Suleiman Msuya
Dk. Magufuli na wahariri wa vyombo vya habari |
WAHARIRI wameeleza kufurahishwa na hatua
ya Rais John Magufuli kuzungumza nao kwenye mkutano maalumu na kumwomba
aendeleze utaratibu huo ili kukuza uhusiano baina yao na Serikali
Wakati wahariri wakionesha kufurahishwa huko,
Wakfu wa Tasnia ya Habari Tanzania (TMF), umesema uko tayari kuandaa mkutano wa
waandishi wa habari na Rais John Magufuli wakati wowote Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), litakaporatibu mkutano huo.
Wahariri hao walisema hayo jana siku 11
tangu Rais afanye nao mkutano Ikulu, Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho
ya mwaka mmoja akiwa Ikulu.
Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga
alisema mkutano huo uliendeshwa vizuri pamoja na kasoro zilizojitokeza, lakini
bado Rais anapaswa kupongezwa kwa juhudi alizofanya za kukutana nao.
Alisema kimsingi walishitukizwa hali
ambayo inaweza kuwa sababu ya baadhi ya watu kufikiria kuwa hawakujiandaa kwa
maswali.
Katibu wa TEF, Neville Meena alisema TEF
ilipata taarifa za mkutano asubuhi ya siku hiyo huku wakiwa Dodoma
kushughulikia Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari.
“Pamoja na kuchelewa kwa taarifa pia
nakumbuka kuwa walitangaza kuwa maswali yataulizwa na watu wawili waendeshaji,
hivyo tumejifunza siku nyingine nadhani mambo yatakuwa sawa,” alisema.
Mhariri Msanifu Mkuu wa JAMBO LEO,
Joseph Kulangwa alisema kilichotokea katika mkutano huo, ni ishara tosha kuwa
hakukuwa na maandalizi mazuri hivyo kinachopaswa sasa ni kujipanga kwa wakati
mwingine.
Jane Mihanji wa Uhuru alisema pamoja na
changamoto ambazo zilioneshwa na waandaaji waandishi wanapaswa kujipanga
kulingana na mazingira husika.
Mhariri wa Mwanahalisi, Jabir Idrisa
alisema wakati mwingine mikutano kama hiyo ya Rais inakosa mvuto kutokana na
aina ya waongozaji kwa kubagua wauliza maswali.
“Wakati mwingine tunapaswa kujipanga
kwani kuna waandaji ambao wanachagua watu wa kuwapa kipaza sauti hali ambayo
inajenga chuki, hivyo bila ujanja unaweza unyooshe kidole mpaka mkutano unakwisha
hujauliza swali,” alisema.
Mhariri wa Raia Mwema, Ezekiel Kamwaga
alitoa mwito kwa waandishi na wahariri kusoma muktadha ili kukabiliana na mtu
ambaye watakuwa wanamwuliza maswali wakipata nafasi.
Aidha, wahariri na waandishi hao walimwomba
Rais kuandaa utaratibu wa kuzungumza na Taifa kila miezi mitatu, kuwapo mawasiliano
mazuri kati ya pande mbili hizo na vyombo vya habari viangalie uwezekano wa
waandishi kubobea katika fani mbalimbali ili kuuliza maswali yenye tija.
Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura
akifunga mjadala huo alisema baada ya kufanyika kwa mkutano huo na kupitia
maoni ya wadau, TMF iliamua kuwakutanisha wahariri na waandishi hao kutathmini
mkutano huo ambao uliibua maswali mengi.
Alisema mkutano huo ulionesha dhahiri upungufu
kwenye maandalizi hali ambayo ilichangia wananchi kutoridhishwa na maswali na
majibu yaliyotolewa hali ambayo iliwasukuma TEF kuandaa mkutano ambao TMF
itafadhili.
0 comments:
Post a Comment