Celina Mathew
RAIS John Magufuli amesema Serikali imeagiza ndege
nyingine nne mpya, kwaajili ya kufufua Shirika la Ndege ya Tanzania (ATCL),
liwe na ndege saba, zikiwemo sita mpya.
Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari
Ikulu Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema tayari malipo ya awali ya ndege
hizo zote yameshatolewa na Serikali.
Alifafanua kuwa, ndege tatu za mwanzo zimeshalipiwa
asilimia 30 ya bei na zimeshaanza kutengenezwa; moja ni aina ya Mbombdier Q400
itakayowasili Juni mwakani, kama mbili zilizoingia nchini Septemba mwaka huu.
Nyingine mbili ambazo nazo zimeshalipiwa asilimia 30 ya
bei kwa mujibu wa Rais Magufuli ni JET CSC 300; ambazo zitakuwa na uwezo wa
kubeba abiria 137 hadi 150, zinazotarajiwa kufika nchini mwanzoni mwa 2018.
Rais Magufuli alitaja mpango mwingine wa kununua ndege
aina ya Boeing, yenye uwezo wa kubeba abiria 242, ambazo kabla ya mchakato wa
ununuzi kuanza, walitakiwa kulipa dola za Marekani milioni 10, ambazo zimeshalipwa,
hivyo mazungumzo ya awali yataanza mwezi huu.
Alisema Serikali inafanya hivyo kwa kuwa anaamini kuwa
nchi inajenga utalii, sekta ambao haiwezi kujengwa wakati kuna ndege za
kubahatisha.
Alifafanua kuwa ununuzi wa ndege hizo kubwa, Jet mbili
na Boeing moja, unalenga kuwezesha Taifa
kuwa na ndege za moja kwa moja kutoka Marekani, China au Urusi na katika
mataifa mengine hadi Tanzania, ili watalii waje kwa wingi badala ya kwenda nchi
zingine.
Alisema ifikapo 2018 mwanzoni, Tanzania itakuwa na ndege
saba jambo litakalosaidia nchi kufika mahali pazuri na kuifanya kuwa ya utalii.
Reli
Mbali na ndege kwaajili ya sekta ya utalii, Rais Magufuli
alisema nchi pia Serikali imeamua kujenga Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa
cha Standard gauge, ambapo Sh trilioni moja zimeshatengwa na wakandarasi 40
wameshachukua zabuni na zinatarajiwa kurudishwa mwezi huu.
Alisema reli hiyo kwa awamu ya kwanza itaanzia katika Jiji
la Dar es Salaam na kufika Morogoro.
Alifafanua kuwa amedhamiria kutekeleza miradi ya
maendeleo kwa kuhakikisha bajeti ya asilimia 40 iliyotengwa kwaajili ya
maendeleo inapelekwa.
Hakuna kula tena
Rais Magufuli alisema alikuta bajeti ya maendeleo ikiwa
asilimia 26, jambo lillilosababisha sehemu kubwa ya mapato ya Serikali, itumike
kwaajili ya kula na kusisitiza kuwa Watanzania walikula sana na sasa wakati wa
kula umekwisha.
Katika kuhakikisha fedha hizo za maendeleo zinapatikana
kama ilivyopangwa, Rais Magufuli alisema amepunguza gharama za matumizi yasiyo
ya lazima pamoja na safari za nje.
Alisema katika kubana matumizi alimua kuhudhuria mikutano
mitatu kati ya 47 aliyoalikwa na nchi nyingine na kuagiza wasaidizi wake wakiwemo mabalozi
waliopo nchini humo wamuwakilishe.
“Unaweza kukuta sisi tukaenda huko tukajisomba watu 100
wakati fedha hizo wananchi wanahangaika na zingewasaidia mahospitalini, hivyo
nimefanya hivyo ili kuhakikisha kunakuwa na Tanzania mpya yenye mwelekeo,”
alifafanua.
Alisema kupunguza safari za nje hakukuwa na madhara, kwa
kuwa hakukuzuia nchi nyingine kuja hapa nchini kwa kuwa hadi sasa marais zaidi
ya saba wameshakuja nchini na bado wanaendelea.
Rais Magufuli alisema kwa kufanya hivyo, kumesaidia hata
nchi nyingine kuja kutembelea Tanzania, ikiwemo kutembelewa na viongozi wan chi
za Vietnam, Morocco, Rwanda na nyinginezo kuashiria kuwa anabana matumizi.
Alisema pia kubana matumizi kumemsadia kuchaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Taasisi ya Troika ya Jumuiya
ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), inayojihusisha na masuala ya siasa na
kwa lengo la kujenga nchi kwanza kabla ya kwenda nyingine.
“Naona tunaenda vizuri ndio maana nimepunguza sherehe za
Uhuru ambazo tungesheherekea tukamaliza; badala yake fedha zake nimejengea
Barabara ya Mwenge ambayo Watanzania wanapita bila changamoto ya foleni jambo
ambalo ni maendeleo,” alisema.
Aliongeza kulikuwa kuna sherehe nyingine ambazo fedha
zake zilipelekwa Mwanza na alifanya hivyo ili kurudisha imani ya Watanzania
katika kuwatumikia.
Pia, alisema Bunge lilibana matumizi na kutoa fedha
ambazo zilipekelekwa hospitalini kwa ajili ya kusaidia kina mama katika masuala
ya dawa na vitendea kazi hospitalini.
0 comments:
Post a Comment