Grace Gurisha
HATIMAYE aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na
Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona katika Serikali ya Awamu ya Tatu, leo
wanahitimisha kifungo cha miaka miwili, kilichoambatana na kifungo cha nje cha kufanya
usafi.
Mramba na Yona wanamaliza kifungo hicho leo baada ya
kufanya usafi kwa saa nne kila siku kwenye hospitali ya Palestina, Sinza, Dar
es Salaam, kama walivyopangiwa na baada ya hapo watakuwa huru uraiani.
Mawaziri hao walipitia wakati mgumu walipokuwa wakifanya
usafi kwenye hospitali hiyo kutokana na wadhifa na heshima waliyokuwanayo ndani
na nje ya nchi.
Awali mawaziri hao wa zamani walitumikia kifungo cha
miaka miwili jela, lakini baadaye walibadilishiwa kifungo hicho na kuwa cha nje,
baada ya kuonesha utiifu gerezani kwa kufanya kazi walizopangiwa kwa bidii.
Baada ya tathmini ya utii wao iliyofanywa na Jeshi la
Magereza kukamilika, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilibariki uamuzi huo wa kupewa
adhabu ya kifungo cha nje.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha alisema
sheria ya huduma kwa jamii namba sita kifungu namba 3(1) ya mwaka 2002, inasema
mtu anayetiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni miaka mitatu kurudi chini,
Mahakama inaweza kumpa adhabu ya kutumikia jamii.
Mramba na Yona baada ya rufaa walibaki na adhabu ya miaka
miwili, ambapo walitiwa hatiani kwa kutumia madaraka vibaya na walipaswa kumaliza
kifungo mwezi huu.
Hakimu Mkeha alisema Magereza walifikisha barua
mahakamani hapo Desemba 5, mwaka jana, wakipendekeza kifungo cha nje kwa
mawaziri hao.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo ya Mkeha, baada ya kupokea
barua hiyo Mahakama iliamuru watu wa huduma za jamii kuchunguza kama
wanastahili kupewa adhabu hiyo na baada ya uchunguzi walirudisha ripoti kwamba
wanastahili.
Hakimu Mkeha alisema vigezo vya kupewa adhabu hiyo ni
umri mkubwa ambapo Mramba na Yona wana umri wa miaka 75 na kama wahusika ni
wakosaji wa mara ya kwanza.
Kigezo kingine ni kama watuhumiwa walijutia kosa lao na kukubali
kuitumikia jamii bila kulipwa, kuangalia umbali wanakoishi na eneo wanalokwenda
kufanyia shughuli za kijamii na tabia za washitakiwa.
Hakimu Mkeha alisema sheria haijapendekeza makosa yapi
wasipewe kifungo cha nje, isipokuwa imetamka kwa yeyote aliyefungwa kuanzia
miaka mitatu kushuka chini.
“Mramba na Yona baada ya kuridhika kwamba wanashitakiwa,
wamepangiwa kufanya usafi hospitali ya Palestina Sinza kila siku na watatumikia
hadi Novemba 5. Watakuwa wanafanya kazi kwa saa nne,” alisema Hakimu Mkeha.
Julai 6, mwaka jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
iliwahukumu kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya Sh milioni tano, huku
ikimwacha huru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja baada ya
kumwona hana hatia.
Walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya
madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 kwa kutoa msamaha
wa kodi kwa kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya M/S Alex Stewart ya
Uingereza.
Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la majaji watatu, Saul
Kinemela, Sam Rumanyika na John Utamwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jopo hilo.
Kwa mara ya kwanza washitakiwa hao walifikishwa
mahakamani hapo mwaka 2008. Hata hivyo, Oktoba 2, mwaka jana walipinga adhabu
hiyo na kukata rufaa.
Katika rufaa waliyokata Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam mbele ya Jaji Projest Rugazia, walipunguziwa adhabu kwenye kuisababishia
Serikali hasara, hivyo wakabaki na adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela kwa
kutumia madaraka vibaya.
0 comments:
Post a Comment