Sharifa Marira
CHAMA cha Act-Wazalendo, kimeeleza
kushangazwa na taarifa ya Serikali kwamba wananchi walioathirika na tetemeko la
ardhi mkoani Kagera wajitegemee wenyewe na kwamba michango iliyopatikana ni ya Serikali
na taasisi zake.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali
Salum Kijuu, aliwaeleza waandishi wa habari kwamba fedha zilizochangwa
zitatumika katika ukarabati wa taasisi za Serikali zilizoharibika na kwamba
endapo michango mingine itapatikana itasaidia wazee na walemavu, hivyo wananchi
wengine wajisaidie wenyewe.
Taarifa iliyotumwa na Katibu wa Kamati
ya Maendeleo ya Jamii wa ACT-Wazalendo, Janeth Rithe kwa vyombo vya habari
ilieleza kuwa chama hicho kimeshtushwa
na kauli hiyo ambayo haiikubali, kwani inadhalilisha waathirika na watu wote
waliojitoa kuwasaidia.
“Tunachukulia kauli hii kama tangazo la
wizi wa uaminifu wa wananchi waliochanga. Ni busara ya kawaida kuwa hatua ya
kwanza katika kushughulikia maafa ni kurudisha hali ya maisha ya watu katika
hali ya kawaida sambamba na ukarabati wa miundombinu,” alisema Rithe.
Alieleza kuwa suala la ujenzi wa
miundombinu ya taasisi za umma ni jukumu la msingi la serikali na siyo kutumia
fedha zilizochangwa kuchangia wananchi .
“Kufuatia wizi huu ACT Wazalendo
tunaitaka serikali kuu kujitenga na kufuta kauli ya kiongozi huyo kwa sababu
inaigombanisha serikali na wananchi inaowaongoza,”alisema Rithe
Alisema pia kuwa chama hicho kinaitaka Serikali kuelekeza misaada iliyopatikana kwa michango ya
wananchi, taasisi na nchi rafiki katika kusaidia wananchi walioathirika kurudi
katika maisha ya kawaida, ikiwemo ukarabati na ujenzi wa nyumba za kuishi.
Alitoa wito kwa taasisi za kiraia nchini kuchukua nafasi yake katika kuendelea
kuikumbusha serikali wajibu wake wa msingi wa kuboresha maisha ya watu.
Septemba 10 mwaka huu lilitokea tetemeko
la ardhi katia mkoa huo na kusababisha athari mbalimbali zikiwemo vifo, majeruhi,
uharibifu wa makazi na miundombinu ya umma na watu binafsi.
Jumla ya watu 117,721 waliathirika katika
tetemeko hilo kwa kupoteza makazi yao, mali na athari za kisaikolojia katika
Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa, huku watu 17 wakipoteza
maisha na 560 kujeruhiwa.
Katika tukio hilo nyumba 2,072 za makazi
zilianguka nyingine 14,595 za makazi zilibomoka baadhi kuta nyingine kupata
nyufa kubwa hivyo kuzifanya kuwa hatarishi kwa makazi ya binadamu.
Maafa hayo yalisababisha uharibifu
mbalimbali wa miundombinu ya barabara na majengo ya watu na taasisi mbalimbali,
ikiwemo shule na hospitali.
Hata hivyo, kufuatia maafa hayo
wananchi, taasisi, nchi marafiki, waliitikia wito wa kuwasaidia wahanga na kukarabati
miundo mbinu iliyoharibika na zaidi ya bilioni tano zilipatikana.
0 comments:
Post a Comment