Edith Msuya
Salim Bimani |
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeitaka Serikali kuhakikisha Muswada
wa Sheria ya Habari kandamizi uliowasilishwa bungeni unaondolewa na kutoa fursa
zaidi kwa wadau kushiriki kutoa mapendekezo yao kwa maslahi mapana ya Taifa.
Akizungumza jana Dar es Salaam katika maadhimisho ya
kimataifa ya kukomesha vitendo vya ukatili na uhalifu dhidi ya wandishi wa
habari duniani, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma, Salim Bimani,
alisema Muswada huo unamnyima mwandishi uhuru wa kufanya kazi yake.
Alisema katika kuadhimisha siku hiyo, chama hicho
kinapinga vitendo vyote wanavyofanyiwa wandishi wa habari na kufungwa kwa
vyombo vya haabari.
“Kumekuwa na vitendo vya kutisha wandishi na vyombo vya
habari, kuingilia uhuru wa vyombo vya habari na kupokonywa vitambulisho, kutekwa,
kushambuliwa na mbwa wa Polisi na kujeruhiwa, vitendo ambavyo si vizuri,” alisema.
Alisema Umoja wa Mataifa ulipitisha Azimio namba A/RES/68/163
kwenye mkutano wake wa 68 uliofanyika mwaka 2013 na kuazimia kuwa ifikapo
Novemba 20 kila mwaka iwe siku ya kimataifa ya kukomesha ukatili na uhalifu
dhidi ya wandishi wa habari.
“Azimio hilo linazitaka nchi wanachama kulitekeleza na
kuondoa utamaduni wa kuwatendea ukatili wandishi wa habari, ikikumbukwa mauaji
ya waandishi wawili wa Ufaransa waliouawa Mali Novemba 2, 2013,” alisema.
Aidha, alisema chama hicho kinaungana na Watanzania wote
na wadau wengine duniani kupinga ukatili na uhalifu dhidi ya wandishi na
watendaji wote katika tasnia ya habari duniani.
Alisema ni vema Serikali ikaheshimu Azimio hilo na kujenga
mazingira rafiki ya uwajibikaji huku wahalifu wakichukuliwa hatua stahiki haraka
na waathirika wote wa kadhia hizo wapate huduma stahiki na kwa wakati.
0 comments:
Post a Comment