Charles James
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco),
limelalamikiwa kwa kuchelewesha kuwaingizia umeme wateja wake licha ya kulipa
gharama zinazohitajika.
Mmoja wa wateja wa Shirika hilo Joseph
Temba wa Chanika aliiambia JAMBO LEO Dar es Salaam jana kuwa alilipia gharama
za nguzo mbili tangu Agosti, ili kuunganishiwa nishati hiyo, lakini mpaka jana
hakuna kinachoendelea.
Alisema anashangazwa na danadana
anazopigwa na watendaji wa Tanesco licha ya kulipa gharama zinazohitajika, lakini
kila mara anaambiwa Shirika halina nguzo.
“Hivi kweli Tanesco inaweza kukosa nguzo
za kuwaingizia wateja wake umeme? Waziri Muhongo (Profesa Sospeter), anafanya
kazi kubwa, lakini kuna baadhi ya watendaji wanataka kumwangusha ili aonekane ni
‘jipu’, hii si sahihi watimize majukumu yao ipasavyo ili nchi isonge mbele kama
Rais John Magufuli anavyotaka kuona Tanzania ya viwanda,” alisema Temba.
Abdallah Omary wa Kongowe alimwomba Rais
Magufuli ‘kutumbua’ watendaji wa Tanesco wanaoshindwa kwenda na kasi yake kutumikia
Watanzania.
“Mimi nataka nifungue mashine ya kukoboa
na kusagisha nafaka, lakini nacheleweshwa na Tanesco. Nimelipa Sh 700,000 tangu
Septemba niwekewe umeme, lakini Tanesco wanadai hawana
nguzo, nauliza ni lini zitaletwa?” alihoji Omary.
Alisema ni vema sasa Serikali ikatafuta
mbadala wa Tanesco kwa kuwa umeme ni chanzo cha maendeleo ya kiuchumi duniani.
Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam ambaye hakutaka kuandikwa jina gazetini, aliiambia JAMBO LEO kuwa
iwapo Tanzania itakuwa na umeme wa uhakika, ndoto za Rais Magufuli zitatimia.
Alisema iwapo nchi itakuwa na viwanda
vya kutosha itaondoa ukosefu wa ajira nchini kwani watu wengi wataajiriwa na
bidhaa kutengenezwa nchini badala ya kuagiza nje.
JAMBO LEO ilimtafuta Mkurugenzi Mtendaji
wa Tanesco, Felchesmi Mramba lakini hakupatikana kuzungumzia suala hilo
kutokana na simu yake kuita bila kupokewa.
0 comments:
Post a Comment