Fidelis Butahe
Donald Trump na John Magufuli |
WACHAMBUZI wa masuala ya siasa wamemfananisha
Rais John Magufuli na Rais mteule wa Marekani,
Donald John Trump na kubainisha kuwa mabadiliko katika nchi za Afrika yataletwa
na wananchi wa nchi husika.
Pia, wachambuzi hao wamebainisha kuwa kiongozi
wa nchi nyingine hawezi kuhoji kuvunjwa kwa demokrasia na utawala bora katika
nchi ambayo wananchi wake wako kimya kuhusu jambo hilo.
Aidha, wadau hao wa siasa waliozungumza
katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Star Tv jana asubuhi na wengine
kuhojiwa na gazeti hili, walisema Marekani ina cha kujifunza katika demokrasia
kutoka Tanzania na kuwataka watawala wa Afrika wanaokiuka misingi ya demokrasia
na utawala bora kujipanga kwa maelezo kuwa Marekani chini ya Trump, inaweza
kuwaumbua.
“Hawa (Magufuli na Trump) wanafanana kwa
misimamo. Rais Trump anasema nchi za Afrika hazina sababu ya kupewa misaada kwa
sababu zina rasilimali nyingi,” alisema mchambuzi Kheri James wa jijini Mwanza.
James ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuia
ya Vijana ya CCM (UVCCM) wilayani Ilemela alisema Rais Magufuli anafanana na
Trump kwa kuwa na misimamo, akisimamia anayoamini hasa anaposema hakuna sababu
ya kuwa ombaomba wakati Tanzania ina rasilimali nyingi.
Alisema katika hotuba zake mbalimbali
wakati wa kampeni, Trump alieleza misimamo yake kuhusu Bara la Afrika kwamba
lina watu wavivu na rais Magufuli amekuja na falsafa ya kutaka watu wafanye
kazi.
“Magufuli ni Trump mstaarabu,” alisema
James ambaye katika mahojiano hayo ya TV, alikuwa na Dotto Ismail wakizungumza
kutoka Mwanza, Dk. Onesmo Kyauke wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na Dk. Dustan Matungwa anayesoma Chuo Kikuu cha Rutgers nchini Marekani
wakizungumza kutokea Dar es Salaam.
Akizungumzia mfumo wa demokrasia wa
Marekani, Dk. Matungwa alisema licha ya kukubalika na kutumika kwa miaka mingi,
huku taifa hilo likiheshemika duniani,
lakini bado inaweza kujifunza kutoka Tanzania.
Alisema kimfumo, licha ya wananchi
kupiga kura kuchagua Rais wa nchi hiyo kama walivyofanya Novemba 8, lakini kura
zinazomweka madarakani kiongozi wa taifa hilo zinapigwa na watu wachache.
Wakizungumza na JAMBO LEO kwa nyakati
tofauti, mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema,
“kauli za Magufuli na mwelekeo wake kwamba Tanzania iwe nchi inayojitegemea si
ngeni, ni kauli ambayo tumeanza kuiimba tangu uhuru. Nyerere (Julius-Rais wa
Awamu ya Kwanza) mara nyingi alituonya juu ya kutegemea wahisani na misadaa ya
nchi za nje na alisema ni hatari kwa uhuru wa nchi.”
“Rais yeyote anayekuja akiwa na dhamira
ya kutuondoa kwenye utegemezi na kutufanya tuwe na uhuru zaidi kiuchumi ni
jambo jema.”
Alisema kauli za Rais Magufuli kuitaka
Tanzania iwe nchi inayojitegemea ni jambo zuri kwa wahisani wa Marekani, kusisitiza
kuwa kauli nyingi za Trump kuhusu Afrika na uongozi wake ni kauli zenye ukweli
ndani yake.
“Nchi nyingi Afrika zimefikisha miaka 50
tangu zipate uhuru, lakini tunashuhudia viongozi wake hawafuati taratibu za
utawala bora, baadhi yao wanakaa madarakani muda mrefu, familia zao zinakuwa na
mali isiyoelezeka, wanatibiwa na kusomesha nje,” alisema.
Alisema kiongozi wa Marekani, taifa
kubwa duniani akakemea mambo hayo na kuwa tayari hata kuminya misaada pale
inapobidi ni ujumbe tosha kwa viongozi wa Afrika kujisahihisha.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha,
Profesa Gaudence Mpangala alisema, “mfano Marekani imezuia misaada Zimbabwe ili rais wa nchi hiyo abadili sera
zake na inawezekana chini ya Trump, shinikizo kwa nchi hiyo na nyingine Afrika
ikawa kubwa zaidi.”
“Nchi zote za Afrika ni huru, lakini
haziwezi kuingiliwa katika kila jambo kama ambavyo Trump anavyodai. Aliwahi
kusema Mugabe (Robert-Rais wa Zimbabwe)
na Museven (Yoweri-Rais wa Uganda) atawafunga. Sasa atawafunga kwa
kigezo gani. Hilo haliwezekani, nadhani kauli zake zinalenga kukosoa watawala
wa Afrika.”
Alisema tatizo la nchi nyingi za Afrika
ni kutoheshimu demokrasia, huku kiongozi mkuu wa nchi akiwa na madaraka makubwa
kutaka Tanzania kubadilika kwa maelezo kuwa hivi sasa nchi haijulikana ipo
katika ujamaa au uliberari.
“Tunahitaji mabadiliko ambayo yanaweza
kuletwa na wananchi wenyewe, ila si kwa mtindo anaouzungumzia Trump,” alisema
Profesa Mpangala.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Profesa Mwesiga Baregu na kusisitiza
kuwa mabadiliko katika nchi za Afrika, yataletwa na waafrika wenyewe.
“Amesema (Trump) wanaong’ang’ania
madarakani hatakuwa na uvumilivu nao…,unajua demokrasia inajengwa na watu
wenyewe katika nchi zao pamoja na kwamba kuna mazingira ya kimataifa yanayoweza
kuwezesha au kudhoofisha,” alisema.
Alibainisha kuwa Watanzania ndiyo wenye
wajibu wa kujenga demokrasia nchini, huku akitolea mfano jinsi wengi wao
wanavyokaa kimya licha ya kuibuka kwa matukio yanayokiuka Katiba ya nchi na
sheria mbalimbali.
“Mikutano ya hadhara imezuiwa ila
watanzania wapo kimya, watu wanakamatwa bila sababu za msingi ila watanzania
wamekaa kimya. Hakuna aliyesemamambo hayo si sawa, wapo kimya! Tunapaswa
kusimama kwa sauti kutetea misingi ya demokrasia,” alisema.
Alisisitiza kuwa misingi ya demokrasia
katika nchi yoyote inaanzia katika nchi husika, “awe Trump au nani, akiwakuta
na jambo lenu atawasaidia, ila kama hamna mwinuko wa kuilinda demokrasia, hiyo
itakuwa ni shida.”
0 comments:
Post a Comment