Salha Mohamed
Paul Makonda |
SERIKALI inatarajia kujenga vituo 20 vikubwa vya polisi
vyenye thamani ya Sh. bilioni 10 ili
kusogeza huduma ya usalama kwa raia.
Vituo hivyo vitajengwa jijini Dar es Salaam kwa uwiano wa
vituo vinne katika kila wilaya. Kila kituo kimoja kikikisiwa kugharimu Sh
milioni 500.
Mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda, alibainisha hayo wakati
akitembelea vituo vidogo vya polisi jijini humo jana.
Alisema ujenzi wa vituo hivyo utaenda sambamba na idadi
ya askari wa kutoa huduma bora kwa wananchi. Makonda alieleza kuwa vituo hivyo
vitakuwa na mfumo wa mawasiliano baina ya kituo kimoja na kingine ili mtuhumiwa
akikamatwa wote wajue yuko katika kituo gani cha polisi.
“Tunataka kujenga kituo cha polisi katika kila wilaya
ambacho kitakuwa na uwezo wa kuwa na askari wasiopungua 100 na sehemu za kuweka
silaha zao,”alisema.
Alisema vituo vingi vya polisi jijini Dar es Salaam hufungwa
mapema na kusababisha wananchi kukosa huduma nyakati za usiku, huku vingine
vikishindwa kutenganisha mahabusu hasa kwa wale wenye mahitaji maalumu.
Alisema wataangalia sehemu zenye uhitaji na watu wengi
ili watu wapate huduma na kuimarisha usalama wa wananchi wa maeneo yao.
Makonda alisema ana shauku ya kuona kila Mtanzania
anakuwa na uwezo wa kutembea usiku na mchana bila kuhofu kuibiwa mali zake.
“Tunataka wafanyabiashara wawe wanafunga maduka yao saa
nne usiku kama wanavyofanya nchi za wenzetu kama Dubai na wananchi wanakuwa na
uhakika na usalama wao,”alisema.
Alisema zipo nchi ambazo hazina uhalifu ambapo mtu
akiacha kitu chake anakikuta alipokiacha huku akiwaasa wananchi kushirikiana na
jeshi hilo.
“Kumekuwa na matukio ya ujambazi, uporaji kwa kutumia pikipiki unaongezeka, hivyo ni wajibu
wetu kuhakikisha kuna utulivu na usalama katika mkoa wetu,” alisema.
Alisema wananchi wanalalamika kutopata huduma kutoka Jeshi
la Polisi, lakini hali hii inatokana na askari kuwa wachache katika vituo hivyo,
huku wakifanya kazi katika mazingira magumu na kushindwa kuacha vituo hivyo
bila askari.
“Kituo kikubwa kitahudumia wananchi wengi na ndoto yangu
kuwe na askari wengi mtaani na wengine kubaki mitaani,”alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Kanda maalumu
ya Dar es Salaam Simon Sirro, Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Kamanda Hezron
Gimbi alisema mradi huo wa vituo vya polisi utasaidia jeshi hilo kufanya kazi
yao kiufanisi zaidi.
“Mradi huu utaongeza ufanisi na kupunguza msongamano wa
kutoa huduma kwa wananchi hasa katika upelelezi na hata mahojiano,”alisema.
0 comments:
Post a Comment