Abraham Ntambara
Jaji Francis Mutungi |
MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi
amefuta usajili wa vyama vitatu kutokana na alichoeleza kuwa ni kupoteza sifa
za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa Jaji Mutungi, vyama vilivyofutiwa usajili ni
Jahazi Asilia, Chama cha Haki na Ustawi (Chausta) na APPT- Maendeleo.
APPT- Maendeleo inaongozwa na Peter Mziray ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini.
Akizungumza na JAMBO LEO jana Dar es Salaam, Mziray alisema
chuki binafsi za Msajili ndizo zilizomsukuma kufuta vyama hivyo, lakini akasema
anamwombea Jaji Mutungi Mwenyezi Mungu aendelee kumwongeza vyeo.
“Ni chuki binafsi hakuna la zaida, kwa sababu hapa kuna
vyama vingine havina hata mwenyekiti wa kitongoji, kuna vyama vina migogoro na
kuna vyama polisi wanadai vinavunja amani ya nchi. Sasa mimi APPT-Maendeleo
nimemkosea nini?” Alihoji Mziray.
Mziray aliongeza kuwa sababu nyingine ni suala la
Zanzibar, kwa kuwa yeye ni miongoni mwa viongozi waliokosoa na kubainisha kwamba
hatua ya kufutiwa chama haimpi presha yoyote na kusema: “Wacha mapenzi ya Mungu
yatimie.”
Alisema kwa kuwa Jaji Mutungi ni Mkristo kama yeye na kwa
kuwa amemfutia chama, Mungu atamwadhibu hapa hapa duniani.
Alisema kwa hali ilivyo sasa siasa inaelekea kubaya
nchini kwa sababu ingawa yeye ni kiongozi, hakuna hata siku moja waliyokaa na
Jaji Mutungi kuzungumza juu ya chama chake na wala hakuwahi kuitwa.
Alisema huenda ni kwa sababu Msajili huyo amechongewa kwa
Rais John Mgufuli, kwamba alikuwa akituhumiwa kuwa ni mwana Ukawa hivyo
kuchangia kufutwa kwa APPT- Maendeleo.
Awali, Jaji Mutungi akizungumza na waandishi wa habari alisema:
“Nachukua nafasi hii kuutaarifu umma wa Watanzania kuwa, kwa mamlaka niliyopewa
chini ya kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992,
nimefuta usajili wa vyama vya siasa vitatu kuanzia leo Novemba 9.”
Jaji Mutungi alifafanua kuwa vyama hivyo vilipoteza sifa
na kufikia hatua hiyo kutokana na kwenda kinyume na matakwa ya sheria ya
usajili ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwasilisha hesabu za mapato na matumizi
ya mwaka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukaguliwa kwa
mujibu wa kifungu cha 14(1)a.
Mengine ni kushindwa kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya
Siasa tamko la orodha ya mali za chama kwa mujibu wa kifungu cha 14(1)(b)(ii),
kushindwa kutekeleza matakwa ya kifungu cha 15(1) kwamba mapato yote ya fedha
ya chama yawekwe katika akaunti ya chama.
Aidha, alisema mashariti mengine yaliyokiukwa na vyama
hivyo ni kutokuwa na ofisi ya chama Tanzania Bara na Zanzibar kwa mujibu wa
kifungu cha 10(d), kutokuwa na wanachama Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha
10(b) na kushindwa kuweka kumbukumbu za mapato na matumizi ya chama kwa mujibu
wa kifungu cha 14(1)a.
Mutungi alifafanua, kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 7(3)
Sheria ya Vyama vya Siasa, taasisi yoyote hairuhusiwi kufanya kazi kama chama
cha siasa ikiwa haijasajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Aliwakumbusha waliokuwa wanachama na viongozi wa vyama
hivyo, kwamba hawapaswi kufanya shughuli yoyote ya kisiasa kwa kutumia jina la
chama kilichofutwa kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi ikiwamo ya
vyama vya siasa.
Aliviasa vyama vya siasa kuheshimu Katiba na kanuni za
vyama vyao ili kuepusha migongano ndani ya vyama ambayo inafanya vyama kuwa
dhaifu na kushindwa kutekeleza sheria na majukumu yake kisiasa.
0 comments:
Post a Comment