Christopher Bageni |
TAKRIBANI miezi miwili baada ya Mahakama
ya Rufani kumhukumu kunyongwa hadi kufa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya
Kinondoni (OC-CID), Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni, kigogo huyo wa
polisi ameibuka na kutaka hukumu hiyo kupitiwa upya kwa maelezo kuwa ilikuwa na
makosa.
Bageni ambaye mahakama hiyo ilimtia
hatiani kwa kosa la mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge
mkoani Morogoro, alitoa waraka jana akichambua hukumu hiyo kupitia Wakili wake Gaudioz
Ishengoma na kusisitiza kuwa hakutendewa haki.
Katika hukumu hiyo ya kitanzi inayolalamikiwa
na Bageni iliyosomwa Septemba 16 mwaka huu, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa mkoa
wa Dar es Salaam (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na maofisa
wengine wawili wa Polisi, Ahmed Makelle na Rajabu Bakari waliachiwa huru, baada
ya Mahakama kuwaona kuwa hawana hatia.
Bageni alihukumuwa adhabu hiyo baada ya
mahakama ya Rufani kukubaliana na rufaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye
alikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwaachia huru katika kesi ya
mauaji ya wafanyabiashara hao.
Wafanyabiashara hao, Savings Chigumbi,
Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva teksi wa Manzese, Juma Ndugu,
waliuawa Januari 14, 2006, kwa kupigwa risasi Mbezi Luis, Dar es Salaam.
Katika waraka huo, Bageni ameitaka
mahakama ifanye marejeo ya hukumu yake ya Septemba 13 mwaka huu, akisisitiza
kuwa mtoa maombi alinyimwa haki sawa ya kusikilizwa wakati wa kutathmini ushahidi
ulioko kwenye kumbukumbu za mahakama kwa kuegemea kwenye ushahidi wa upande wa
mashtaka pekee.
“Kwamba katika kuchanganua ushahidi
ambao uamuzi wa mahakama uliegemea, mahakama ilishughulika tu na ushahidi wa msingi (Exam in Chief) wa upande
wa mashtaka na iliangalia kwa juu juu tu ushahidi wa utetezi hususan wa mtoa maombi,”
alisema Bageni katika waraka huo.
Katika ufafanuzi wake, Bageni alisema
kuna kukinzana kwa haki kwamba mtoa maombi alinyimwa haki sawa ya kusikilizwa,
kwa mahakama kuchagua na kuegemea kwenye upande wa mashtaka pekee na kushindwa
kuzingatia ushahidi wa upande wa utetezi.
Alisema uamuzi wa mahakama umetolewa
katika msingi wa makosa ya dhahiri kwenye kumbukumbu za mahakama na hivyo kupelekea upotoshaji wa haki.
Akielezea upotoshaji huo wa haki
alisema, “kuzingatia mwongo wa kanuni katika asili, thamani na matumizi ya
ushahidi wa kuungwa mkono, kushindwa kuchanganua na kutathmini ushahidi kwa umakini kwenye kumbukumbu,”
“Mahakama ilishindwa kuainisha kwamba
ushahidi wa mjibu rufaa wa Nne (Mtoa maombi) kimazingira kama ilivyo, ni dhahiri
kwamba unakosa thamani ya kuhitaji ushahidi wa kuunga mkono, na hivyo si salama
kuuegemea katika kumtia hatiani,” alisema.
Katika maelezo hayo, Bageni alisema
mahakama ilishindwa kubaini kwamba katika ujumla wake ushahidi wa upande wa
mashtaka haukuweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka, huku akishangaa
mahakama ya rufani kwa kushindwa kuamua rufaa hiyo.
“Kwa kutenguliwa kwa uamuzi wa kuachiwa
huru kwa mtoa maombi na kubadilishiwa kwa kutiwa hatiani na hivyo kuhukumiwa
adhabu ya kifo…, kwa sababu ya hoja
zilizotolewa katika taarifa ya maombi haya yafaa kwamba mahakama hii ifanye marejeo ya uamuzi wake ili kurekebisha
upotoshwaji wa haki,” alisema.
Tayari wake za marehemu wafanyabiashara
hao wa madini wa Mahenge, wameeleza nia yao kufungua kesi dhidi ya Serikali
kuidai fidia wakisema hukumu ya kesi hiyo imeonyesha waume zao wameuawa
kimakosa.
0 comments:
Post a Comment