Mbowe achafua hali ya hewa bungeni


Sharifa Marira, Dodoma

Freeman Mbowe
KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amechafua hali ya hewa bungeni, baada ya kusema wabunge wa CCM wamehongwa Sh milioni 10 kila mmoja ili kupitisha Muswada wa Huduma ya Habari na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/18.

Mbowe alitoa tuhuma hizo wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu jana ambapo pia kambi hiyo ilimshauri Rais John Magufuli ‘kumtumbua’ Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ikisema ndiye aliyeongoza kikao kilichotoa rushwa hiyo.

Kambi hiyo pia ilitaka ‘kutumbuliwa’ kwa Baraza la Mawaziri ikieleza kuwa limepoteza sifa, kwani viongozi wa umma hawapaswi kupokea rushwa.

Mbowe alisema wabunge na mawaziri ni viongozi wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, namba 13 ya mwaka 1995 lakini kuna taarifa kuwa Jumanne saa mbili usiku katika kikao cha ndani cha CCM, fedha hizo zilitolewa.

Kwa mujibu wa Mbowe, kikao hicho cha wabunge wa CCM kiliitishwa na Waziri Mkuu Majaliwa na kuratibiwa na Naibu Katibu wa CCM, Abdallah Ulega na mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana.

“Tuna taarifa kwamba kwenye kikao hicho ambacho lilijadiliwa suala la Muswada wa Habari ambao unawasilishwa bungeni kesho (leo) na Mpango wa Maendeleo ya Taifa ambao umeshawasilishwa mliamua kuwapa zawadi wabunge wote Sh milioni 10,” alisema Mbowe.

Alisema kwa taarifa alizonazo, fedha hizo zilitolewa kwa wabunge, mawaziri, Spika na Naibu Spika ili kufanikisha kupitisha hoja hizo, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo, Mbowe alikwenda mbali zaidi kwamba mgao huo uliendelea kutolewa katika ofisi za CCM makao makuu ukiratibiwa na Naibu Katibu wa Wabunge wa CCM (Ulega) ambaye pia ni Mbunge.

“Je, Waziri Mkuu taarifa hizi ni za kweli?” Alihoji Mbowe.

Hata hivyo, Naibu Spika Dk Tulia Ackson alizuia swali hilo kujibiwa akisema maswali kwa Waziri Mkuu ni yanayohusu sera kwa hiyo wabunge wakumbushane vizuri na kumtaka Mbowe aulize swali linalohusu sera.

Mbowe alirudia swali lake na kudai kuwa masuala ya rushwa na masuala ya maadili ya viongozi ni sehemu ya sera.

“Kama Bunge hili linataka kuaminishwa kuwa masuala haya ambayo ni rushwa si ya kisera masuala ambayo yako ‘ serious’ kwa Taifa, hutaki Waziri Mkuu atoe majibu, Waziri Mkuu tunaomba ujibu swali tafadhali na Naibu Spika tuachie Waziri Mkuu ajibu swali hili, ni swali la kisera,” alisema Mbowe.

Kutokana na hali hiyo, Dk Tulia alimwambia Mbowe ataruhusu Waziri Mkuu kujibu maswali yanayohusu sera kama ambavyo atamzuia mwingine yeyote.

“Kwa hiyo hata wewe ndio maana nimekupa nafasi tena, ili uulize swali linalohusu sera ndivyo kanuni zetu zinavyosema,” alisema Dk Tulia.

Mbowe na Dk Tulia waliendelea kuvutana kuhusu swali hilo na Mbunge huyo wa Hai alipopewa nafasi tena, alirudia na kusisitiza suala la rushwa katika Taifa ni la kisera, linatokana na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 na ni matunda ya sera.

“Kwa hiyo hili swali ni la kisera na sijasema tuhuma hizi ni za kweli ila nimeuliza Waziri Mkuu atujibu ni za kweli au si za kweli, Naibu Spika unalinda nini?” Alihoji Mbowe.

Kutokana na kauli hiyo, Dk Tulia alisema: “Nadhani kwa hapa sasa tulipofika kama wewe unaona hili swali ni la sera, kanuni hizi ndio zinaniongoza mimi, kwa maana hiyo nitaendelea na maswali mengine.”

Mwongozo

Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde aliomba Mwongozo kwa Spika akidai kuwa swali hilo halijapewa majibu sahihi na kutaka liundiwe tume huru ya kimahakama ya kibunge ili lifanyiwe uchunguzi ndani ya Bunge.

Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia aliomba Mwongozo akitaka Mbowe athibitishe kauli yake ndani ya Bunge, ya wabunge wa CCM kupewa fedha hizo na kama hawezi kuthibitisha hatua zichukuliwe na Bunge.

Akijibu miongozo hiyo Dk Tulia alifafanua sababu ya kuzuia kujibiwa kwa swali la Mbowe kuwa ni kutokana na kuongelea mambo ya rushwa ambapo kwa mujibu wa sharia, vipo vyombo maalumu vya kushughulikia na si Bunge.

Alisema pia hawezi kumwambia Mbowe athibitishe kauli yake kwa wabunge kwa sababu suala hilo alilizuia na kusisitiza kuwa kama kuna ushahidi upelekwe sehemu husika na baada ya chombo hicho kufanya kazi ikithibitishwa watachukua hatua, kwa sababu watakuwa wamevunja sheria.

Nje ya Bunge

Kambi ya Upinzani imesema itamwandikia barua Rais John Magufuli kumshauri ‘amtumbue’ Majaliwa kutokana na kudaiwa kuhusika kwenye suala hilo, pamoja na kuundwa kwa tume ya kimahakama ili ichunguze suala hilo.

Mbowe ambaye alizungumza na waandishi wa habari kufafanua suala hilo, alisema Ulega aliita wabunge wa CCM akiwambia Waziri Mkuu ana nia ya kukutana nao na kutakuwa na mgeni rasmi ambaye ni Kinana na katika kikao hicho wabunge hawakufurahishwa na namna Serikali inavyoendeshwa, mdororo wa kiuchumi, kukosekana kwa huduma za jamii na mambo yanayolikabili Taifa.

“Waziri Mkuu na Kinana walijaribu kuwatuliza wabunge ili waivumilie Serikali na kulinda chama chao ikiwa ni pamoja na kupitisha mambo haya mawili na fedha hizo ziligawiwa kwenye bahasha za khaki na dada anayeitwa Mariam, tunao ushahidi wa kutosha,’’ alisema Mbowe.

Alisema tuhuma hizo ni nzito zinamhusu Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri zinahusu Bunge na uongozi wa Bunge ilistahili Serikali kujiuzulu na alipomwuliza Waziri Mkuu kama angesema si kweli angemtaka kuundwa kwa tume ya kimahakama, kwa sababu Bunge haliwezi kujichunguza.

“Inapofika hatua sasa Dola inahonga wabunge, tuna Serikali hapa? Tumewabana wabunge wa CCM wengine wamesema ni kutokana na maisha magumu kama Mbunge analipwa Sh milioni 10 kwa mwezi, anasema maisha ni magumu hao wananchi wanalipwa na nani?” Alihoji Mbowe.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisema mtihani mkubwa wa pili ambao anatakiwa Rais aufanye na kufaulu, ni kuchukua hatua ya ‘kumtumbua’ Waziri Mkuu ili asikwepe.

Alisema Rais afikirie upya uteuzi wa Dk Tulia kwa kuwa ana mamlaka ya kumwondoa na umefika wakati wa kuyatumia kumwondoa bungeni kwa kuwa hafai.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo