Mariam Cyprian, Tanga
Dk. John Magufuli |
SERIKALI ya Kuwait iko tayari kuendelea kuisadia Tanzania
katika sekta za elimu, afya na maji ikiwa ni njia ya kuunga mkono na kuukubali
uongozi wa Rais John Magufuli.
Ahadi hiyo ilitolewa juzi na Balozi wa Kuwait nchini,
Jasema Al Najem katika mahafali ya 15 ya kidato cha nne ya sekondari ya wasichana
ya Al Kheir jijini hapa.
Al Najem aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo,
alisema Kuwait ina imani kubwa na uongozi wa Rais Magufuli na kutokana na hilo,
itaendeleza uhusiano wake wa kusaidia sekta hizo muhimu.
Alisema kuna umuhimu wa jamii ya kitanzania kutilia mkazo
suala la elimu kwa watoto wa kike,
kwa sababu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi zinazochangia kusitisha masomo yao.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Africa Muslims Agency
tawi la Tanga ambayo ndiyo
inayoendesha shule hiyo, Ahmed Shehata alisema kutokana na namna walivyoandaa mwanafunzi wao wana imani,
kwamba wahitimu wote 34 wa kidato cha nne shuleni
hapo watafaulu na kwenda kidato cha tano.
“Watoto wa kike wamekuwa wakipata changamoto katika
upataji wao elimu hivyo kutokana na
changamoto hizo, tumehakikisha Al Kheir ina maabara ya masomo ya Sayansi, maktaba
yenye vitabu vyote pamoja na kompyuta zilizo na mtandao wa intaneti pamoja na walimu wenye
uhodari ili kuhakikisha tunakuwa na ufaulu mzuri shuleni kwetu,” alisema.
Mkuu wa Shule hiyo, Zubeda Kimolo alisema kutokana na
malezi yanayotolewa shuleni hapo,
wanafunzi waliofaulu kwenda vyuo vikuu na
vituo vya kazi za sheria, ualimu, ufamasia, udaktari, ukandarasi na uhasibu wamekuwa mfano wa kuigwa na
hivyo kuipa sifa shule hiyo.
0 comments:
Post a Comment