Salha Mohamed
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
inatarajia kuweka kambi ya upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua.
Upasuaji huo utakaoanza kesho katika
taasisi hiyo, utashirikisha madaktari kutoka nchini Australia na jopo la
madaktari hospitalini hapo.
Akizungumza jana na JAMBO LEO, Ofisa
habari wa taasisi hiyo, Maulid Mohamed alisema upasuaji huo utahusisha kufungua
kifua na kuutibu moyo.
“Upasuaji huo utakuwa mkubwa kwa
kufungua kifua na kuutibu moyo, leo (jana) tutaanza kuwaangalia wagonjwa
wanaohitaji kufanyiwa upasuaji huo,” alisema.
Alisema tayari wameshaanza kufanya uchunguzi
wa awali kwa wagonjwa hao kabla ya upasuaji ili kuangalia afya ya mgonjwa kabla
ya kufanya upasuaji.
Alisema upasuaji huo utahusisha watu
wazima na watoto wenye matatizo ya moyo wapatao 35.
Maulid alisema ili kufanikisha upasuaji
huo inahitajika damu ya kutosha ili kuweza kufanikisha matibabu hayo kwani
utahusisha kufungua kifua.
“Kufungua kifua kutahitaji damu zaidi,
ambapo unaweza kukuta mtu mmoja wakati wa upasuaji anahitaji chupa 6 hadi 10,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo,
zinahitajika chupa takribani 200 za damu
ili kuweza kufanya upasuaji huo kwa ufanisi zaidi.
0 comments:
Post a Comment