Lissu afutiwa dhamana, Lema akamatwa


Grace Gurisha

Tundu Lissu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeamuru Mbunge wa Singida Mashariki,Tundu Lissu (Chadema) kukamatwa, baada ya kukiuka masharti ya dhamana ya kwenda mkoani bila kibali cha Mahakama.

Pia Mahakama imeamuru itolewe hati ya kuwaita wadhamini wa Lissu, ambao ni Robert Katula na Ibrahim Ahmed wakajieleze kwa nini wasilipe fungu la dhamana kutokana na kwamba Mbunge huyo amekuwa akikiuka masharti ya dhamana.

Wakati hayo yakiendelea Dar es Salaam, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema naye amekamatwa na polisi waliomsafirisha kutoka Dodoma hadi Arusha ambako anashikiliwa kwa mahojiano kwa tuhuma za uchochezi, akitarajiwa kufikishwa mahakamani.

Hati ya kukamatwa kwa Lissu ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya kubaini kuwa Mbunge huyo hayuko kizimbani, ndipo alipotaka kujua kwa nini hayupo, kwa sababu hakuna ruhusa yoyote aliyopokea.

Mdhamini wa Lissu, Katula alimweleza Hakimu kuwa Mbunge huyo amekwenda kwenye kesi ya uchaguzi, Mahakama Kuu ya Mwanza.

Kauli hiyo ilimkasirisha Hakimu Simba akasema: "Kama tusingempa dhamana angekwenda kusikiliza kesi hiyo saa ngapi? Kwa sababu Mahakama Kuu ya Mwanza amesimama kama wakili na huku ni mshitakiwa na anajua kabisa dhamana inatolewa kwa masharti.

"Kwa nini anafanya hivi, kwa sababu mahudhurio yake yamekuwa mabovu ni dharau au nini? Alitakiwa kutumia busara kuomba ruhusa na si kuondoka bila taarifa," alisema Simba.

Katula alidai kuwa Lissu alimwambia aliandika barua ya ruhusa ya moja kwa moja, hali iliyomfanya Hakimu huyo kushangaa na kumweleza mdhamini huyo kuwa hakuna ruhusa ya jumla.

Hakimu Simba alimgeukia Wakili wa Serikali, Patrick Mwita na kumwuliza anasemaje kuhusu Lissu kukiuka masharti ya dhamana ndipo alipoomba hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa itolewe.

"Hati ya kukamatwa kwa Lissu itolewe bila sababu yoyote wala kujitetea na samansi za wadhamini Katula na Ahmed wajieleze kwa nini wasilipe fungu la dhamana, kutokana na kwamba waliyemdhamini amekuwa akikiuka masharti," alisema Simba.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 21 itakapotajwa. Si mara kwanza Lissu kukosekana mahakamani bila taarifa, alishawahi kwenda Ujerumani kwa matibabu bila kutoa taarifa, ambapo wakati yote hayo yanaendelea, mawakili wake hawakuwapo.

Washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Mhariri Mkuu wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Mhariri Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Ilidaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, Dar es Salaam, washitakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika hatua nyingine, Mbunge Lema, anashikiliwa katika mahabusu ya Polisi ya Kituo Kikuu cha Polisi Arusha kwa mahojiano akidaiwa kutoa lugha za uchochezi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, Lema anashikiliwa hadi Jeshi hilo litakapomaliza mahojiano naye kuhusu tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi na baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo atafikishwa mahakamani.

Kamanda Mkumbo alisema Lema amekuwa akitoa lugha za uchochezi na kuzirudia kila mara, hivyo wameona vema wamkamate wamhoji ili aweze kufafanua.

“Juzi tulimkamata akitoka Dodoma na tulifanya naye mahojiano na kumwachia kwa dhamana, lakini kuna baadhi ya makosa hatukuwahi kumhoji, sasa tumeamua kumhoji kwa mara nyingine,” alisema.

Hata hivyo, alipotakiwa kutaja maneno ya uchochezi aliyotamka Lema, Kamanda Mkumbo hakuwa tayari kuyaweka hadharani akisema kufanya hivyo ni kuharibu ushahidi na pia si sheria kwa suala ambalo bado liko kwenye uchunguzi.

Hata hivyo, Novemba mosi Kamanda Mkumbo akiwa anazungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, alitaja maneno ya uchochezi anayodaiwa Lema kuyataja kuwa ni:

“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiendelea kukandamiza demokrasia, siasa za ukandamizaji Taifa litaingia katika umwagaji wa damu, nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa kidikteta.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo