*Ni baada ya kuvuka milima na mabonde ya kampeni
*Atumia
maneno kama ya Magufuli akikubali ushindi
Suleiman Msuya
Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump |
LICHA ya kupitia changamoto mbalimbali
hata kukataliwa na baadhi ya vigogo ndani ya chama chake, mgombea wa Republican,
Donald Trump ameiduwaza dunia baada ya kuibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa
Marekani uliofanyika juzi.
Katika muktadha huo huo, Rais huyo
mteule wa Marekani wakati akitangaza kukubali ushindi wake huo dhidi ya Hillary
Clinton wa Democrats, alitumia maneno kama ya Rais John Magufuli.
Katika uchaguzi huo, Trump alimshinda
mpinzani wake huyo kwa kupata kura 289 za majimbo sawa na asilimia 48.2 dhidi
ya Clinton aliyepata kura 218 sawa na asilimia 47.1 katika majimbo 50 ya
uchaguzi huo uliosimamisha dunia.
Ushindi huo wa Trump, umekuja baada ya
kupitia misukosuko mingi kwenye kampeni za uchaguzi huo, zilizokuwa za vuta
nikuvute huku mgombea huyo akionekana kuwa katika hali mbaya kwa kupingwa hata
na baadhi ya watu maarufu ndani ya Republican.
Hatua hiyo ilipata kusababisha chama
hicho kifikirie kubadili mgombea katikati ya kampeni kwa kuhofia kushindwa na
Clinton ambaye awali alipewa nafasi kubwa kutwaa ushindi.
Muda mfupi baada ya matokeo yanayomfanya
Trump kuwa Rais wa 45 wa Marekani, Clinton alimpigia simu kumpongeza kwa
ushindi.
Baada ya hapo alipanda juukwaani kwenye
makao makuu yake ya kampeni jijini New York, na kutoa hotuba ya ushindi
akitumia maneno kama yaliyotumiwa na Rais Magufuli alipotangazwa mshindi katika
Uchaguzi Mkuu, uliofanyika Oktoba mwaka jana.
Trump alisema: “Uchaguzi umekwisha, mimi
ni Rais wa Wamarekani wote, sasa tufanye kazi kujenga Marekani mpya, naahidi
sitawaangusha.”
Alisema Clinton alimpa ushindani mkubwa
lakini sasa ni wakati wa yeye kutumia maarifa yake kibiashara kuongoza Taifa
hilo kubwa ili lipate maendeleo.
Trump alisema mipango yake ni kulinda
wastaafu, kuboresha na kujenga miundombinu aliyoielezea kuwa imeonesha kuchoka akiahidi
pia kuboresha uhusiano wa kimataifa.
Katika uchaguzi huo ambao ulikuwa na
ushindani Trump alishinda majimbo mengi muhimu ya Ohio, Florida, North
Carolina, Alabama, Kentucky, South Carolina, Nebraska, Indiana, West Virginia,
Mississippi, Tennessee, Oklahoma na Texas ingawa Clinton alishinda Virginia.
Aidha, Trump alishinda majimbo mengi ya
Kusini mwa Marekani na Clinton akashinda ya Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo,
kwa mujibu wa makadirio ya Shirika la Utangazaji la ABC.
Chama cha Republican pia kilipata wingi
wa wabunge katika Bunge la Wawakilishi.
Baada ya Clinton kumpigia simu Trump kumpongeza
kwa ushindi, Trump naye alimpongeza mshindani wake huyo kwa uamuzi huo na kusema
alionesha ukomavu wa kisiasa.
Obama
Kwa ushindi huo, Rais Barack Obama naye alimpigia
simu kumpongeza kwa ushindi ambapo pia alimwalika Ikulu ya White House kesho
ili wajadiliane masuala mbalimbali.
Obama pia alimpigia Clinton na
kumpongeza kutokana na alivyofanya kampeni.
Watanzania
Akizungumzia uchaguzi huo, Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk George Kahangwa alisema
ushaguzi huo unapaswa kuwa fundisho kwa vingozi wa nchi za Afrika aliosema wamekuwa
wagumu kuondoka madarakani hata wakishindwa.
Alisema uchaguzi huo umeonesha misingi
ya demokrasia, kwani hakukuwa na mazingira yoyote ya kuwanyima haki wananchi,
hivyo kuheshimu uamuzi wao.
Dk Kahangwa alisema Trump alikuwa muwazi
hali iliyojenga imani kuwa wananchi hawatamwunga mkono lakini wameonesha kuwa
walikuwa naye.
Dk Frank Tily pia wa UDSM, alisema
Wamarekani wanaamini Trump ataleta mabadiliko katika nchi hiyo, hivyo wanapaswa
kupongezwa kwa uamuzi huo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba aliwapongeza Wamarekani huku akibainisha kuwa
bado jamii haijawa na imani na mwanamke katika uongozi.
Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo
ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema wanampongeza Rais mteule Trump, kwa
hotuba yake ya awali kwa kuahidi kuwa Rais wa wote.
“Ushindi huu ni ushindi wetu sote
wanachama wa Jumuia ya Kimataifa ya Kidemokrasia (IDU), hivyo tunatuma salamu
nzito kwa madikteta popote walipo, kuwa utawala mpya wa Marekani hautavumilia kuona
demokrasia na haki za binadamu zinaminywa,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema kilichotokea
Marekani ni cha kupongezwa pamoja na kuwa anaona Marekani ya malalamiko
ikirejea kutokana na ahadi za Trump kwenye kampeni.
Mtatiro alisema Trump aliahidi kuondoa
sheria zilizoanzishwa na Obama za kutoa huduma kwa jamii, hivyo upo uwezekano
wa wananchi hasa wa kipato cha chini kuanza kuumia.
“Ni jambo la kupongeza, kwani wananchi
wa Marekani wameamua, nadhani Afrika na Tanzania ikiwamo tunapaswa kujifunza
kilichotokea hata kama hatupendi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment