Wasomi wasisitiza wabunge waibane Serikali


Suleiman Msuya na Fidelis Butahe

SIKU moja baada ya wabunge ‘kuirarua’ Serikali bungeni, wakitaka itoe majibu stahiki kuhusu hali ya uchumi nchini na masuala mengine nyeti imepongezwa na wasomi, wakiwataka kushikilia msimamo wao wa kuikosoa kwa maelezo kuwa wana haki ya kuzungumza kwa mujibu wa Katiba.

Wamesema moto wa wawakilishi hao wa wananchi ukiendelea bila woga na kuanza kutetea maslahi ya vyama vyao, utalifanya Bunge kutekeleza wajibu wake ipasavyo na kuwa msaada kwa Serikali.

“Ukiwasikiliza hoja zao zimejikita katika maisha ya wananchi ila hata wao wanaonesha kuwa wanataabika…, nadhani wakiendelea hivyo Serikali itanyooka,” alisema Hellen Kijo-Bisimba, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Tangu kuanza kwa vikao vya mkutano wa Tano wa Bunge la 11 Jumanne wiki hii, wabunge kwa nyakati tofauti wameibana Serikali, zaidi ikiwa juzi baada ya kudai kuwa imekuwa na matumizi makubwa kuliko kinachopatikana.

Baadhi ya wabunge hao, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo) , John Heche (Chadema), Dk Raphael Chegeni, Hussein Bashe na Ahmed Salum (wa CCM), wakichangia mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18, walimponda Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwa kutoa takwimu zinazokinzana na hali halisi ya uchumi huku pia wakigusia suala la elimu.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Frank Tily alisema kinachofanywa na wabunge hao ndiyo kazi, “wasimamie hicho hicho wanachokisema.”

Alibainisha kuwa ni jambo la aibu kwa wabunge kufanya kazi yao kwa mitazamo ya vyama wakati wanajua kuwa wanawalisha wananchi.

Alisema iwapo watatofautiana katika kujadili hoja, hakuna mtu atakayewashangaa lakini wakionesha tofauti za kivyama, watakuwa wamekosea wananchi wanaowawakilisha.

Mhadhiri mwingine wa Chuo hicho, Profesa Kitila Mkumbo alisema: “Kuna mambo mawili nayaona. Kwanza, ukweli haufichiki, lazima uzungumzwe maana wabunge ni sehemu ya wananchi na wanaona hali halisi ya maisha ya wananchi huko wanakotoka, hali ni ngumu kwa kweli.

“Ila pia hatua ambazo Magufuli anazichukua zinawabana hata wabunge wenyewe na mfano ni hili suala la kubana safari za nje.”

Profesa Gaudance Mpangala wa Chuo Kikuu Ruaha, alisema mshikamano uliooneshwa na wabunge hao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya uchumi iliyolikumba Taifa.

Alibainisha kuwa sasa wabunge wa CCM wameanza kuona mahitaji ya wananchi, ili waweze kujiondoa katika kundi la kulaumiwa ni lazima wakiseme kile kinachowakwamisha wananchi waliowachagua na kwamba hali hiyo itaongeza uwajibikaji serikalini.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Damian Gabagambi, alisema Bunge ndicho chombo cha kusimamia Serikali katika majukumu yake, hivyo wanachofanya ni sawa na kinapaswa kupongezwa.

Alisema licha ya Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kuonesha dhamira ya kufanya kazi na kuleta maendeleo ya wananchi, unapotokea upungufu ni lazima uhojiwe.

Profesa Gabagambi alisema mshikamano huo wa wabunge unaweza kuchangiwa na wao kukutana na changamoto mbalimbali katika majimbo yao, hata katika chombo hicho cha kutunga sheria ambacho kinadaiwa kukabiliwa na ukata kwa sasa.

Hata hivyo, Bashiru Ally ambaye ni Mhadhiri wa UDSM alipingana na wenzake na kubainisha kuwa ugeni wa baadhi ya wabunge, upya wa Serikali na idadi kubwa ya wabunge wa upinzani bungeni unaweza kuwa chanzo cha yote yanayozungumzwa tangu kuanza kwa vikao vya Bunge hilo.

“Upya wao unaweza kuwa wa kujua mambo, ujasiri wa kusema, mawazo mapya, makosa na mambo mengi. Hakuna sababu ya kulinganisha Bunge hili na mabunge yaliyopita wakati kuna vigezo vingi,” alisema Bashiru.

“Kuna mpango wa maendeleo wa miaka mitano ambao huko nyuma haukuwepo na sasa wanaujadili, kuna sheria mpya, matatizo mapya, sioni kitu kinachoshangaza. Ningeshangaa iwapo ningeona tofauti mpya ziendeleze na mambo ya zamani.”

Hoja hiyo ya Bashiru ilikosolewa na Mkurugenzi wa Kituo cha Uchumi na Maendeleo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Christopher Awinia, akibainisha kwamba kwa muda mrefu Bunge lilikuwa na kasoro, kwamba mshikamano wa wabunge hao ni kitu kipya kinachopaswa kupongezwa.

Alisema Bunge ni chombo huru kwa mujibu wa Katiba na hakipaswi kuingiliwa na mtu, ”Wanatakiwa kukaza buti na kuendelea na msimamo huo kwani hiyo ndio kazi ya Bunge si kama walivyokuwa wanafanya awali, kushabikia mambo ambayo hayana msingi wala tija kwa wananchi na Taifa.”

Katika kusisitiza jambo hilo, Kijo-Bisimba alisema: “Kuna mambo yanagusa wabunge na inaonekana wameshindwa kuvumilia kama awali. Bunge linapaswa kufanya kazi ili wananchi waweze kufikiwa na huduma muhimu na si kufanya siasa kama ilivyokuwa huko nyuma.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo