Leonce Zimbandu
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza
kuanza mchakato wa ujenzi wa vituo 20 vya Polisi vitakavyogharimu Sh bilioni
10.
Mkoa wa Dar es Salaam umegawanywa kwenye Manispaa tano,
hivyo kila wilaya vitajengwa vituo vinne
na kila kituo kitajengwa kwa gharama ya Sh milioni 500.
Makonda alisema hayo kwenye taarifa yake aliyoisambaza
kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kuonya viongozi wasitumie fursa
kutengeneza fomu zao kwa ajili ya kujinufaisha.
“Nimepata taarifa kuwa baadhi ya viongozi wametengeneza
fomu na kuzipitisha mitaani kwa wananchi kwa madai ya kutekeleza agizo la
ujenzi … hatua kali itachukuliwa,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa Makonda alizitaka kamati za ulinzi
na usalama za wilaya na mkoa wa Dar es Salaam, kupeleka mchanganuo wa maeneo
ambako vituo hivyo vyenye uwezo wa kuchukua askari 100 vitajengwa.
Hatua hiyo ya Mkuu wa Mkoa ilitokana na ziara aliyofanya katika
baadhi ya vituo vya Polisi ili kujionea hali halisi ya vituo hivyo na kupokea
malalamiko na changamoto kutoka kwa wananchi.
Changamoto kubwa zilikuwa ni wananchi kukosa huduma kwenye
vituo vya Polisi kwa saa 24, mazingira mabovu ya vituo hivyo na polisi
kushindwa kufika kwenye matukio kwa wakati.
Nyingine ni askari kushindwa kutoa huduma kutokana na
upungufu wa askari na majambazi kuvamia vituo vya Polisi kwa lengo la kuchukua
silaha.
0 comments:
Post a Comment