Wasomi watofautiana Ikulu kupanga mishahara


Fidelis Butahe

WAKATI wananchi wakilia ukata kwa maelezo kuwa fedha imekauka mifukoni, kuna kila dalili hali kuendelea kuwa mbaya zaidi baada ya Serikali kutangaza azma yake kuwa mishahara, marupurupu na maslahi mengine ya watumishi wa umma yataidhinishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma.

Uamuzi huo hata hivyo unaonekana kugawa wachambuzi wa mambo ya uchumi waliozungumza na JAMBO LEO.

Wachambuzi hao wamesema jambo hilo ni zuri kwani litaondoa pengo kubwa la mishahara kwa watumishi wa umma, huku wengine wakisema unamwongeza madaraka Rais na kutaka taasisi husika zipendekeze mishahara na maslahi mengine, huku ofisi hiyo ikibakiwa na kazi ya kusimamia, kushauri na kutoa uamuzi wa mwisho.

Kwa mujibu wa Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali kwa mwaka 2016 uliowasilishwa bungeni juzi, sheria hiyo itakuwa na kifungu kinachoweka masharti kuwa taasisi, wakala, bodi au tume za Serikali, hazitakuwa na mamlaka ya kuidhinisha mishahara na marupurupu kwa watumishi wa taasisi hizo na badala yake kibali kitatolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi.

“Binafsi sioni kama ni jambo zuri, ni sawa na kumwongeza Rais madaraka, yaani hadi mshahara uamuliwe Ikulu?

“Sidhani kama utaratibu huu utasaidia. Serikali inapaswa kuwa na sera ya viwango vya mishahara inayopaswa kulipwa katika mashirika na taasisi za Serikali, si kuweka sheria kwamba wewe utalipwa hivi na wewe vile,” alisema Profesa Gaudence Mpangala, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Ruaha.

Juzi Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju wakati akiwasilisha Muswada huo, alisema lengo la marekebisho hayo ni kuweka usawa wa maslahi kwa watumishi wa umma kulingana na kazi wanazofanya.

Pia, marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha kuwa hakuna tofauti kubwa ya mishahara na marupurupu kwa watumishi wa umma wakati wote wanafanya kazi zinazolingana kwa kuwa na Mamlaka moja itakayoratibu jambo hilo.

Hata hivyo, masharti hayo hayatatumika kwa mishahara, marupurupu na maslahi mengine kwa Bunge, Mahakama, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim alisema, “kulikuwa na kushindwa kwa Serikali katika kuendeleza mambo yake katika baadhi ya taasisi, ndiyo maana baadhi ya taasisi zilipewa mamlaka ya kujipangia viwango vya mishahara lakini kwa utaratibu maalumu, mfano TRA (Mamlaka ya Mapato) na Tanroads (Wakala wa Barabara), ila kwa masharti ya kazi kufanyika kwa faida.

“Kama malengo yamefikiwa (faida) uamuzi wa Serikali ni sawa, tofauti ya kipato inaweza kuleta shida kubwa sana mbele ya safari. Ndiyo maana kuna wakati kila mtu alitaka mtoto wake apate kazi TRA, Tanroads, Bohari Kuu ya Dawa (MSD), maeneo ambayo watu wanajipangia mishahara.”

Alisema watumishi wa taasisi za Serikali kuwa na viwango sawa vya mishahara na watumishi wengine, ni jambo zuri lakini akahadharisha kuwa uamuzi huo huenda ukaathiri Watanzania walioitwa nchini na kupewa nafasi za uongozi kwenye taasisi za Serikali.

Katika maelezo yake, Profesa Mpangala alipingana na Salim na kusisitiza: “Uamuzi wa nani analipwa kiasi gani unapaswa kuachwa  chini ya taasisi husika ambayo itafuata hiyo sera ya mishahara. Hapo unazungumzia hadi serikali za mitaa. Huu ni ukiritimba wa hali ya juu.”

Alibainisha kuwa kilio cha Watanzania kudai Katiba Mpya, ni pamoja na kutaka kupunguza madaraka ya Rais ili yaende kwa wananchi, taasisi na mashirika.

 “Nakubaliana na hoja ya kudhibiti watu kujipangia mishahara holela ila natofautiana nao juu ya namna gani udhibiti usifanyike kwenye malipo makubwa,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema: “Ni kati ya vitu ambavyo vimekuwa vikileta shida maana bodi za taasisi zilikuwa zikiweka viwango vya mishahara wanavyotaka na kujikuta wanatumia fedha nyingi katika mishahara kuliko wanachoingiza.”

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stola alisema jambo hilo ni zuri huku akitoa angalizo kwamba taasisi husika ndizo ziwe zinapendekeza viwango vya mishahara na si kuiachia Ikulu.

“Katika jambo linaloanzia ngazi ya chini lazima lifike mahali ambako kutakuwa na uamuzi wa mwisho, Ikulu haipaswi kufanya kazi hii bila kushirikisha taasisi yoyote ya kitafiti au takwimu.

“Wakati mwingine (Utumishi) inaweza kufanya kazi bila kuangalia hali halisi, ila kama  itakuwa msimamizi tu  wa mwisho lakini mchakato unaanzia vyombo vya chini, ni jambo la kawaida na zuri,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo