Grace Gurisha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeonya
kwamba iwapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda hatafika kutoa utetezi
wake Novemba 15, katika kesi ya madai ya Sh milioni 200 iliyofunguliwa
na waliokuwa makada wa CCM, Mgana Msindai na John Guninita itafunga ushahidi wa
upande wa utetezi na kutoa uamuzi.
Hatua hiyo ilifikiwa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi
Thomas Simba, baada ya Makonda kushindwa kufika mahakamani hapo jana bila
sababu ya msingi, ambapo awali Hakimu alisema lazima siku hiyo (jana) awepo ili
atoe utetezi wake, lakini hakutokea.
“Kama Makonda hatafika mahakamani Jumanne nitafunga
ushahidi wa upande wa utetezi na kutoa uamuzi wa ushahidi uliotolewa na Msindai
na Guninita,” alisema Hakimu Simba
Hadi kufikia hatua hiyo ni baada ya Wakili wa Makonda,
Lucio Peter kuieleza Mahakama kuwa mteja wake hayupo, licha ya Hakimu
kusisitiza jana awepo. Walalamikaji wanawakilishwa na mawakili Esther Shedrack
na Benjamin Mwakagamba.
Katika kesi hiyo ya madai namba 68 ya 2015, Msindai na
Guninita kupitia wakili wao, Mwakagamba walifungua kesi wakiiomba Mahakama hiyo
ya Kisutu imwamuru Makonda aombe msamaha na kumlipa kila mmoja Sh milioni 100.
Wanadai kiasi hicho cha fedha kutokana na maneno ya
kuwadhalilisha yaliyotolewa na Makonda wakati akiwa Katibu Uhamasishaji Chipukizi
CCM alipoitisha mkutano na waandishi wa habari.
Pamoja na hayo, wanaiomba Mahakama itoe zuio la kudumu kwa Makonda asizungumze
tena maneno ya kashfa dhidi yao wala kuyasambaza kama alivyofanya awali.
Pia Makonda alipe riba na gharama za kesi na nafuu zingine.
Walidai kuwa Makonda akiwa Katibu Uhamasishaji Chipukizi
wa CCM, katika mkutano wake alidai kuwa
Msindai na Guninita ni vibaraka wanaotumiwa kuharibu CCM kwa nguvu ya pesa.
Msindai na Guninita wanadai maneno hayo ya Makonda yaliwadhalilisha
na kufanya waonekane kuwa viongozi wasiofaa kuongoza CCM na yaliwadhalilisha
mbele ya jamii na CCM kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment