Vyuo 26 vya Ufundi, Habari vyafungwa


Fidelis Butahe
            
Dk. Adolf Rutayuga
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) limefunga vyuo vya ufundi 26 na kusimamisha vingine 22 kutokana na makosa mbalimbali, ikiwamo kushindwa kuzingatia masharti na kutoa mafunzo yasiyothibitishwa.

Kati ya vyuo vilivyofungiwa, vinane viko Mbeya huku zaidi ya vitatu vikitajwa kuwa Dar es Salaam na Geita.

Miongoni mwa vilivyosimamishwa kwa kutoa mafunzo bila uthibitisho vimo vya Ualimu vya Miso na Tusaale vilivyoko Mafinga na cha Uandishi wa Habari cha Dar es Salaam Institute of Journalism and Mass Communication, chenye matawi mikoa mbalimbali nchini.

Akitangaza hatua hiyo jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Adolf Rutayuga alisema Necta imekuwa ikifuatilia vyuo vya ufundi ili kutathmini kama vinafuata viwango vya ubora wa kitaaluma vilivyowekwa katika kutoa mafunzo.

Alisema baada ya utafiti walibaini vyuo 26 kushindwa kuzingatia masharti ya Baraza katika cheti cha usajili, huku vyuo 20 vikitoa mafunzo yasiyothibitishwa chini ya idara isiyotambulika.

“Pia tulibaini vyuo viwili kuwa na vituo vya satelaiti au kampasi, ambavyo navyo havijathibitishwa na chombo husika,” alisema.

Alibainisha kuwa kuendesha chuo bila kuzingatia matakwa ya Baraza hilo ni kosa kisheria.

Alisema kanuni zinasema hatua kali zinaweza kuchukuliwa kwa kila kosa kulingana na matokeo ya ufuatiliaji uliofanywa na timu maalumu.

Aliongeza kuwa Baraza hilo limechukua hatua kwa vyuo vya ufundi 48 kutokana na makosa yaliyofanywa na limesitisha vyeti vilivyotolewa kwa vyuo 20 kutokana na kushindwa kuzingatia masharti kwenye cheti cha usajili.

Alisema uamuzi huo ulifanywa kwa mujibu wa Kanuni ya 20 ya Usajili wa Vyuo vya Ufundi ya mwaka 2001.

“Vyuo vya ufundi vinatakiwa kupata idhini ya Baraza kabla ya kuanza kutoa mafunzo yoyote. Idhini hiyo inahusu uthibitisho wa mtaala kwa ajili mafunzo yaliyokusudiwa na utambuzi wa idara iliyopangwa kutoa mafunzo hayo,” alisema.

Kuhusu vyuo vyenye vituo vya setelaiti na kampasi, Dk Rutayuga alisema Baraza linahitaji mafunzo kutolewa katika vituo vilivyosajiliwa na kampasi za vyuo vikuu baada ya kuthibitishwa kwamba vinastahili kutoa mafunzo.

“Taasisi mbili zimebainika kutoa mafunzo katika vituo vya satelaiti, vyuo vikuu ambavyo havijasajiliwa na Baraza na hivyo kuadhibiwa. Vyuo hivyo navyo vimefutiwa leseni,” alisema Rutayuga.

Vyuo vilivyofungwa

Green Hill Institute, Institute of Business and Social Studies, Loyal College of Africa, Mbeya Training College, New Focus College, Shukrani International College of Business and Administration, Majority Teachers College, MAM Institute of Education (vya Mbeya).

Vingine ni Belvedere Business and Technology College na Gisan Institute of Health Sciences (vya Mwanza), Marian College of Law, Modern Commercial Institute, Dar es Salaam Institute of Business Management na Samfelis College of Business Studies (vya Dar es Salaam).

Katika orodha hiyo vyuo vya Geita vilivyofungwa ni Geita Medical Laboratory Sciences and Nursing Training College, St. Bernard Health Training Institute na Global Community College.

Pia kipo cha Rukwa College of Health Sciences, Institute of Management and Development Studies cha Iringa na Mbengwenya College of Business and Information Technology cha Mbinga.

Vingine ni Muleba Academy Institute, Tanzania Institute of Chartered Secretaries and Administrators cha Arusha na Victoria Institute of Tourism and Hotel Management cha Mwanza, Ellys Institute of Technology cha Mara na Emmanuel Community College (Kibaha).
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo