*Atoka familia ya mama muuza mahindi ya kuchemsha
*Wakili ampatia wafadhili wa kumlipia kila kitu UDSM
Leonce Zimbandu
Edson Mwakyombe (kulia) |
MWANAFUNZI wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Edson Mwakyombe ambaye alimwaga chozi kwa kukosa mkopo kutoka
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu (HESLB), amepata ufadhili wa
kumsomesha huku akisimulia alivyojisomesha kwa kuuza mahindi.
Edson ambaye mama yake ni mjasiriamali wa kuuza mahindi
ya kuchemsha, alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano na JAMBO LEO kwenye ofisi
za gazeti hilo, Quality Center, barabara ya Nyerere, alipofika kulishukuru kwa kuchapisha
picha yake ikionesha alivyoguswa na kadhia ya kukosa mkopo, ambayo ilisambaa
kwenye mitandao ya kijamii na kuibua wasamaria wema wa kumsomesha.
Alisema haikuwa kazi rahisi kuamini kama angepata wafadhili
wa kumsaidia, kwani alichoamini ni ndoto zake kuishia ukingoni baada ya kukosa
mkopo.
“Nawashukuru wote waliojitokeza kunisaidia ili kutimiza
ndoto zangu, naishukuru JAMBO LEO imefanya kazi kuijulisha jamii shida yangu, kwani
nilijua kwamba kwa kukosa mkopo ndio ulikuwa mwisho wa ndoto yangu ya kusoma
ualimu, ili kuisaidia familia yangu,” alisema Edson.
Kilio
Akieleza sababu za kuangua kilio, Edson ambaye alisema
alifikia hatua hiyo baada ya kukumbuka maisha magumu ya familia yake, akiwamo
mama yake mzazi, Alice Mwanisongole anayeishi kata ya Mafinga, Iringa.
Akisimulia historia fupi ya maisha yake kwa mwandishi wa
gazeti hili, Edson alisoma katika mazingira magumu kutokana na kipato duni cha
wazazi wake.
“Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya baba yangu, Wisdon
Mwakyombe kufariki dunia mwaka 2012, wakati ambao nilikuwa nikifanya maandalizi
ya kurudia mitihani ya kidato cha nne, baada ya awali kupata daraja la nne,”
alisema.
Edson alisema baada ya kurudia mtihani huo alifanya
vizuri na kujiunga na kidato cha tano katika sekondari ya Jeshi ya Kawawa, JKT Mafinga.
Katika mtihani wake wa kidato cha sita shuleni hapo
alifanya vyema na kupata daraja la kwanza akiwa na alama nane, zilizomfanya atimize
ndoto yake ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).
Mkopo
Alisema baada ya majina ya waliochagualiwa kujiunga na UDSM
kutangazwa na jina lake kuwamo alifika Dar es Salaam akifikia kwa mama yake
mdogo Mbagala Kuu ili kufuatilia kama amepata mkopo wa HESLB.
Alisema licha ya alama na aina ya kozi anayotaka kusoma
kuruhusu mkopo, alishangaa jina lake kutokuwa kwenye orodha ya waliokopeshwa
hali iliyomchanganya na kumkatisha tamaa.
“Majina ya kupata mikopo yalipobandikwa kwenye ubao wa
chuo (UDSM), niliyasoma mara ya kwanza sikuona jina langu, nikarudia mara ya
pili na ya tatu, jina langu halikuwamo kwenye orodha. Sikuamini kupoteza ndoto
zangu za kusoma UDSM,” alisema.
Alisema kutokana na tukio hilo, furaha yake na ndugu zake
ilipotea ghafla, lakini aliposikia Bodi ya Mikopo inafanya mkutano Idara ya
Habari, Maelezo, kuhususuala la mikopo ya wanafunzi, aliomba msaada na kufikishwa
hapo ili kuwaona maofisa wa Bodi hiyo na kupata ufafanuzi wa suala lake.
Edson alisimulia kwamba kutokana na ugeni Dar es Salaam,
hakuwa anapajua Maelezo, hivyo alipata mtu wa kumsindikiza, lakini pia ndoto
zake kupata ufafanuzi hazikufanikiwa, ndipo alipoangua kilio na kupigwa picha
na Mpigapicha wa Gazeti hili Venance Nestory, aliyesema alimfahamu baada ya
kusoma kwenye picha aliyoipiga alivyolia.
Hata hivyo, alisema sasa matumaini yake kusomea ualimu
yamerejea baada ya kupata wafadhili huku akieleza kupata wafadhili waliojitolea
kumsomesha kwa miaka miwili.
Hata hivyo, baadaye JAMBO LEO ilizungumza na Wakili
Albert Msendo aliyeratibu utafutaji wafadhili kwa kijana huyo, ambaye alisema
tayari wafadhili watano wamejitokeza kumsomesha Edson kwa miaka yote mitatu kwa
kumlipia ada, malazi na vifaa vinavyohitajika.
0 comments:
Post a Comment