Hussein Ndubikile
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
imetangaza kusitisha mchakato wa kuvipa vyuo saba vya mafunzo ya ualimu mamlaka
kamili ya kujiendesha kiutendaji hadi vitakapofanya maboresho.
Kaimu Kamishna wa Elimu wa wizara hiyo,
Nicolaus Buretta, alibainisha uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa
akitoa taarifa juu ya Mwongozo wa Waraka Namba 5 wa Elimu wa mwaka 2016 kuhusu
utekelezaji wa programu ya mafunzo ya ualimu.
Alivitaja vyuo hivyo kuwa ni pamoja na
Chuo cha Ualimu cha Kleruu cha Iringa, Chuo cha Dakawa, Chuo cha Ualimu cha
Butimba, Chuo cha Mpwapwa, Chuo cha Mtwara na Chuo cha Ualimu cha Patandi na
Chuo cha Ualimu cha Kasulu.
Alisema kikosi kazi kilichoundwa na
wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kilibaini kuwapo changamoto
zinazozuia vyuo hivyo kuwa huru zikiwamo za kutokuwa na vitendea kazi na kukosa
bodi zinazovisimamia.
“Taarifa ya kikosi kazi cha wizara kwa
kushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa, wakuu wa vyuo kimebaini changamoto
zinazozibana vyuo saba vya ualimu kupata mamlaka huru hadi vitakapokamilisha
maboresho,” alisema.
Alisema wanafunzi wa Stashada
waliodahiliwa kwa mwaka wa masomo wa 2016/17 katika vyuo hivyo wataendelea na
masomo yao kama kawaida, huku mchakato wa maboresho ukiendelea.
Alisisitiza kuwa vyuo hivyo vitaendelea
kutoa mafunzo ya ualimu chini ya wizara hiyo kwa kutumia mtalaa wa awali
ulioandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania hadi vitakapokamilisha mchakato huo.
Alisema kikosi kazi hicho hicho
kilibaini kuwa upimaji wa utahini unaofanyika sasa ni kama wa mpito na hauna
uhakika na ubora wake na ufuatiliaji wa Udhibiti ubora wa mafunzo hauna uhakika
kutokana na idadi kubwa ya vyuo vya mafunzo ya ualimu.
Nyingine ni muundo wa utumishi hautambui
wahitimu wa Stashahada ya Juu ya ualimu na kutokuwepo na maandalizi ya
kuwawezesha wahitimu wa ngazi hiyo ya ualimu kujiunga mafunzo ya shahada ya
kwanza kwa mwaka mmoja kama ilivyokuwa inatarajiwa.
Buretta alisema katika utekelezaji wa
waraka huo programu za mafunzo ya taaluma hiyo zitakuwa Astashahada na
stashahada kwa kutumia mtaala wa kitaifa wa taasisi hiyo ulioandaliwa mwaka
2009 kwa ngazi hizo.
Alisema Tarajali ya Stashahada ya Juu ya
Elimu ya Sekondari yaliyokuwa yakitolewa kuanzia mwaka wa nasomo 2014/15
yamehitimishwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Elimu ya
Ualimu, Basiliana Mrimi alisema vyuo hivyo vtakuwa huru hadi wizara
itakapothibitisha kwa kupeleka tamko bungeni la kuvijadili.
0 comments:
Post a Comment