Grace Gurisha
TAASISI ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (Cegodeta)
imemwandikia barua ya wazi Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu
kupanda kwa bei ya umeme, wakiwaomba waipunguze kwa asilimia 20 badala ya kuongeza
kwa asilimia 18.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Cegodeta,
Thomas Ngawaiya alisema walifikia hatua hiyo ya kuandika barua ya wazi kutokana
na tangazo la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) la kuongeza bei ya umeme na
pia walipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kutokana na kwamba umeme
ukipanda watayumba kiuchumi.
Alisema wanaiomba Serikali kusitisha mpango huo, kwa
sababu awali ilisema mara tu gesi itakapoanza kutumika, umeme utashuka bei kwa
lengo la kunufaisha wananchi wa hali zote, vipi leo wabadilishe kauli yao
ambayo waliitoa wanataka wananchi wakimbilie wapi.
“Ili kukuza uchumi ni lazima kupata nishati ya umeme tena
wa uhakika, kama tunalipa kodi ili kuharakisha maendeleo, ni lazima kodi hiyo
isaidie katika jambo hili.
“Tukumbuke kuwa umeme unachochea maendeleo, kwani huwezi
kuendesha viwanda bila nishati hiyo, hivyo kuna haja ya kusitisha mpango huo,” alisema
Ngawaiya.
Mkurugenzi huyo alisema Cegodeta imeona kuwa badala ya
Serikali kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 18 ishushe kwa asilimia 20 na
hapo baadaye iendelee kushusha kadri ya nyongeza kwenye mapato ya gesi asilia
inavyojiri.
Pia alisema mchumi anayeishauri Serikali vitu muhimu
vipande bei badala ya kushuka ili watumie wananchi wote ni mwangamizaji, kwa
sababu bila umeme uchumi wa nchi utadorora, kwa hiyo kwa sababu Waziri Mkuu
ndiye mtendaji wa masuala hayo, Rais amepelekewa nakala.
0 comments:
Post a Comment