Suleiman Msuya
UBALOZI wa Ujerumani nchini, umetoa Sh
bilioni 26.4 kwa ajili ya chakula cha wakimbizi kutoka Burundi na DRC Congo
walioko kambini Kigoma.
Fedha hizo pia zinatarajiwa kusaidia
taasisi mbalimbali ambazo zinahudumia wakimbizi mkoani humo.
Hayo yalisemwa jana na Balozi wa
Ujerumani nchini, Egon Kochanke wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam.
Kochenke alisema Ujerumani imetoa fedha
hizo ikiwa ni mwendelezo wa kusaidia Serikali ya Tanzania kukabiliana na
ongezeko la wakimbizi.
Alisema fedha hizo zinaelekezwa kwa
Shirika la Chakula Duniani (WFP), Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa (UNHCR), Tanzania na asasi mbalimbali ambazo zinajihusisha na utoaji
huduma.
“Tumeamua kutoa fedha hizi ili kusaidia
kundi kubwa la wakimbizi ambalo linaingia Tanzania, naamini msaada huu utasaidia
kwa kiasi fulani,” alisema.
Balozi alisema pamoja na kutoa msaada
huo wanazitaka nchi zenye migogoro zirejeshe amani ili wananchi waliokimbia warejee.
Mwakilishi Mkazi wa UNHCR, Chansa Kipaya
alisema idadi ya wakimbizi imekuwa ikiongezeka na kwa siku zaidi ya watu 3,000
huingia Kigoma.
Alisema hivi sasa kuna wakimbizi 245,083
wa Burundi na DRC Congo ambapo katika kambi za Nyarugusu wako 128,888, Ndutu
65,178, Mtendeli 50,732 na Lumasi 285.
Kipaya alisema UNHCR inahitaji zaidi ya
dola milioni 47 za Marekani kukidhi mahitaji ya wakimbizi wote kambini humo.
Mwakilishi Mkazi huyo alitoa mwito kwa
wadau kuendelea kuchangia UNHCR ili iweze kutoa huduma za msingi kwa wakimbizi.
Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Michael Danford
alisema kwa sasa hifadhi ya chakula ni tani 80,000 huku mahitaji yakiwa tani
254,000 ili kukidhi wakimbizi waliopo.
Alisema WFP inahitaji dola milioni 6.5
kuziba pengo la chakula kwa wakimbizi hadi mwakani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya
Ndani, Balozi Hassan Simba Yahya aliishukuru Ujerumani kwa msaada huo huku
akibainisha kuwa jitihada zinaendelea kuhakikisha migogoro inayoendelea nchi
jirani inatatuliwa.
Balozi Simba alisema Tanzania
itajitahidi kila njia kuhakikisha migogoro hiyo inamalizika na kuasa wakimbizi
kuepuka kuharibu mazingira ya maeneo wanamoishi.
0 comments:
Post a Comment