* Asema suala la Katiba mpya litakuja baadaye
* Asisitiza hakuingia Ikulu kufukua makaburi
Celina Mathew
Rais John Magufuli |
RAIS John Magufuli amewataka Watanzania wamwache
anyooshe nchi kwanza ndio mengine yafuate, kutokana na kukutana na ‘madudu’
ambayo mengine hakuyatarajia, huku akitaja mfano wa mapya matatu aliyokutana
nayo.
Magufuli aliyezungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini
Ikulu, Dar es Salaam jana, siku moja kabla ya kutimiza mwaka mmoja tangu aingie
madarakani, alitaja ‘madudu’ hayo kuwa ni pamoja na kupotea kwa meli 60
bandarini.
Mbali na meli hizo, Rais Magufuli alisema alishangazwa kukuta
orodha ya wanasiasa, wakiwamo wanaozungumza sana ndani ya CCM anayoiongoza na
katika vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD,
waliokopa mabilioni ya fedha kwenye benki na kutishia kufilisika kwa taasisi
hizo za fedha.
Rais Magufuli ambaye ameendelea kuwa mashuhuri kwa
Watanzania, pia alielezea kushangazwa kukutana na kashfa ya kuwepo mkopo wa dola
za Marekani milioni 20, sawa na zaidi ya Sh bilioni 40, kwa ajili ya ujenzi wa
kiwanda mkoani Lindi, ambazo zimeyeyuka na kiwanda husika hakipo.
Meli
Katika kufafanua ‘madudu’ hayo, alitolea mfano namna nchi
ilivyokuwa ikipoteza fedha nyingi na kusema hakutarajia katika nchi hii, meli
zije zifike 60 na zisiorodheshwe kokote.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, meli hizo ambazo zilitia
nanga katika bandari ya Dar es Salaam; moja ya chanzo kikubwa cha mapato ya
Serikali, kila moja ilikuwa na uwezo wa kubeba kontena 3,000.
Ingawa hakufafanua zaidi, lakini kwa taarifa hiyo
kutosajiliwa kwa meli hizo, kuna uwezekano wa kuwepo kwa kontena 180,000
zilizoingia nchini bila kulipa kodi, hatua iliyosababisha aseme “tulifikia
pabaya”.
Mikopo
Akizungumzia wanasiasa kufilisi benki, Rais Magufuli
alisema viongozi hao wanaoheshimika na wananchi, wengine wakionekana kuwatetea,
wamekuwa wakichangia kufa kwa benki, kutokana na kukopa fedha nyingi na
kusababisha madeni makubwa.
“Benki zilikuwa zinakopesha wanasiasa wa Ukawa na CCM,
lakini cha kushangaza hawarudishi fedha hizo na kuna benki zimefilisika, hivyo
inabidi waanikwe bila kujali itikadi zao, ili kurejesha nidhamu katika
ukopaji,” alisema Magufuli bila kutaja benki hizo.
Pamoja na kutotaja benki hizo, lakini kauli hiyo imekuja
siku chache baada ya kufungwa kwa wiki moja kwa Benki ya Twiga Bancorp, baada
ya kuishiwa mtaji.
Magufuli pia aligusia uwepo wa wanasiasa waliokuwa
wakitumia nyumba za umma bila kulipa kodi ya pango lakini bila kuwataja majina,
ingawa hivi karibuni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), lilitupa nje vyombo vya
kampuni ya Mbowe Hotels na Kampuni ya Free Media inayomiliki Gazeti la Tanzania
Daima, chini ya familia ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kutokana na
malimbikizo ya deni la Sh bilioni 1.2 ya pango.
Kiwanda
Mbali na mikopo hiyo ya wanasiasa, wakiwamo wanaodaiwa
pango, Rais Magufuli pia alizungumzia uwepo wa mkopo wa dola milioni 20,
zilizodaiwa kuwa za kujenga kiwanda Lindi.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, hakukuta fedha hizo ambazo
ni sawa na zaidi ya Sh bilioni 40, lakini hata kiwanda chenyewe hakikuwapo.
Kutokana na hali hiyo, alisema alilazimika kuchukua baadhi
ya hatua, lakini akafafanua hazijalenga kufukua makaburi; “Sikuja hapa
kuchimbua makaburi maana nikiyachimbua mengine nitashindwa kuyafukia, ninachofanya
ni kuendeleza wengine walikoishia na kuhakikisha nchi inasonga mbele.
Ajira
Akizungumzia shutuma zinazoelekezwa kwake kuwa Serikali
inatumia gharama zile zile za kulipa mshahara, wakati imeondoa watumishi hewa,
alifafanua kuwa fedha zilizokuwa zikipelekwa kwa watumishi hewa, sasa
zinatumika kuongeza mshahara kwa waliopandishwa vyeo.
Rais Magufuli alifafanua kuwa watumishi hewa
wasingepunguzwa, hata malipo ya mshahara kwa mwezi yangefikia Sh trilioni moja,
tofauti na ilivyo sasa ambapo wafanyakazi wanalipwa zaidi ya Sh bilioni 500
kila mwezi.
Kuhusu kusimamishwa ajira, alifafanua kuwa uamuzi huo
ulikuwa wa miezi miwili ili kushughulikia watumishi hewa, lakini tayari
Serikali imeanza kuajiri.
"Ndio maana hata juzi nilitoa ajira za madaktari wa
hospitali ya Mloganzila karibu 100 na tunatarajia kuongeza zaidi ya 200, ili
ifunguliwe mwezi ujao, hivyo (kusitishwa kwa ajira) ilikuwa kwa wakati ule wa
miezi miwili tu na tulifanya hivyo kubana matumizi.
“Hebu jiulize, unakuwa na watumishi hewa 17,000 ambao
wanalipwa mishahara, posho, wanachangiwa fedha mifuko ya pensheni,"
alisema.
Alisema watumishi hao hewa kuna fedha walichangiwa kwenye
mifuko hiyo ambapo kuna Sh bilioni 6.7 zilirudishwa jambo lililosababisha
asitishe kuajiri watu wakati kuna watumishi hewa.
Alifafanua kuwa ilibidi lifanyike suala moja la kuondoa
wafanyakazi hewa, halafu baada ya hapo ndipo lifanyike lingine la kuajiri na
kwamba suala la watumshi hewa linaendelea kuchambuliwa hivyo wanaweza kufikia
hata zaidi 20,000.
Rais Magufuli aliongeza kuwa hata ajira zinazotolewa sasa
ni kwa uangalifu wa hali ya juu, ili Serikali isiingie kwenye mchezo ambao ulijitokeza
na kujikuta watumishi hewa wanarudishwa kazini kwa kubadilisha majina yao na
kuweka mengine.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, uwepo wa watumishi hewa zaidi
ya 17,000, maana yake ni Watanzania zaidi ya 17,000 ambao si hewa walionyimwa.
0 comments:
Post a Comment