Abraham Ntambara
WAKATI keshokutwa Rais John Magufuli akitimiza
mwaka mmoja madarakani, baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamemwomba
aendelee kutilia mkazo uwekezaji wa viwanda na kutatua tatizo la mikopo kwa wanafunzi
wa elimu ya juu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na
JAMBO LEO, walisema sehemu hizo Rais anatakiwa kuziangalia na kuzipa kipaumbele
kwa manufaa ya Taifa katika kufanikisha kuwa na wasomi wengi na maendeleo ya
kiuchumi.
Mecky Mzenga alisema kwa kuwa dhamira
yake tangu kampeni na hata baada ya kuingia madarakani amekuwa akihubiri kuhusu
viwanda anatakiwa kuelekeza nguvu kwenye uwekezaji wa viwanda nchini.
“Vijana wengi hawana ajira, kwa sababu
sekta zinazoajiri ni chache ikilinganishwa na wahitaji, kwa maana hiyo
anatakiwa kutilia mkazo hilo ili kupunguza ukosefu wa ajira nchini,” alisema
Mzenga.
Jamila Hamduni alisema kama viwanda
vitakuwapo na ajira zikapatikana, zitasaidia pia kuondoa tatizo la ombaomba
nchini kwa kuwa watu watakuwa wakijipatia kipato na kuendesha maisha yao vizuri
bila utegemezi.
“Hii itasaidia kuondoa ombaomba mitaani
na namwombea afanikiwe katika hilo,” alisema Jamila.
Rashid Hamisi alimwomba Rais aangalie
changamoto zinazokabili wanafunzi wa elimu ya juu hususan katika mikopo ambapo
alikumbusha kuwa kipindi cha kampeni na baada ya kuchaguliwa, alisisitiza kuwa
haitakuwa inacheleweshwa.
“Rais aliahidi suala la mikopo kwa
wanafunzi wa vyuo vikuu haitakuwa ikicheleweshwa, lanini kwa sasa tunaona
changamoto hiyo, kwa maana hiyo anatakiwa kulifanyia kazi ili lisijirudie,” alisema
Hamisi.
Hamisi alisema pia katika mikopo
anatakiwa kuagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HSLB) kufanya tathmini ya
wanafunzi wanaoomba mikopo ili
kuhakikisha wanaostahili wanapata.
Aidha, walimpongeza kwa uongozi wake
wenye mtazamo wa kujali watu wa hali ya chini na jinsi ya utafutaji wao wa
kipato ambapo wafanyabiashara kama Wamachinga ambao walikuwa kipindi cha nyuma
wakinyanyaswa sana, kwa sasa hali hiyo imepungua.
0 comments:
Post a Comment