Abdallah Amiri, Igunga
VIONGOZI wa
vyama vya siasa nchini wametakiwa kuacha kuwalinda wahalifu ikiwamo wanaokata
miti ovyo na kuacha mifugo ikizurura mijini.
Wito huo
umetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora,
Revocatus Kuuli alipozungumza na wanahabari juzi.
Alisema baadhi
ya wanasiasa wamekuwa mstari wa mbele kuwatetea wahalifu kwa kisingizio cha
kulinda kura zao za mwaka 2020, akisema kwa nafasi yake hawezi kuunga mkono
jambo hilo hata kidogo.
Kuuli alisema
kwamba kila kiongozi aliyechaguliwa ana wajibu wa kusimamia wananchi wake kwa
kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira ili wilaya isiendelea kuwa jangwa.
Mkurugenzi huyo
alisema kwamba kuanzia sasa mwanasiasa yoyote atakayefika ofisi kwake kwa lengo
la kumtetea mhalifu wa mazao ya misitu hatakuwa rafiki yake.
Alibainisha
kwamba hivi sasa halmashauri yake kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la
Heifer wamejipanga kuotesha miti laki tano ambayo wataisambaza maeneo
mbalimbali wilayani humo kwa ajili ya kukabiliana na jangwa.
Kuuli pia
ameonya kwamba baiskeli itakayokamatwa imebeba mikaa au kuni itataifishwa na
kuuzwa kwa wananchi na fedha hizo zitaingizwa serikalini.
Alidai kwamba
kuni zote zitakazokamatwa na idara yake ya maliasili watapewa Idara ya Magereza
kwa ajili ya kutumia wafungwa, huku mifugo inayozurura mwenye mali
atakayekamatwa atatozwa elfu 50,000/=.
0 comments:
Post a Comment