Mwandishi Wetu
Vurugu Marekani |
MAANDAMANO ya kupinga ushindi wa Rais mteule wa Marekani,
Donald Trump katika uchaguzi mkuu wa Marekani, juzi yaliingia katika siku ya
pili yakiambatana na vurugu, huku wananchi wakihofia haki zao za uraia kukiukwa.
Katika pwani ya Mashariki ya nchi hiyo, maandamano hayo
yalifanyika Washington, Baltimore,
Philadelphia na New York, wakati katika pwani ya Magharibi, maandamano hayo
yalifanyika Los Angeles, San Francisco na Oakland katika jimbo la California na
Portland, Oregon.
Pamoja na sehemu kubwa ya maandamano hayo kuripotiwa kuwa
ya amani, lakini kumeripotiwa matukio ya vurugu na uharibifu wa mali za watu
katika maeneo mbalimbali, zilizosababisha Polisi kuyaita kuwa ni hatari na
kutumia nguvu kuyanyamazisha.
Aidha, sehemu kubwa ya waandamanaji imetajwa kutawaliwa
na vijana wadogo ambao hawajatimiza umri wa kupiga kura, huku waandaaji wakiwa
katika umri huo huo, wakisisitiza kuwa wanataka vijana waamke, ili watetee
maisha yao ya baadaye.
Maji ya pilipili
Katika Portland, ambako inadaiwa takriban watu 4,000 waliandamana, polisi wameripoti kuwa vioo vya
magari vimevunjwa, baadhi ya magari yalichorwa kwa kutumia rangi za kupuliza,
huku madirisha ya baadhi ya nyumba yakiharibiwa, kitendo kilichosababisha watumie
maji ya pilipili na risasi za mpira kuwatawanya.
"Kutokana na tabia za waandamanaji kuonekana kuwa na
viashiria vya makosa ya jinai na hatari, maandamano hayo sasa yamechukuliwa
kuwa vurugu na wananchi wamehadharishwa,” taarifa ya Polisi ilieleza huku
ikiripotiwa kuwa watu 29 walikamatwa.
Kwingineko taarifa imeeleza kuwa makumi kwa maelfu waliendelea
kuandamana katika barabara kadhaa za Marekani, wakipinga ushindi wa Trump
uliotokana na kura za majimbo 290 dhidi ya mpinzani wake Hillary Clintons
aliyepata kuwa 228.
Kura za majimbo zilizompa ushindi Trump zilitoka katika
majimbo yaliyokuwa yakibishaniwa ya Florida kura 29; North Carolina (15); Ohio
(18); Pennsylvania (20) na Wisconsin (10).
Hata hivyo, katika kura za Wamarekani, Hillary alishinda kwa
kura 60,212,217 dhidi ya za Trump aliyepata kura 59,875,784.
Kura za Majimbo
Marekani katika uchaguzi wa rais, kura hupigwa za aina
mbili; ya kwanza ni ya kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura, ambayo ndiyo
Hillary alishinda na kura zingine 538 zinazopigwa na wawakilishi wa majimbo.
Katika kura hizo 538, kila jimbo hupewa sehemu kulingana
na idadi yake ya watu, ambapo jimbo lenye watu wengi zaidi la California lina
kura 55 na majimbo mengine yenye idadi ndogo ya watu yana kura tatu kila moja.
Hivyo, Hillary alishinda kura nyingi zaidi za Wamarekani,
lakini akazidiwa na kura za majimbo, alizoshinda Trump na hivyo kuwa uchaguzi
wa tano Marekani, ambao mshindi wa kura za Wamarekani wengi, ameshindwa kuingia
Ikulu baada ya kushindwa kupata kura 270 zinazotakiwa kwa mshindi katika kura
za majimbo.
Uchaguzi mwingine wa hivi karibuni uliokuwa na sura hiyo,
ni wa mwaka 2000, wakati mgombea wa Democrats, Al Gore aliposhinda kura za
Wamarekani 50,999,897 dhidi ya mgombea wa Republican, George Bush aliyepata
kura 50,456,002, lakini aliyeshindwa katika kura za Wamarekani, akawa rais
baada ya kushinda katika kura za majimbo.
Mali za Trump, Ikulu zalindwa
Kutokana na maandamano ya siku ya kwanza kulenga majumba
ya kifahari ya Trump, polisi waliweka ulinzi maalumu katika majumba hayo.
Katika hoteli mpya ya Trump Pennsylvania Avenue iliyoko
Washington na nyingine iliyopo Chicago, polisi waliweka uzio kuzuia watu
kuzikaribia. Katika Jiji la Manhattan, polisi walitumia vizuizi vya zege, mbele
ya jumba refu la Trump Tower.
Katika Ikulu ya Marekani mamia ya waandamanaji waliandamana
kuzunguka jengo hilo mpaka kwenye hoteli ya kimataifa ya Trump, wakati Trump na
Rais Barack Obama, wakiwa kwenye kikao cha kwanza cha kukabidhiana madaraka.
Wafuasi wa Trump
Taarifa zaidi zilieleza kuwa katika baadhi ya majengo ya
Trump ya New York na Chicago, kuliibuka mapambano kati ya wafuasi wa Rais
mteule na waandamanaji.
Waandamanaji waliokuwa na mabango wakipinga kauli za
Trump dhidi ya wanawake na wahamiaji, walifunga barabara, makutano ya barabara,
kuchoma picha na sanamu za Rais huyo mteule na katika baadhi ya maeneo,
walizingira majengo yenye jina la Trump.
Ajibu mapigo
Pamoja na hali hiyo, lakini Tump mwenyewe kupitia anuani
yake ya Tweeter, aliandika: “Nimemaliza tu
uchaguzi uliokuwa wa wazi na wa mafanikio, sasa wamejitokeza wataalamu wa
kuandamana (akimaanisha waliolipwa), wakishinikizwa na vyombo vya habari. Si
haki!”
Mmoja wa watu wa karibu wa Trump, Rudy Giuliani alizungumza
katika kipindi cha Fox & Friends juzi na kuwaita waandamanaji hao kuwa
ni “ kundi la vijana waliokosa malezi bora wanaolia hovyo barabarani.
“Tulieni, mambo si mabaya kama mnavyodhani,” alihamasisha
Giuliani, ambaye anatajwa kuwa huenda akawa Mwanasheria Mkuu wa Marekani.
Maandamano zaidi
Wanaharakati walieleza kuwa wanajipanga kuhusu hatua
inayofuata, ili makumi kwa maelfu wengine waendelee kuandamana nchini kote,
lakini wakiwa na lengo litakalokuwa wazi zaidi.
“Ni wakati wa kutoa mafunzo kwa vijana wetu namna ya
kupinga jambo kwa kutumia umma bila kufanya vurugu,” alisema mmoja wa
wanaharakati, Benjamin Jealous na kuongeza: “Kuonesha hasira dhidi ya walioko
katika madaraka kwa nidhamu na malengo.”
Baadhi wamefungua ukurasa wa Facebook wa kuhamasisha
maandamano zaidi jijini Washington, D.C., ambao ulishapata zaidi ya wasomaji 30,000
juzi mchana, huku maelfu wakiendelea kujiunga kila saa.
Mfunguaji wa ukurasa huo, Trish Gilbert, alisema
maandamano hayo yatakuwa ya amani dhidi ya sera za kibaguzi za Trump.
“Tutawaonesha wote; wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
wajumbe wa Seneti (wanaopiga kura za majimbo) na Rais mteule, kwa kuwa ni kweli
anakwenda kuwa Rais, lakini sisi tutaendelea kuwapo, lakini hatutasahau
kilichotokea, hivyo wasijaribu kuchezea tulichofanikisha kama Wamarekani,”
alisema Gilbert.
Tayari zaidi ya watu 100,000 walisaini waraka katika
mtandao wa Change.org, wakitaka waliopiga kura za majimbo kumchagua Trump,
kuhakikisha Ikulu anapewa Hillary.
*Imeandikwa kwa msaada wa mashirika
mbalimbali ya habari.
0 comments:
Post a Comment