WAKAZI wa Dar es Salaam wameitaka
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kutupilia mbali ombi la Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco) la kupandisha bei ya umeme.
Hatua ya Tanesco imefika ikiwa imepita
miezi saba tangu kutangazwa kwa bei mpya ya umeme iliyokuwa na punguzo la
asilimia 1.5 hadi 2.4.
Wakizungumza jana na JAMBO LEO, wananchi
hao walisema kupandishwa bei ya umeme kutazidisha ugumu wa maisha.
Mkazi wa Mikocheni, Rashid Said alisema kinachotaka
kufanywa na shirika hilo si sawa, kwani hali ya kifedha kwa wananchi ni ngumu hivyo
maisha yatazidi kuwa magumu.
“Wananchi wasikubali kupandishwa bei
hiyo, hata wakishirikishwa kutoa maoni, tutazidi kuumia hasa wananchi wa hali
ya chini,” alisema.
Alisema Serikali ilisema gharama za
umeme zitapungua huku wakishangaa kupandishwa kwa gharama hizo siku chache baada
ya kushushwa.
Mkazi wa Manzese, Hussein Suleiman
alisema kupandishwa kwa gharama hizo kutaathiri wananchi na kuwa na maisha
magumu huku wakishindwa kutumia huduma hiyo.
“Wananchi wengi watashindwa kutumia
huduma hiyo kwa sababu ya gharama kuwa kubwa na kushindwa kuzimudu,” alisema.
Frida Gervas wa Mikocheni alisema
kupandishwa kwa bei ya umeme si sawa. “Wanavyotaka kupandisha bei hiyo si sawa
kabisa kwa sababu sasa hivi fedha haipatikani kirahisi wakipandisha hali
itazidi kuwa ngumu,” alisema.
Mkazi wa Tegeta, Enock Edward alisema endapo
Shirika hilo litapandisha gharama za umeme wananchi wa maisha ya chini wataumia.
Alisema hali hiyo itasababisha kupata kizio
kidogo cha umeme kwa kiwango cha fedha walichozoea kununua kila siku na kutumia
gharama kubwa kupata kiwango kitakachotosheleza.
“Mimi nashangaa tangu tuambiwe kuna gesi
hatuoni faida yoyote wananchi hadi sasa hakuna unafuu wowote, na sasa wanataka
kupandisha gharama za umeme,” alisema.
Alisema wananchi wengi walitarajia kuona
gharama za umeme zikipungua kutokana na upatikanaji wa gesi lakini hali imekuwa
tofauti na inavyokwenda.
Ewura inajiandaa kukusanya maoni ya
wadau kutokana na maombi ya Tanesco kuongeza bei ya nishati kwa wastani wa
asilimia 18.9 mwakani.
0 comments:
Post a Comment