumishi wa umma hauna budi kuendeshwa kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kufuata sheria na kanuni,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo