Mwandishi Wetu
Dk. John Mgufuli |
Mkurugenzi wa Kituo cha Ecolife kinachojishughulisha na masuala ya
mazingira, Dk. Rogate Mshana ametathmini mwaka mmoja tangu Ras John Magufuli alipoingia
madarakani akisema kiongozi huyo ameanza vizuri na kurudisha imani ya
Watanzania kwa Serikali yao.
Akizungumza na JAMBO LEO, Dk. Mshana alisema kinachotakiwa sasa ni
Watanzania vikiwamo vyama vya upinzani, kumuunga mkono ili afanikishe mpango
aliokusudia katika kujenga uchumi imara.
“Hapo awali Watanzania wengi walianza kukata tamaa na utendaji
mbaya wa Serikali kiasi cha kuamini kuwa wanaweza kujiendesha wenyewe bila Serikali,”
alisema Dk Mshana na kufafanua:
“Mfumo mzima ulioza kwa rushwa na huduma za serikali zilikuwa kama
hazipo kwa walio wengi bali kwa wale waliopo tu
katika ngazi mbalimbali za uongozi.”
Kutokana na hali hiyo, alisema Rais Magufuli alianza kwa kutimiza
ahadi zake za kupiga vita rushwa, kulipa kodi, kuinua watu maskini, kuimarisha
elimu, afya, utawala bora na kuweka mipango ya kuwafikisha mafisadi na
majangili katika vyombo vya sheria.
“Kazi hii imeanza vizuri kinachotakiwa ni kujenga mfumo adilifu wa
taifa wenye kuheshimu utawala wa sheria,” alisema Dk Mshana.
Akirejea mazingira ya awamu zilizopita, alisema vyombo vya habari
viliandika mara nyingi kuhusu Watanzania kukata tamaa wakieleza kwamba nchi
haitaweza tena kujitawala kwa uadilifu kutokana na vilio vya ufisadi, lakini
Rais Magufuli amebadili hali hiyo.
Alisema katika mazingira ya sasa, vyama vya upinzani vinapaswa
kumsaidia Rais Magufuli katika mapambano yake ya kulijenga taifa lenye maadili.
Alisema iwapo wapinzani watazingatia wataikosoa Serikali kwa lengo
la kujenga watasaidia mipango ya kuwaondoa Watanzania kwenye umaskini.
“Vyama vya upinzani ni muhimu kutambua kuwa serikali inafanya kazi
sasa baada ya uchaguzi na kwamba ukosoaji wake uwe wa kujenga na siyo kubeza,”
alisema Dk. Mshana.
Alisema katika mfumo huu vyama vyote vikiwa viadilifu na kukosoana
kwa hoja na heshima bila kuchafuana kwa lugha chafu hata kizazi kijacho
kitajifunza mambo mema na uraia unaojali uadilifu.
Hata hivyo, alisema Serikali nayo inapaswa kuhakikisha ustawi wa
vyama vya siasa nchini.
“Kuna mambo bado ya kufanya, kwa mfano kuifanya serikali isione
vyama vya upinzani kama maadui bali sehemu muhimu katika kutoa ushauri nasaha
wa namna ya kuleta maendeleo Tanzania,” alisema.
Vyama vya upinzani pia vimetambua juhudi hizi za kuokoa raslimali
za nchi kutumiwa hovyo au kufisidiwa hivyo vina wajibu wa kuunga mkono kazi hii
ambayo wamekuwa wakiipigia kelele kwenye majukwa katika awamu zilizopita.
Kero nyingi za wananchi ambazo vyama vya upinzani vilikuwa vinazungumzia
zinaanza kutatuliwa licha ya kwamba mkakakati huo umekuwa ukikabiliwa na
changamoto nyingi.
0 comments:
Post a Comment