Celina Mathew
Luteni Kanali mstaafu Dk Haruni Kondo |
MWENYEKITI wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania (TPC),
Luteni Kanali mstaafu Dk Haruni Kondo ameagiza kuundwa tume ya kuchunguza
ubadhirifu kwenye shirika hilo likiwamo suala la watumishi hewa.
Aidha, ameagiza wahusika watakaobainika wachukuliwe hatua
na kwamba shirika halitamfumbia macho mwizi, mla na mtoaji rushwa maana kwa
kiasi kikubwa changamoto hizo zimekuwa zikisababisha shirika kudorora.
Dk Kondo alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa kwenye shirika hilo kuna
watu wanaotumia nafasi zao kujinufaisha na kuacha shirika linateketea.
Alisema kwa sasa umefika wakati mtu anaacha kazi na
kujadili mpira bila hatua kuchukuliwa maana eneo hilo ni la kazi na si kijiwe.
“Kwa kiasi kikubwa mashirika yanaathirika sana na
watendaji maana wanajisahau na kutumia madaraka yao vibaya, hivyo ni vema
wakaachana na makandokando waliyonayo maana hatutamvumilia atakayeendeleza
michezo kama hiyo,” alisema.
Aliongeza kuwa ana taarifa kuwa watu kama hao bado wapo
kwenye shirika hilo na endapo ataruhusu hali hiyo kuendelea shirika litapoteza
sifa hivyo atahakikisha anakabiliana nayo.
“Mtanzania hana uoga anafanya vitu anavyotaka, haogopi
kuua shirika mfano unakuta mtu anafanya ubadhirifu wa kubadili Sh milioni 500
na kuifanya Sh bilioni moja hali ambayo inasababisha wachache kujinufaisha na
fedha nyingi ambazo hawajazitolea jasho,” alisema.
Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi kuliko nchi nyingi
lakini cha kushangaza zinatumika vibaya, hivyo alilitaka shirika hilo kuendana
na kaulimbiu ya Rais ya kuwa na nchi ya viwanda na kufikia uchumi wa kati.
Aliomba ufafanuzi wa ubadhirifu kwenye nyumba ya shirika
yenye vyumba sita Ubungo ambayo ilikuwa inamilikiwa na Posta kwa ajili ya
kutunza kumbukumbu na baadaye kuuzwa kwa mbia mwaka 2013.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Kaimu Postamasta Mkuu wa
TPC, Fortunatus Kapinga alisema jengo hilo lenye ghorofa tatu na vyumba sita,
halikukamilika ujenzi wake hivyo likawa limefanywa eneo la kutunza kumbukumbu.
Alisema mpangaji alipatikana kupitia zabuni lakini
kiwango ambacho kilipatikana ni cha zamani cha Sh 600,000 lakini baadaye
aliomba afanye marekebisho.
Aliahidi mbele ya Mwenyekiti huyo kuwa marekebisho ya
mikabata na mchakato huo utakamilika mwishoni mwa mwaka huu ili aweze kuhamia.
Hata hivyo alisema kwa upande wa manunuzi mbia huyo
alitaka kuwapeleka mahakamani kutokana na kiasi anacholipa ambapo walimuahidi
kuwa fedha zitazokuwa zinapatikana watamlipa taratibu ili kuweza kulimiliki
wenyewe.
Baada ya ufafanuzi huo, Mwenyekiti huyo aliwataka
waliohusika kusainisha mkataba huo kuhakikisha wanawajibika maana unaonesha
kuwa kwenye nyumba hizo tatu shirika linapata Sh milioni 1.8 kwa mwezi ambapo
kwa miaka mitatu ni Sh milioni 64.8 hivyo mbia anadai kuwa ametumia Sh milioni
398,741.
“Watu wenye madoadoa waliopo kwenya shirika hili ambao
wanajijua wameshiriki kwenye hilo ni vyema wakaondoka wasisubiri kuondolewa
maana samaki mmoja akioza ni wote,” alisema.
Akizungumzia watumishi hewa ndani ya shirika, aliitaka
tume itakayoundwa kuhakiki upya vyeti vya watumishi hao ili kuhakikisha kuwa walioghushi
vyeti wanawajibishwa.
0 comments:
Post a Comment