*Ni walioingia, kuishi Marekani kinyume
*Wakenya 30,000 nao kurudishwa kwao
Fidelis Butahe
Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump |
WAKATI Rais mteule wa Marekani, Donald
Trump akisubiriwa kutekeleza ahadi yake ya kutimua wahamiaji haramu, Baraza la
Watanzania zaidi ya 50,000 waishio katika Taifa hilo kubwa duniani, limesema
hatima yao inasubiri uamuzi wa kiongozi huyo.
Wakati Watanzania hao wakisubiri huruma
ya Trump katika mchakato wa kuondoa wahamiaji haramu akitangaza kuondoa milioni
tatu baada ya kuapishwa, Kenya imetangaza raia wake 30,000 wanaoishi Marekani
watarejeshwa.
Akizungumza na JAMBO LEO kwa njia ya
simu na barua pepe, Rais wa Baraza hilo, Charles Bishota alisema rungu la
kiongozi huyo atakayeapishwa Januari 20, halikwepeki kwa Watanzania hasa wanaoishi
Marekani kinyume cha sheria na waliohukumiwa kwa uhalifu.
“Kwa sasa tunasubiri Trump aanze kazi
ili tutambue ni jinsi gani atakavyoshirikiana na nchi yetu. Maneno yake (Trump)
wakati wa uchaguzi waliyasikia wengi, lakini Marekani kuna taratibu zake za
uhamiaji,” alisema Bishota na kuongeza:
“Hata ndani ya chama cha Republican
mjadala huu wa uhamiaji unaendelea na mpaka sasa Spika wa Bunge na Trump wana
mtazamo tofauti kidogo tofauti kuhusu hili; lakini tuna imani taratibu za
sheria zilizopo zikiwamo mahakama za uhamiaji, zitaheshimiwa hadi sheria
zitakapobadilishwa.”
Wakati Bishota akieleza hayo, kiongozi wa
zamani wa Baraza hilo, Ben Kazora aliiambia JAMBO LEO kwamba idadi ya Watanzania
wanaoishi Marekani sasa ni takribani 50,000, hata hivyo hakueleza kati yao ni
wangapi wanaoishi kihalali.
Kuchaguliwa kwa Trump kuwa Rais wa 45 wa
Taifa hilo kumeibua hofu miongoni mwa raia wa mataifa mbalimbali wanaoishi bila
nyaraka halali, wakiwamo Watanzania, kutokana na sera za mfanyabiashara huyo
maarufu kutotaka wageni haramu.
Katika kampeni zake, Trump alisema
hahitaji wageni walioingia Marekani kwa kukwepa sheria na kwamba atawatimua ili
wakaanze mchakato wa kuomba kuingia nchini humo wakiwa kwenye mataifa yao.
Katika ufafanuzi wake, Bishota alisema:
“Sina takwimu kamili za Watanzania waliohukumiwa. Natarajia kuona
watakaobainika wanapitishwa kwenye
mkondo wa sheria. Sheria iko wazi, kwamba kabla ya kutolewa, mhusika lazima
apitishwe kwenye Mahakama ya Uhamiaji ambako atakuwa na haki ya kujitetea.”
Alisema endapo kutakuwa na mabadiliko ya
Sheria ya Uhamiaji, huenda mambo yakabadilika, kwa kuwa Taifa hilo huwa makini
kutangaza mambo yaliyobadilika.
“Mara nyingi suala kama hili
likitangazwa wadau huwa wanazungumzia jinsi gani inaweza kuwagusa ingawa mara
nyingi matokeo yanaweza kuwa tofauti kutegemeana na mazingira ya kila mtu aliye
huku,” alisema Bishota.
Alisema Watanzania wengi walio nchini
humo waliingia kama wanafunzi na baada ya kuhitimu masomo, walifanya kazi kulingana
na taaluma zao na wengine kugeukia ujasiriamali.
“Wengi tunafahamiana kupitia jumuiya
zetu, tunashirikiana wakati wa shughuli mbalimbali na wengi tunafuata sharia,
ila sina takwimu zinazopingana na jambo hili,” alisema.
Alipoulizwa kama tayari wameshakutana
kujadili sintofahamu hiyo alisema: “Hatujawahi
kukutana kujadiliana hili suala. Uchaguzi ndo kwanza umekwisha na Rais
hajaanza kazi, kama kuna mabadiliko ya sheria basi suala hilo litazungumzwa
tu.”
Alisema jukumu kubwa la Watanzania
wanaoishi nje ni ushiriki wao katika uandaaji wa sera ya nchi kuhusu Watanzania
waishio ughaibuni.
“Tungependa sana tushirikishwe, kwani
tuna imani mchango wetu ni mkubwa. Tumeshawasilisha maombi yetu rasmi kwa Serikali
ya Tanzania na tunasubiri majibu,” alisema.
Kwa upande wake, Kazora alisema: “Si
rahisi mtu kurudishwa Tanzania bila kosa. Ila wanaoishi hapa (Marekani) kinyume
na sheria wataondolewa na Rais yeyote na hata Tanznaia huwa ipo hivyo kwa wahamiaji
haramu.”
