Celina Mathew
Edson Mwakyombe |
MWANAFUNZI wa mwaka wa kwanza wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Edson Mwakyombe, ambaye alimwaga chozi kwa
kukosa mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB),
amepata mama wa kumlea akiwa chuoni hapo hadi atakapomaliza masomo.
Mama huyo anayejulikana kwa jina la
Isariah Mathias alijitokeza juzi akitangaza kumdhamini katika masomo yake ya
mwaka wa pili lakini pia kwa masuala mbalimbali akiwa chuoni hapo, huku
akisema: “Mimi ndiye mama wa Edson kwa hapa Dar es Salaam, nimejitolea kumlea.”
Akizungumza na JAMBO LEO jana, Isariah alisema
akiwa mzazi na mama, aliguswa na ujumbe wa picha ya Edson akilia kwa kukosa
mkopo wa elimu ya juu, kwenye mtandao wa Instagram wa rafiki yake aliyemtaja
kwa jina la Angela.
Alisema baada ya kuona taarifa hiyo alimwomba
rafiki yake huyo simu, kisha akaandika kwamba ameguswa, na kuomba kuwa sehemu
ya watakaomsaidia Edson ili kufanikisha ndoto yake, kisha kuweka namba ya simu
chini.
Alisema baada ya kuandika ujumbe huo,
rafiki yake huyo alituma ujumbe kwa Wakili Albert Msando ambaye ni Mratibu wa
ufuatiliaji wafadhili kwa kijana huyo ambaye aliahidi kumtafuta mwanafunzi huyo
chuoni hapo.
“Muda mfupi baadaye, nilipokea simu ya mtu
aliyejitambulisha kwa jina la Msando akasema amempata Edson akitaka nimwelekeze
pa kunipata,” alisema.
Aliendelea kueleza kuwa aliwaambia
atawatafuta, lakini Msando alimsihi kumfuata ofisini kwake na kumkubalia.
Alisema Msando alifika ofisini hapo
akiwa na Edson na kumweleza kuwa atamsaidia kwa kumlipia ada ya mwaka wa pili
akiwa chuoni hapo na katika masuala mbalimbali ya kawaida.
“Nilizungumza na Edson kwa kirefu
akaniambia amefiwa na baba yake, jambo ambalo lilinihuzunisha, hivyo nikamsihi
kuwa nitamlipia ada na nikamwambia kuwa nitakuwa mama yake kwa sasa katika kila
hali,” alisema.
Mathias alisema kujitolea kwake si kutokana
na utajiri bali amekuwa na tabia ya kusaidia watu hali inayomsababishia
kutopungukiwa na badala yake Mungu kuzidi kumbariki.
Mzazi huyo alitoa mwito kwa watu wengine
walioguswa kujitokeza kusaidia wanafunzi wengine maana si mmoja aliyekosa mkopo,
bali wapo wengi ili kuwawezesha kutimiza malengo yao ya kimasomo.
Mfadhili mwingine ambaye ni mfanyabiashara,
Andrew Komba aliyejitokeza kumfadhili Edson ada kwa mwaka wa kwanza, alisema hali
iliyomkuta mwanafunzi huyo anaifahamu kwa kuwa aliwahi kuwa mwanafunzi kwenye
chuo hicho.
Alisema akiwa chuoni hapo, alipata
kushuhudia wanafunzi marafiki zake wakiacha chuo kutokana na kukosa mikopo.
Alisema Serikali ina changamoto kwenye
suala la elimu hususan mikopo na hivyo amejitokeza kuiunga mkono kwenye
harakati za kuhakikisha utoaji elimu bure na kuondokana na umasikini zinafanikiwa.
“Kuona mtu yupo kwenye hali kama ile
inanikumbusha mambo mengi wakati nikiwa chuoni hapo na kwa kuwa mimi ni
mfanyabishara, niameamua kumsaidia ili aweze kuendelea na masomo yake,” alisema.
Aliongeza kuwa kilichotokea ni mwanzo tu
na kwamba kwa sasa wamejipanga kuanzisha taasisi itakayoshughulikia masuala
hayo ili kuwezesha wenye uwezo kujitokeza kusaidia wanafunzi wanaopatwa na
changamoto hizo.
Aidha, alisema kitendo walichofanya
kimefanya idadi kubwa ya watu kujitokeza huku wengine wakipiga simu kwa lengo
la kusaidia wanafunzi kama hao, hivyo anaamini kuwa litaleta ukombozi mkubwa
kwenye sekta ya elimu.
Mzazi
Akizungumza na JAMBO LEO mama mzazi wa
Edson, Alice Mwanisongole ambaye alilishukuru gazeti hili na wafadhili
waliojitokeza kumsomesha mtoto wake, alisema amesomesha mtoto wake huyo hadi sasa
kwa biashara ya mahindi ya kuchemsha.
“Nilikuwa nikiuza mahindi ya kuchemsha
na mtaji wangu ulikuwa Sh 7,000 nilikuwa nikinunua mahindi 50 hadi 70 na kila moja
niliuza kwa Sh 200 hadi Sh 300,” alisema na kuongeza:
“Niliifanya nikitembeza mtaani ili
nipate fedha ya kumsomesha Edson na kiasi kingine kwa chakula, lakini hivi sasa
mahindi hakuna, nanunua samaki wabichi kilo mbili na kuuza mitaani.”
Awali alisema Edson alimwambia kuwa amekosa
mkopo wa kuendelea na masomo ya chuo kikuu, Alice akahisi kuchanganyikiwa
kutokana na gharama.
Lakini sasa alisema faraja yake imerejea
baada ya kupata wafadhili wa kumsomesha mwanawe, anaamini ndoto zake sasa zitatimia.
0 comments:
Post a Comment