Mke wa Magufuli azua gumzo Kenya


NAIROBI, Kenya

Janeth Magufuli hospitalini
PICHA ya Rais John Magufuli akimjulia hali mkewe, Janeth, aliyelazwa katika Hospitali Kuu ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, imeibua mjadala mzito miongoni mwa Wakenya.

Picha ya CCTV iliyotolewa juzi na Ikulu ya Tanzania ilimwonesha Magufuli na mkewe akiwa katika hospitali hiyo ya rufaa.

Hata hivyo haikufahamika mara moja Janeth anasumbuliwa na nini lakini hospitali alimolazwa, ina hadhi sawa na hospitali ya Taifa ya Kenyatta iliyoko jijini hapa.

Rais Magufuli, kutokana na vitendo vyake, anatoa changamoto kwa marais wengine wa Afrika na maofisa wa serikali wanaopendelea kupeleka wagonjwa wao katika hospitali za ng’ambo hata kwa magonjwa madogo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, hospitali hiyo ina eneo la meta za mraba 3,700 la wagonjwa wa nje linalohudumia watu 1,000 kwa siku.

Ina vyumba 34 vya kuchunguza wagonjwa, famasia na majengo ya mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari na wataalamu wengine wa afya.

Changamoto hiyo ya Magufuli inakuja siku chache baada ya Gavana wa Bomet, Issac Rutto kwenda Afrika Kusini kupata tiba maalumu ya jeraha kwenye jicho lake.

Jeraha hilo lilitokana na kipande cha bomu la kutoa machozi kilichompata baada ya kurushwa na polisi waliokuwa wakitawanya kundi la watu kwenye uwanja wa Silibwet, Bomet.

Agosti, Rais mstaafu Mwai Kibaki alifanyiwa upasuaji uliofanikiwa wa mshipa wa shingo nchini Afrika Kusini.

Mkuu huyo wa Nchi wa zamani alilazwa kwenye hospitali ya Netcare Sunninghill jijini Johannesburg, baada ya kupewa rufaa kutoka hospitali ya Karen.

Vyanzo vya habari kutoka familia yake, vilisema alipelekwa Afrika Kusini kutokana na ushauri wa madaktari wake.  

Wakati huo huo, Salha Mohamed anaripoti, kwamba Mama Magufuli aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Sewahaji ameruhusiwa na kurejea nyumbani.

Mama Magufuli aliruhusiwa jana baada ya afya yake kuimarika kwani alipelekwa Muhimbili baada ya kuugua ghafla na kupoteza fahamu.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa alisema kabla ya kuondoka Sewahaji, Mama Magufuli alishukuru madaktari na wauguzi wa Muhimbili kwa matibabu mazuri aliyopata.

Pia alishukuru Watanzania wote kwa kumwombea afya njema ambapo alimshukuru Mungu kwani afya yake imeimarika.

"Napenda kushukuru madaktari na wauguzi, nimepata huduma nzuri sana maana siku nilipoletwa hapa, sikuwa na fahamu na hali yangu ilikuwa mbaya, lakini mmenipigania na leo narudi nyumbani nikiwa na afya njema.

"Naomba pia nishukuru Watanzania wote kwa kuniombea, nawahakikishia kuwa sasa niko vizuri na madaktari wameniruhusu nirudi nyumbani ambako nitamalizia matibabu yangu," alisema Mama Magufuli.

Mama Magufuli alilazwa hospitalini hapo tangu juzi baada ya kuugua ghafla na kupoteza fahamu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo