Joyce Anael, Moshi
Manispaa ya Moshi |
MBUNGE wa Moshi Mjini, Jafary Michael ametoa rai kwa
Mamlaka husika kukamilisha mchakato wa kuifanya Manispaa hiyo kuwa Jiji bila
kuhusisha itikadi za kisiasa.
Jaffary alitoa rai hiyo juzi wakati akizungumza na
waandishi wa habari mjini hapa, ambapo alisema mchakato huo una harufu ya
itikadi za kisiasa, hivyo ni vema siasa zikawekwa pembeni na mchakato
ukakamilishwa.
“Mchakato wa Manispaa ya Moshi kuwa Jiji ulianza muda
mrefu na haujakamilika hadi sasa na kuna kila dalili kuwa unatekelezwa kwa
kufuata itikadi za kisasa,” alisema.
Aidha, alisema tayari wamepanua mipaka hadi kilometa za mraba
142, na sasa wanahitaji Tamisemi ibariki mipaka hiyo na Rais kutangaza kuwa
Jiji.
“Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam
Lukuvi tayari amesaini sisi kupanuka kutoka kilometa za mraba 58 hadi 142, na
mchakato huu umekamilika na sasa tunahitaji baraka za Tamisemi kupitia kwa Rais
ili tuweze kuwa Jiji,” alisema.
Alisema katika kushughulikia masuala ya kimaendeleo, Mamlaka
husika hazina budi kuweka pembeni itikadi za kisiasa kutokana na ukweli kuwa watakoathirika
ni wananchi na chama au vyama vya siasa.
Alisema kuna haja ya Rais kuelewa kuwa hakuna gharama kubwa
zinazohitajika kuipandisha Moshi kuwa Jiji na badala yake itasaidia kukuza
uchumi wa wakazi wa eneo hilo na Taifa kwa jumla.
Aliongeza kuwa taratibu zote za upanuzi wa mji wa Moshi
kuwa Jiji zilifuatwa tangu mwaka 2012 kwa kutumia kodi za wananchi ambazo ni
zaidi ya Sh milioni 100, zilizotumika kuelimisha wananchi na michakato mingine.
“Makao makuu ya nchi yanakwenda Dodoma, na katika hili
nadhani Manispaa ya Dodoma itapandishwa hadhi kuwa Jiji, sasa ninamwomba Rais
John Magufuli, kabla ya kutangaza Dodoma kuwa Jiji aangalie pia mji wa Moshi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment