Grace Gurisha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
imewahukumu kifungo cha miezi mitatu jela, raia 107 wa Malawi au kulipa faini
ya Sh milioni moja kila mmoja huku ikielekeza kuwa watakapomaliza adhabu hiyo warudishwe
kwao mara moja.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Victoria
Nongwa, baada ya washitakiwa hao kusomewa mashitaka mawili na kukiri kuingia
nchini na kuishi bila kibali cha
Serikali.
Hakimu Nongwa alisema mshitakiwa wa kwanza hadi wa tatu
Jessy Phiri (29), Saulos Lohane (43) na Jungu Kaunda watatakiwa kulipa faini
ya Sh 500,000 kila mmoja kwa sababu walikutwa
wakiishi nchini bila kibali.
Kabla ya hakimu kutoa hukumu hiyo, washitakiwa hao
waliomba wapunguziwe adhabu, lakini Hakimu Nongwa alisema adhabu aliyotoa kwao
ni ndogo hivyo hawezi kushuka zaidi ya hapo kutokana na kwamba sheria kuhusu
makosa hayo iko bayana.
“Washitakiwa mmepatikana na hatia kwa hiyo mtatumikia
kifungo cha miezi mitatu jela au kulipa faini, mshitakiwa wa kwanza hadi wa tatu
watalipa faini ya Sh 500,000 kila mmoja na mshitakiwa wa nne hadi wa 107 kila
mmoja atalipa Sh milioni moja na mtakapomaliza kutumikia adhabu hii Serikali
iwarudishe kwenu mara moja,” alisema Nongwa.
Awali, akisoma hati ya mashitaka, Mwendesha Mashtaka wa
Idara ya Uhamiaji, Method Kagoma alidai kuwa Novemba 12 washitakiwa hao wakiwa
Kinondoni Shamba, Dar es Salaam wakiwa raia wa Malawi walikutwa nchini bila viza.
Pia katika tarehe hiyo hiyo na eneo hilo hilo, washitakiwa
wa kwanza, wa pili na wa tatu, walikutwa wakiishi nchini bila kibali wala hati
za kusafiria huku wakijua ni kosa kisheria.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa, washitakiwa hao waliangua
vilio kwa kutojua la kufanya kwa sababu wote wako ndani.
Washitakiwa hao walikuwa na watoto wengi hali ambayo
iliwafanya waendelee kulia kwa madai kuwa hawajui hatima ya watoto wakati wao
wakiwa gerezani.
0 comments:
Post a Comment