Hussein Ndubikile
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa |
WANAFUNZI wa Chuo cha Elimu ya Biashara
cha Dar es Salaam (CBE) wamemwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenda kujionea
changamoto zinazowakabili kabla ya Siku ya Mahafali yanayotarajiwa kufanyika
Novemba 12.
Changamoto hizo kwa mujibu wa wanafunzi
hao ni pamoja na uhaba
wa vyumba vya madarasa na madawati.
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa
chuo hicho kushindwa kuzifanyia kazi hali inayosababisha wanafunzi hao kufanya
vibaya katika masomo yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais wa
Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho (COBESO), Murshid Marijani kwenye mkutano
wa kwanza wa Baraza la Wanafunzi la Chuo uliowakutanisha na Menejimenti ya Chuo.
Alisema wanafunzi wamekuwa wakishindwa
kufanya vizuri kwenye masomo yao kutokana na ubovu wa miundombinu ikiwamo ya
mrundikano wa wanafunzi madarasani huku akisisitiza kuwapo takribani wanafunzi
1,786 wanaorudia masomo.
"Wanafunzi 1,786 wanarudia masomo kutokana
na mrundikano madarasani, vyumbani kuna joto kali linalowasumbua, uhaba wa
madawati na walimu kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo," alisema.
Marijani alisema atahakikisha anakutana
na Waziri Mkuu Majaliwa ili amweleze changamoto zilizoshindwa kutatuliwa huku
akibainisha kuwa Rais wa Wanafunzi ni miongoni mwa wanaochangia hayo kwa
kushindwa kuongoza ipasavyo Serikali iliyomaliza muda wake.
Alisisitiza kuwa hadi sasa chuo hakina
mfumo wa mtandao hali inayowafanya wanafunzi kushindwa kupata taarifa za
kimasomo na kuendana na mfumo wa kielimu duniani, huku akiongeza kuwa gharama
za vyumba vya kulala katika chuo hicho ni kubwa ikilinganishwa na vyuo vingine.
Alifafanua kuwa wanafunzi wanaoishi
mabwenini, hupata usumbufu kutokana na kunguni, hivyo aliuomba uongozi upulizie
dawa kuwaondolea adha hiyo.
Pia alisema mikopo ya wanafunzi imekuwa
ikicheleweshwa na viongozi wanaohusika na kusababisha shida kwa wanafunzi
wanaotegemea fedha hizo kuendesha maisha yao.
Alizitaja pia za uhaba wa vibweta, usumbufu
wa wasimamizi wa mitihani kwa wanafunzi, unyanyasaji wanafunzi unaofanywa na
walimu wa idara, maabara isiyotosheleza idadi ya wanafunzi na ubovu wa vyoo.
Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada
ya Usimamizi wa Biashara, Vailet Monyo alisema chuo kinakabiliwa na ukosefu wa
uandaaji semina na mafunzo ya kompyuta kwa vitendo.
Mwanafunzi Michael Mniko alisema
wahadhiri wa chuo hicho wamekuwa hawafundishi vizuri ila cha kushangaza wanatoa
kazi darasani bila kujali kuwa wanafunzi
hawaelewi.
Mkuu wa Chuo, Profesa Emmanuel Mjema
alisema kiasi cha ada wanacholipa wanafunzi hao hakitoshelezi kutatua matatizo
yote ya chuo.
"Ada ya Sh milioni 1.5 kwa
wanafunzi wa Shahada, Sh milioni 1.2 Astashada na Cheti Sh 990,000 hazitoshelezi
kuweka kompyuta madarasani," alisema.
Alisema CBE ni miongoni mwa vyuo bora
nchini na Afrika Mashariki hivyo aliahidi baada ya miezi miwili tatizo la
mtandao litatatuliwa pamoja na chuo hicho kuuzia wanafunzi kompyuta mpakato kwa
gharama nafuu.
Mjema alisema ukarabati wa miundombinu
ya vyoo, mabweni na ubadilishaji wa bwalo la chakula ili kuwa maabara kwa lengo
la kuwezesha kupata elimu katika mazingira yanayoridhisha.
0 comments:
Post a Comment