Alisema Watanzania hawapaswi kujawa hofu kwa maelezo kuwa Rais Barack Obama anayemaliza muda wake, katika utawala wake wa miaka minane amefukuza wahamiaji wengi zaidi kuliko watangulizi wake.
“Nakumbuka juzi katika kipindi cha
dakika 60 hapa Marekani, Trump alitamka wazi kwamba atawafukuza wahalifu ila wasio
na makosa makubwa atawafikiria. Alisema wazi kuwa kwake kitu muhimu kuliko
vyote ni kuimarisha mipaka, hilo ndilo jambo lake kubwa analosisitiza lakini si
kufukuza walio hapa,” alisema.
Kazora alibainisha kuwa kila nchi ina
sheria yake ya uhamiaji na ambao hawajazivunja hawawezi kuwa na hofu, “maneno
ya Trump katika kampeni yameshtua watu sana, kikubwa hapa ni kufuata sheria tu
maana alichokisema si jambo geni kwa wahamiaji katika nchi yoyote duniani.”
Kenya
Habari kutoka Kenya zinakadiria kuwa
raia 30,000 wa nchi hiyo ambao ni wahamiaji haramu Marekani wamo hatarini
kurudishwa nchini humo kutoka Marekani.
Kuna takriban wahamiaji haramu milioni
11 waishio Marekani ambao Trump alitishia kuwarudisha makwao wakati akifanya
kampeni.
Hata hivyo wengi wao waliamini kwamba
angebadili msimamo baada ya kutangazwa mshindi, lakini ni dhahiri sasa kwamba
Trump hatarudi nyuma katika msimamo wake wa sera ya uhamiaji.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji mwaka jana
lilitoa makadirio kuwa Wakenya 30,000 wanaishi Marekani kinyume cha sheria
“Idadi hii inatokana na takwimu za viza
na zingine kutoka Ofisi ya Sensa ya Marekani,” taarifa ilisema.
Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani
inakadiria kuwa idadi ya Wakenya haramu nchini humo iliongezeka mara saba kati
ya mwaka 1990 na 2013.
Mwaka 1990, Wakenya ambao hawakuwa
wamesajiliwa Marekani walikadiriwa kuwa 3,000, wakaongezeka hadi 15,000 mwaka
2000 na 24,000 mwaka 2013.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Sensa ya
Marekani, kulikuwa na takriban Wakenya 106,484 wakiishi nchini humo mwaka 2013,
wakiwamo hao haramu.
Takriban 62,858 walikuwa wameajiriwa na
wengine wakiwa shuleni au wasiokuwa na umri wa kuanza shule.
Nusu ya fedha zinazotumwa Kenya kutoka Wakenya
waishio nje (Diaspora), zinatoka Marekani na Kanada.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya
Kenya, Wakenya hadi Juni walituma nyumbani Sh bilioni 165, huku Sh bilioni 85
zikitoka Marekani.
Fedha hizo zinazidi za kigeni
zinazoingia kutokana na mauzo ya chai, maua, kahawa na utalii.
Juzi Msemaji wa Serikali, Eric Kiraithe
alizungumzia kuhusu wakenya walio hatarini kurudishwa nyumbani.
Alisema si sehemu ya “fahari ya Taifa la
Kenya” kwa wananchi wake walio nchi za nje “kucheza mchezo wa kujificha na
sheria.
“Tunafarijika, kwamba (Trump) analenga
wahalifu. Kwa Wakenya ambao wamefika Marekani kwa sababu yoyote ile, tunawataka
waishi kwa kuheshimu sheria ya Marekani,” Kiraithe alisema.
“Huwezi kuishi kokote kinyume cha sheria.
Kuna fursa nyingi hapa (Kenya),” alisema.
“Kuna Wakenya wengi ambao ni wakulima na
wengine wafugaji na wanafanya vizuri tu. Hivyo kama kuna mtu hawezi kuhifadhiwa
kihalali katika nchi nyingine, ni vema wakawahi kupanda ndege mapema na kurudi
nyumbani, ni bora,” Kiraithe alisema.
Kati ya mwaka 2009 na mwaka juzi,
Wakenya 3,050 wahamiaji haramu walikamatwa Marekani na 593 kati yao
wakarudishwa nchini.
Kipindi hicho hicho, Wakenya 34,233
walipewa ukazi wa kudumu Marekani. Mwaka juzi pekee Wakenya 24,425 walitembelea
Marekani kwa sababu mbalimbali.
Katika kipindi hicho hicho, Wakenya 49 walikwenda
Marekani kama wakimbizi wakati 568 walipokewa kama watafuta hifadhi.
Idadi ya Waafrika wasiosajiliwa Marekani
wanakadiriwa kuwa takriban 300,000 nje ya wakimbizi haramu milioni 11.4 ambao
Trump anataka kuwatimua.
0 comments:
Post a Comment