Joyce Kasiki, Dodoma
Profesa Joyce Ndalichako |
JESHI
la Polisi mkoani hapa linashikilia walimu watatu wa sekondari wilayani Kongwa kwa tuhuma za kuzuia
wanafunzi wawili wa kidato cha nne kufanya mtihani wa Taifa ulioanza Novemba
mosi.
Akizungumzia tukio hilo jana Kamanda wa
Polisi wa Mkoa, Lazaro Mambosasa alisema walimu hao walizuia wanafunzi hao
kufanya mtihani wa Kiingereza.
Wanafunzi waliozuiwa kufanya mtihani huo
ni Amina Said wa sekondari ya Zoissa na Bahati Ntigonza wa sekondari ya Mnyakongo.
Mambosasa alisema Amina alizuiwa kwa
kuhofiwa ana ujauzito na walimu hao wakaamuru akapimwe ujauzito wakati wenzake
wakiendelea na mtihani ambapo hata hivyo majibu yalionesha hakuwa na ujauzito.
Bahati alizuiwa kuingia chumba cha mtihani
kwa kuwa alivaa viatu visivyo na gidamu, hivyo alirudishwa nyumbani kufunga gidamu
huku wenzake wakiendelea na mtihani.
Kamanda Mambosasa alitaja watuhumiwa hao
kuwa ni Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Mnyakongo, Lukonge Mwezo, Mkuu wa Sekondari
ya Zoisa, Omari Athumani na mwalimu wa zamu wa Sekondari ya Mnyakongo Daud John.
Aidha alisema upelelezi utakapokamilika
walimu hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kamanda huyo alitoa rai kwa walimu wote
wanaosimamia mitihani kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Baraza la
Mitihani (NECTA) kwani walichokifanya walimu hao hakikustahili kwa kipindi hiki
cha mtihani.
Alisema Polisi haitasita kuwachukulia
hatua za kisheria watakaokiuka taratibu zilizowekwa katika kazi hiyo ya
kusimamia mitihani.
Baada ya kukamatwa kwa walimu hao,
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Kongwa, Andrew Nyemba
alitaka kuzingatiwa kwa taratibu, sheria na kanuni katika kushughulikia suala
hilo litakalofanya wanafunzi hao kupata haki kwa kutofanya mtihani huo.
0 comments:
Post a Comment