Fidelis Butahe
Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump |
WASOMI nchini wameuchambua mfumo wa
uchaguzi wa Marekani wakieleza kuwa licha ya kuwapo kikatiba unaweza
kutafsiriwa kuwa unawanyima haki wananchi, huku wakibainisha sababu za wananchi
kuandamana kumpinga Rais mteule wa Taifa hilo, Donald Trump.
Wamesema katika mfumo huo, mgombea
atatangazwa mshindi iwapo atapata kura nyingi za uwakilishi, hata kama atakuwa
ameshindwa katika kura za kawaida zinazopigwa na wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na
gazeti hili, wamesema kati ya majimbo 50 ya nchi hiyo, yapo makubwa zaidi, yenye
nguvu ya kiuchumi na idadi kubwa ya watu, jambo ambalo ni msingi kwa mgombea
kupata kura nyingi za uwakilishi iwapo
atakubalika zaidi katika maeneo hayo.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Novemba
8 na matokeo kutangazwa juzi, Trump alipata kura za kawaida 59,441,779 huku
mpinzani wake, Hillary Clinton akipata 59,649,308.
Katika matokeo hayo, Clinton alishinda
kwa tofauti ya kura 207,529, lakini katika kura za uwakilishi, Trump alipata
279, Clinton 228, ikiwa ni tofauti ya
kura 51.
“Marekani kila jimbo lina hadhi, kura za
uwakilishi ni 538 na kila jimbo lina kiwango chake cha uwakilishi kulingana na
sababu mbalimbali. Mfano Tanzania katika uchaguzi, mkoa wa Singida na mkoa wa Dar
es Salaam ambao ndio kitovu cha uchumi wa nchi, yote ina haki sawa, ila
Marekani hakuna kitu kama hicho,” alisema Dk Benson Bana, Mhadhiri wa Chuo
Kikuu Dar es Salaam (UDSM).
“Hizi kura 538 za uwakilishi wanazigawa
mara mbili, zinakuwa 269 kwa 269. Ili mtu ashinde inategemea ameshinda katika
jimbo lipi na lina uzito upi kulingana na vigezo walivyoweka. Kura hizi
hujumlishwa na anayepata zaidi ya 270 lazima atangazwe mshindi. Iwapo watapa
kura sawa, utatafutwa utaratibu mwingine.”
Alisema utaratibu huo wa Marekani si
mbaya, huku akikosoa utaratibu wa Tanzania wa kuwapa wabunge wote haki sawa,
hata kama mmoja kachaguliwa na wananchi 200,000 na mwingine 6,000.
Dk Bana alisema licha ya kasoro hiyo,
Tanzania bado ni nchi ndogo na ina idadi ndogo ya watu, hivyo haipaswi
kujielekeza kwenye utaratibu huo wa Marekani.
Kuhusu baadhi ya wananchi waliojitokeza
kumpinga Trump mitaani, Dk Bana alisema, “hayo ni mambo ya kawaida kwenye siasa
za uchaguzi, hao wanaoandamana ni wanaojua kwamba wataathirika na msimamo wa Trump,
unaandamana vipi wakati uchaguzi umeendeshwa kwa misingi ya uhuru na haki na
Clinton kakubali kushindwa?”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino
(Saut), Profesa Mwesiga Baregu alisema: “Uchaguzi wa Marekani mwaka 2000, kati
ya George Bush na Albert Gore, Gore alishinda kura za kawaida na kulizuka
mvutano kabla ya Mahakama kuingilia kati.
“Uchaguzi wa mwaka huu hakuna
aliyelalamika, ndiyo maana hali imekuwa shwari. Marekani ni shirikisho na wana
mabunge mawili, la Seneti na la uwakilishi, hata kwenye urais inakuwa hivyo.
Marekani, majimbo kama majimbo yana maslahi kuhusu urais, vilevile wananchi nao
wana maslahi yao.”
Profesa Baregu ambaye alikuwa mjumbe wa
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema mfumo huo unataka kufanana kiasi
na mapendekezo yaliyokuwa kwenye rasimu ya Tume hiyo ya kuwa na Bunge la
Tanganyika, Zanzibar na la Muungano linalojitegemea.
Alisema Marekani walitanguliza maslahi
ya majimbo, ili rais aamuliwe kwa kura za uwakilishi na za wananchi zifuate
baadaye.
“Unaweza kusema mfumo wao si sawa na
hauheshimu haki za watu, lakini wao wameona mfumo huo ni sahihi,” alisema.
Kuhusu maandamano yaliyoanza kuitia doa
nchi hiyo, alisema idadi kubwa ya Wamarekani walitarajia ushindi kwa Clinton,
jambo ambalo halikutokea na ndiyo sababu ya maandamano hayo.
0 comments:
Post a Comment