Wabunge ‘wamrarua’ Waziri wa Fedha


Sharifa Marira, Dodoma

Wakichangia mjadala kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/18 uliowasilishwa juzi, wabunge walisema, Dk Mpango anahusika na hali mbaya ya uchumi inayowakabili Watanzania kwa sasa kwa sababu hashauriki.

WABUNGE wamemtolea uvivu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakimtuhumu kujawa kiburi na kumtabiria kuwa Waziri wa pili ‘kutumbuliwa’, baada ya Charles Kitwanga aliyekuwa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Wabunge hao walikwenda mbali zaidi na kueleza kwamba wakati nchi inaelekea kukwama, adhabu anayoweza kupata Dk Mpango ni kuondolewa kwenye wadhifa wake, kwa sababu Waziri huyo hamshauri vizuri Rais.

Wabunge hao kwa nyakati tofauti walihoji sababu za Serikali kuwaletea mpango huo wa maendeleo bila kueleza utekelezaji uliopo sasa.

Michango ya wabunge

Mbunge wa Busega, Dk Raphael Chegeni (CCM), alisema ingawa Dk Mpango ni msomi, lakini ana kiburi, si msikivu na hataki kushauriwa, kwani wabunge walimshauri mambo mengi kwenye Mpango wa Mwaka 2016/17, lakini hakutaka kusikiliza na ndiyo sababu hali imekuwa ngumu kila eneo.

“Dk Mpango unapaswa kuwa msikivu na kuacha kiburi, una jeuri tunayokushauri yachukue, tunakusaidia ufanye kazi. Tulikwambia mambo mengi ukatudharau sasa yanatokea, kila kona hakuna unafuu,” alisema Chegeni.

Alisema uchumi unaozungumzwa kwenye mpango uliwasilishwa na Waziri wa Fedha hauendani na hali halisi ya maisha ya wananchi kwani halmashauri hazijapewa fedha hadi sasa.

“Wananchi hawana fedha, wabunge hawana fedha, fedha ambazo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaeleza kukusanya ziko wapi wakati madeni yameongezeka?” Alihoji na kuongeza:

‘’Waziri timiza wajibu wako, nyenyekea; umekuwa tatizo sana hata ukiitwa kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti ni ngumu kupatikana. Umeitwa hata na wafanyabiashara unakataa, dhamana uliyopewa ni kubwa usiitumie vibaya.”

Hata hivyo, Chegeni alikwenda mbali zaidi na kumgeukia Rais John Magufuli akisema licha ya ndoto yake ya kulipeleka Taifa kuwa la viwanda, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ‘ni mzee wa sound (blabla)’ na anafanya porojo .

‘’Waziri wetu Mwijage anajulikana kama Mzee wa porojo, sijui hiyo Tanzania ya viwanda tutafika lini, acheni maneno na kusigana wenyewe kwa wenyewe, mnatofautina kauli kila mmoja anaongea lake, fanyeni kazi kwa pamoja kila wizara itoe maoni yake katika huo mpango,” alisema Dk Chegeni

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) alimtabiria mabaya Dk Mpango akisema ndiye atakayefuata kwa kutumbuliwa na Rais Magufuli, kwani hali ya Taifa ni mbaya na kwamba nanga itakapokwama, Waziri huyo atatolewa ili yeye abaki salama hata kama watakuwa wamekosea wote.

‘’Mipango itakapokwama wewe ndiye utabebeshwa zigo hilo ‘utatumbuliwa’ japo mmekwamisha wote. Nakutabiria, unakaribia sana ‘kutumbuliwa’. Serikali imefilisika, haiwezi kutekeleza chochote, isaidiwe kwani kila kitu kimesimama,” alisema Heche.

Heche alisema Waziri mwingine mbabaishaji ni Mwijage kwani “ukikutana na Mwijage hapo nje ukimsalimia anakwambia kijana unataka kiwanda? Anaingiza mkono mfukoni kutoa kiwanda kwa sasa viwanda sijui vinapatikana mfukoni?”

Alisema hakuna kiwanda kilichojengwa hata kimoja na viwanda ndivyo vinaajiri kuanzia mama ntilie hadi mhandisi.

‘’Kuna taarifa mnatisha wafanyabiashara na risiti … mmeruhusu trafiki makosa ya barabarani leo hii imekuwa ni chanzo cha mapato katika Serikali ya CCM,” alisema Heche.

Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM) alisema Dk Mpango anabebesha wananchi kodi nyingi kwa kuwa hajui yanayowakuta wabunge majimboni, kutokana na ukweli kwamba Waziri huyo hajawahi kuomba kura.


“Dk Mpango wananchi wametutuma sisi CCM, sasa tunawaumiza. Au kwa sababu kaka yangu hujaenda kuomba kura? Katika mpango unaoishia, tuliwaambia msiweke kodi kwenye uhamishaji fedha, hamkutusikiliza, utalii na maeneo mengi hamkutusikiliza, matokeo yake robo iliyopita benki zimezalisha hasara, kila kona hakuna fedha, kodi isiwe lengo lako kwenye kila jambo, tunaua biashara,” alisema.

Bashe aliwataka wabunge wasiwatoe roho mawaziri wa Elimu, Afya kutokana na ukosefu wa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na ukosefu wa dawa, bali wanapaswa kulia na kumshikilia Dk Mpango kwa kuwa ndiye anayeshikilia fedha zote.

‘’Wabunge wanalalamika dawa hakuna, mikopo hakuna, mimi natoka Kamati ya Huduma za Jamii ambayo tunasimamia wizara hizo, hakuna fedha mtawatoa roho, Ummy (Mwalimu), Kigwangallah (Dk Hamisi) na Ndalichako (Joyce), kama tunataka kusaidia Serikali tushughulike na Wizara ya Fedha, kuna matatizo,’’ alisema Bashe.

Naye Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum (CCM) alisema Dk Mpango hajaonja ‘joto ya jiwe’ ambayo wabunge wanapewa na wapiga kura wao kutokana na hali mbaya ya uchumi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo