Mwandishi Wetu
WAKATI wadau wa habari wakipendekeza
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari usijadiliwe bungeni, ili kutoa nafasi
kwao kuujadili kwa kina, Rais John Magufuli amepigilia msumari wa mwisho katika
maombi hayo, baada ya kuahidi kusaini sheria hiyo mara itakapofikishwa mbele
yake.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari
Ikulu Dar es Salaam jana katika mahojiano yaliyorushwa moja kwa moja na
televisheni na redio mbalimbali nchini, Rais Magufuli alisema hawezi kuingilia
Bunge maana nchi ina mihimili mitatu.
Akifafanua jibu baada ya kuombwa
kusitisha kujadiliwa kwa Muswada huo, Rais Magufuli alisema nchi ina mihimili
mitatu ya Bunge, Serikali na Mahakama, hivyo akichukua uamuzi kwenye suala
hilo, kwa kiasi kikubwa atakuwa amekiuka sheria na kanuni za Bunge.
Alisema sheria yoyote inapopelekwa
bungeni ina misingi na mahitaji yake kwa wakati huo na kwamba bahati nzuri
alikuwa mbunge na anajua Muswada huo ni wa siku nyingi na mpaka sasa
haujakamilika.
“Nimekuwa mbunge kwa miaka 20,
Muswada wa Sheria ya Habari ulianza mwaka
2011, baadaye kukatolewa muda wa kujadiliana zaidi, lakini kuanzia muda huo watu hawakujiandaa hadi sasa,
hivyo hata wangepewa hata miezi mitatu, wasingeweza kujiandaa,” alisema.
Alisema ukweli ni kuwa sheria yoyote
baada ya kutungwa, inaweza kurekebishwa ili kwenda na mabadiliko na kwa kuwa
kwa sasa Muswada huo uko bungeni wakati kuna mihimili mitatu, kumwuliza mambo
ya Bunge ambayo hayajaletwa kwake kwa sasa ni sawa na kumwonea.
“Katika nchi ya utawala wa sheria
tuwaache wabunge watimize wajibu wao sasa kuniambia kwamba utakapoletwa
niukatae, nataka niwaeleze bila unafiki, kuwa siku utakapokuja mimi nitausaini
hapo hapo, ili kusudi msubiri wakati mwingine kuibadilisha mfanye hivyo, maana
sitaki kuingilia uamuzi wa Bunge,” alisema.
Alisema lazima ifahamike kuwa sheria hiyo
imechelewa kupelekwa bungeni na inawezekana watu wanaizungumza kwa lugha ya
wamiliki fulani na kuongeza kuwa kama wanahabari wataanza kufanya hivyo,
watakuwa wanapotea.
“Kwa sababu katika Muswada wa awali
niliouona sifahamu wabunge watakachoamua, lakini niliyoyaona ni ya kulinda
maslahi ya wanahabari wote na kutakuwa na chombo cha kusimamia taaluma kama
taaluma nyingine.
“Sasa kwa kuwa sitaki kuzungumzia sana
yaliyopo bungeni, yamekugusa wewe Katibu (Henry Muhanika- Katibu Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania
(MOAT), nilijua utakuwa
bungeni kuutetea na kuwashauri wabunge, naona sehemu nzuri ni bungeni,” alisema
akimjibu Muhanika aliyeuliza swali.
Kuhusu madai ya kuhongwa kwa baadhi ya
wabunge wa CCM, ili wapitishe Muswada huo kuwa Sheria, Rais Magufuli alisema
hataki kuingilia chombo chenye mamlaka ya kuamua na endapo kuna wabunge
wamehusika kuchukua fedha ili kuruhusu Muswada huo kupita kama ilivyodaiwa na
Mbowe (Freeman, Mwenyekiti wa Chadema) vyombo vinavyohusika vichukue hatua.
Alisema kama ni chama fulani kimezungumza
kwa lengo fulani, ni vema wanaohisi suala hilo wakaungane nao, maana Bunge lina
mamlaka zake na vyombo kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru)
kupitia sheria namba 3 ya mwaka 2016 hivyo vitatumika kufanya kazi.
0 comments:
Post a Comment