Abraham Ntambara
Dk Charles Msonde (katikati) |
BARAZA la Mitihani Tanzania (Necta) limesema wanafunzi
435,221 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha pili ulioanza jana nchini
kote.
Aidha limesema wanafunzi 1,045,999 wamesajiliwa kufanya
upimaji wa darasa la nne ambao unatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 23 mwaka
huu.
Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk. Charles Msonde
alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa upimaji huo wa kidato cha pili ulioanza
jana unatarajiwa kukamilika Novemba 25.
“Maandalizi yote kwa ajili ya upimaji huo yamekamilika,
pamoja na kusambazwa kwa mitihani itakayotumika katika upimaji huo na nyaraka
zote muhimu kwenye mikoa na halmashauri zote Tanzania Bara,”alisema Msonde.
Alisema idadi ya shule za sekondari ambazo wanafunzi wana
vigezo vya kufanya upimaji huo ni 4,669 wakati shule za msingi 17,032 ndizo
zitakazoshiriki mtihani wa darasa la nne.
Msonde alisema kati ya wanafunzi waliosajiliwa kufanya
upimaji wa kidato cha pili, wavulana ni 214,013 sawa na asilimia 49.17 na wasichana
ni 221,208 sawa na asilimia 50.83.
Alifafanua kwamba watahiniwa 67 ni wasioona na watahiniwa
wenye uoni hafifu ni 306 ambao maandishi ya karatasi zao za mitihani hukuzwa,
akibainisha kuwa kwaka jana waliosajiliwa walikuwa 396,770, hivyo kuna ongezeko
la watahiniwa 38,451 (9.7%) wa kidato cha pili kwa mwaka huu.
Katibu huyo mtendaji alisema wanafunzi wavulana watakaofanya
upimaji wa darasa la nne ni 507,732 sawa na asilimia 48.54 na wasichana 538,267
sawa na asilimia 51.46 ambao utafanyika katika jumla ya shule 17,032.
Msonde aliongeza kwamba mwaka jana kulikuwa na watahiniwa
1,037,305 ikilinganishwa na mwaka huu hivyo kuwa na ongezeko la watahiniwa
8,694 sawa na asilimia 0.8% katika upimaji wa Darasa la Nne.
Alizitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na halmashauri
kuhakikisha taratibu zote za upimaji zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha mazingira ya vituo yapo salama, tulivu na kuzuia mianya inayoweza
kusababisha udangavyifu.
Pia aliwataka wasimamizi wote kufanya kazi yao kwa
umakini na uadilifu wa hali ya juu ambapo wameaswa kujiepusha na vitendo vya
udanganyifu kwani Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote atakaebeinika kukiuka
taratibu za uendeshaji wa upimaji wa kitaifa.
Alisema wanaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri wanafunzi
wao, hivyo matarajio ni kwamba watafanya upimaji kwa kuzingatia taratibu zote
ili matokeo yaonyeshe uwezo halisi kulingana na maarifa na ujuzi waliopata
ambapo aliwaomba wadau kutoa taarifa watakapo baini uwepo wa udanganyifu.
0 comments:
Post a Comment