Sharifa Marira
Mwigulu Nchemba |
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mwigulu Nchemba amesema Polisi haikuruhusu
mkutano wa hadhara wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, bali ilitumia
busara kutotawanya wananchi kwani walishajikusanya.
Alisema baada ya mkutano huo, Jeshi hilo
lina uwezo wa kumhoji Lipumba ni wapi alikosea katika kufanya mkutano huo
kuliko kutawanya wananchi ambao wangeweza kuumia.
Mwigulu alitoa majibu hayo juzi baada ya
kuibuka kwa hoja kwenye kundi la WhatsApp linalojulikana kama Tanzania Yetu
2016 ambalo lina wajumbe kutoka maeneo mbalimbali wakihoji sababu za Jeshi hilo
kuruhusu mkutano wa Lipumba wakati imepigwa marufuku nchi nzima.
“Si kwamba tunaruhusu, ila njia nzuri ya
kudhibiti tukio ambalo limeshatokea
yaani watu walishakusanywa, kuwatawanya tungeweza kuumiza au kuua watu,
tulichofanya ni kuruhusu amalize halafu tumwambie makosa yake,’’ alisema
Mwigulu.
Baadhi ya wajumbe walihoji kuwa ikiwa
Polisi imetumia busara katika mkutano wa Lipumba kutotimua watu kwa nini
ilitimua wananchi kwenye mkutano wa Chadema wa Kahama?
Akijibu swali hilo, Mwigulu alisema:
“Nilikuwa bado Kilimo lakini nakumbuka nikiwa wizara hii, Mbunge wa Buyungu, Kasuku
Bilago (Chadema) watu walikusanyika bila kibali nikawaambia mwacheni aongee na
wananchi waondoke.’’
Aluiongeza: “Mbunge wa Viti Maalumu
Chadema, Cecilia Paresso, pia vivyo hivyo kipindi mikutano hata ya wabunge
ilipozuiwa, niliwaambia askari walindeni wafanye mikutano na wananchi
wakishaondoka waulizeni walipokosea kama ilivyotokea kwa Lipumba’’.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe walitaka
kujua sababu za mikutano ya hadhara kuzuiwa huku wengine wakieleza kwamba Serikali
inahofia matusi alisema mikutano haijazuiwa kwa sababu ya matusi ila ni
utaratibu wa siasa.
“Kuna miaka miwili ya uchaguzi
yaani wa serikali za mitaa na uchaguzi
mkuu, kuna hamasa ya daftari, basi
tufanye kazi hata miaka miwili kati ya
mitano,’’ alisema na kuongeza:
“Ni vema kwa sasa tuongelee fursa na
tukosoane kwenye kazi ili wananchi wapate manufaa, halafu uchaguzi ukifika
tuongee uchaguzi, haya mambo ya kuwaza uchaguzi kwa miaka minne ijayo, si uzalendo tufanye kazi
Serikali imeshaundwa.’’
Katika kundi hilo pia iliibuka hoja ya
Serikali kutaka kuua vyama visivyo na wabunge kwa kuruhusu mikutano kwa wabunge
pekee ambapo Mwigulu alisema: ”Hili la vyama kwa kweli mtazamo wake ni tofauti
maana wanatakiwa watengeneze miundo ya vyama kabla ya mikutano wanaweza kufanya
hivyo kwa mikutano ya ndani si lazima ya hadhara.”
0 comments:
Post a Comment