Wabunge walia ukata serikalini


Mwandishi Wetu, Dodoma

WABUNGE wamesema Serikali ina ukata kutokana na wao kushindwa kuhudhuria vikao vyote vya wabunge wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe akizungumzia hali hiyo kwenye mahojiano maalumu jana, alisema ukata umefikia hatua ya kugeuza Bunge kuwa sawa na kisiwa.

Alisema ukosefu wa fedha umesababisha safari ambazo ni za muhimu kwa wabunge nje ya nchi akitolea mfano mikutano ya SADV kuzuiwa.

“Hata muda wa shughuli za Bunge umefupishwa, kwani ukiangalia katika hali ya kawaida huwa tunajadili Mpango wa Maendeleo wa Taifa, kwa siku tano lakini Bunge hili jambo zito kama hilo linajadiliwa kwa siku tatu, tunajaribu kuhoji kulikoni, kumbe hakuna fedha,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, suala la ukata lilijitokeza kwa mara nyingine kwa wabunge mwanzoni mwa wiki walipokutana kwenye kikao elekezi ambapo bila kujali tofauti zao za kiitikadi, waliitolea macho Serikali wakitaka kujua hatima ya wananchi ‘kufungishwa mikanda’ kwa lazima.

Wabunge hao waliieleza Serikali kuchoshwa na vilio vya wananchi vinavyotokana na ukosefu wa fedha.

Taarifa kutoka kwa mmoja wa wabunge aliyehudhuria kikao hicho zilisema walizungumzia mengi kila mtu bila kujali wadhifa wake, taasisi na hata mihimili ya Bunge likiwamo suala la Bunge kukosa fedha ambalo lilitawala kikao, katika hilo “sote tulishikamana dhidi ya Serikali, tukitaka hali hii itafutiwe ufumbuzi.”

Chanzo hicho kilisema mnyukano wa kimitazamo kuhusu hali mbaya ya uchumi, ulihitimishwa kwa Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, kutakiwa kutoa kauli ya Serikali  bungeni juu ya hatima ya ukata nchini wakati akihitimisha mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa kuandaa mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/18 leo.

Wakati wakichangia Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2017/18 wabunge walielezea ukata kuwa upo kwao, kwani walipata tabu hata kwenye vikao vya kamati vilivyofanyika kwa wiki mbili mjini hapa.

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) alisema kipindi cha kamati wabunge walikuwa wanashindia maji madogo kutwa nzima na ikifika muda wa chai, mhudumu alikuwa akiangalia Mbunge asije akachukua vipande viwili vya  nyama kutokana na ukata.

Mbunge wa Busega, Dk Raphael Chegeni (CCM) alisema haki za wabunge zinapaswa kuzingatiwa, kwa sababu wanataka kufanya kazi na hakuna anayeweza kufanya kazi bila fedha.

Alisema ingawa hawezi kupinga taarifa za Serikali kwamba uchumi unakua, kwa sababu tarakimu haziongopi hali halisi inadhihirisha hali ya uchumi wa kila mtu ni mbaya.

“Serikalini hakuna fedha, watu hawana fedha, yaani hakuna mtu anayeweza kusema ana fedha kwa kiwango cha kuwa na uchumi bora, Serikali itimize wajibu, ihakikishe taarifa zake za hali ya uchumi zinarandana na hali halisi ya maisha ya watu,” alisema.

Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum (CCM) alisema wabunge walilia ukata kwenye kikao chao cha mwanzoni mwa wiki na kwamba hali waliyonayo wananchi wanalia zaidi.

Mkutano wa Tano wa Bunge ulianza Novemba mosi na unaratajiwa kuahirishwa Novemba 11. Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilila, alisema muda wa shughuli za Bunge upo kama inavyotakiwa.

“Hakuna mkutano wa Bunge unaofanyika kwa wiki mbili, ila ndani ya wiki mbili, huwa kuna vikao visivyopungua tisa na ndiyo muda wa Mkutano huu,” alisema Dk Kashilila.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo