Waandishi Wetu
Mwili wa Samuel Sitta ndani ya ukumbi wa Bunge |
MWILI wa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel
Sitta, umekuwa wa kwanza kuagwa kibunge, kwa Bunge la Muungano kufanya kikao
maalumu cha kuaga kiongozi mashuhuri.
Katika mazishi hayo ya kibunge
yaliyofanyika jana, Bunge lililazimika kutengua kanuni ili kuruhusu mwili wa
Sitta kuingizwa ndani ya ukumbi huo, pamoja na ndugu na wanafamilia ambao si
wabunge.
Baada ya mwili wa Sitta kuingizwa
bungeni na kuwekwa karibu na meza ya Siwa, Spika Job Ndugai, aliita
walioandaliwa kutoa dua.
Mwakyembe
Akisoma dua, Waziri wa Katiba na Sheria,
Dk Harrison Mwakyembe alishindwa kumalizia baada ya kulia alipotamka msaada wa
Sitta kwa watu wengine.
Dk Mwakyembe alishindwa kuendelea akalia
na kuamsha vilio kwa wabunge wengine, ndugu na viongozi waliokuwa ukumbini
hapo.
"Sitta alikuwa mtu wa kusaidia wengine,
alinisaidia, sijui nimwelezee vipi Sitta, aah, aaah,’’ kilio kilifuata na
kushusha kipaza sauti chini akijaribu kujikaza kuendelea kuzungumza, lakini
alishindwa na kuondoka.
Ndugai
Spika Ndugai alisema hivi karibuni
aliugua sana na kufikia hatua ya kukata tamaa, lakini akapata nafuu na kumwomba
Mungu aishi ili atende hata nusu ya mambo mema aliyotenda Sitta akiwa Spika.
‘’Sitta alifanya mambo mengi
yaliyobadilisha Bunge na alikuwa mlezi wa wengi nikiwamo mimi, ndiye
aliyeanzisha mfumo wa kuwa na wenyeviti waliomsaidia na nilikuwa mmoja wao, niliugua
sana nikakata tamaa naomba Mungu nipate muda nifanye hata nusu ya aliyotenda,’’
alisema Ndugai.
Majaliwa,
Zitto
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alishindwa
kusoma hotuba ya kuahirisha Bunge badala yake akaomba iingie yote kwenye
taarifa rasmi za Bunge (Hansard).
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (Act-Wazalendo)
katika salamu zake alisema Sitta ana mengi, lakini Tanzania itamkumbuka kuwa
mtu aliyejaribu kuboresha kila alichokabidhiwa, shujaa wa wote wanaoamini
katika uwajibikaji kitaasisi.
“Sitta ni mwanasiasa aliyepanda na kushuka
na kisha kupanda na kubaki kileleni, ameweka rekodi nyingine - kwa Bunge
kufanya kikao maalumu kuanzia mmoja wa wajumbe wake mahiri kati ya mwaka 1975 -
2015 isipokuwa tu kwa kipindi cha 1995 - 2005. Rekodi hii itaendelea kwa
wengine wote watakaofuata baada yake,’’ alisema Zitto na kuongeza:
‘’Ni mtu wa namna gani wewe Sitta? Spika
wa Kasi na Viwango, unayeweka rekodi hata ukiwa umelala ndani ya jeneza lako
lililopambwa na Bendera ya Taifa letu, ukielekea nyumbani kwako Urambo kwenye
nyumba yako ya milele.
“Ulikuwa hushindwi ukiwa hai, umeonesha
umahiri wako hata ukiwa kwenye umauti. Kweli wewe ni Spika wa Watu. Tuliokupenda
tunaokujua,’’ alisema.
Alisema Sitta alikuwa na vyeo vingi;
Mbunge, Naibu Waziri, Waziri, Mkuu wa Mkoa, Waziri tena, Mkurugenzi Mtendaji,
Spika, Waziri tena na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba. ’’Lakini wala,
tunakuita Spika Sitta tu. Kwa nini? Kwa sababu alama yako ni Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania”.
“Si kwamba umeanzisha Bunge wewe, la
hasha. Lakini ulipopokea uspika wa Bunge letu, kama ilivyo jadi yako,
uliliboresha, uliwezesha kutunga kanuni mpya, uliimarisha Mhimili huu na
kuuweka katika nafasi yake ya kikatiba,” alisema Zitto.
Alisema bado anasikia mwangwi wa sauti
yake nene kutoka kwenye Kiti cha Spika akitaka mawaziri wajibu maswali kwa
ufasaha.
“Hukuisahau Tabora yako, ukiona kuna
swali linalohusu mkoa wako wa Tabora hukusita kuwaambia mawaziri wajibu vizuri
(hasa kuhusu barabara) au ukiamsha Jeshi lako akina Lucas Selelii, wakisema
"… wewe leo ukipata dharura Urambo unafikaje?" Yote hiyo kutilia
nguvu umuhimu wa maendeleo ya mkoa wako,’’ alisema.
Alisema Sitta ni kielelezo cha demokrasia
ya vyama vingi bungeni, alitoa nafasi kwa wabunge wote wa kambi zote ndani ya
Bunge, “ulikuwa muungwana”.
Lissu,
Mbowe
Akizungumza kwa niaba ya Chadema, Mbunge
wa Singida Mashariki,Tundu Lissu alisema Sitta alikuwa mmoja wa miamba ya
Tanzania na Bunge na kwamba amepewa heshima kubwa sana kuingizwa bungeni.
Alisema awali Bunge lilikuwa la chama
kimoja, lakini Sitta alilitoa kwenye mfumo huo na kwa sasa limekuwa la vyama
vingi, hivyo yeye ndiye amefikisha Bunge lilipo sasa.
"Sitta alitaka Bunge lenye meno,
linalosimamia na kudhibiti Serikali, Mhimili wa Dola na si msindikizaji wa
mingine, jambo alilolitenda na rekodi yake haiwezi kufutika kwenye nyoyo zetu
wabunge," alisema.
Aliongeza kuwa Sitta hakuwa kibaraka wa
mtu, kwa kuwa tangu akiwa kijana, alionesha ni mtu mwenye misimamo huru na ndio
ulimfanya aweke Bunge kwenye ramani ya siasa za Tanzania.
Alitaka wabunge kutoishia kwenye majonzi
na vilio, badala yake wajiulize kama Bunge lililopo sasa, ndilo Sitta alitaka
liwe au la, kwa kuwa wakijiuliza hayo na kupata majawabu yake, watakuwa
wamemuenzi kwa mazuri aliyofanya.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe alisema Sitta ameondoka na kuacha kazi kubwa ya Katiba ambayo
aliianzisha.
Alisema Sitta kwao alikuwa kiongozi
asiye na ubaguzi wa kiitikadi kwa kuwa aliunganisha makundi yote, alipigania
haki, hakusita kulitaka Bunge kusimama nafasi ya Mhimili wa kusimamia haki.
"Leo mwenzetu ametuacha, hivyo ni
siku ambayo Mungu ametupa nafasi ya kutafakari dhamana tuliyopewa ya kuongoza
wenzetu," alisema.
Magufuli
Mapema asubuhi Dar es Salaam, Rais John
Magufuli aliongoza maelfu ya wananchi kuaga mwili wa Sitta kwenye viwanja vya
Karimjee, kabla ya kupelekwa bungeni Dodoma.
Magufuli alikuwa wa kwanza kuaga saa
4:08 asubuhi na kufuatiwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na
Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete.
Baada ya viongozi hao wakuu kuaga, viongozi
wengine pamoja na wastaafu walipata nafasi hiyo pamoja na wananchi wa kawaida na
baada ya hapo mwili huo ulisafirishwa kwenda Dodoma saa 6 mchana.
Kabla ya kuaga mwili huo, baadhi ya
viongozi, familia na marafiki walipata nafasi ya kueleza namna walivyomfahamu
Sitta, ambapo wengi walieleza alivyokuwa kiongozi shupavu na aliyependa
kusaidia watu bila kutarajia malipo.
Makinda,
Salma Kikwete
Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda alisema
Sitta alikuwa kaka yake aliyempigia debe wakati akigombea ubunge mwaka 1975 na baadaye
alimwongoza vizuri walipofanya kazi pamoja.
“Ninachoshukuru kuliko yote ni kwamba
kabla hajaenda kutibiwa Ujerumani, nilikaa naye kwa saa moja kujadili mambo
mengi ya nchi, lakini bahati mbaya amerudi amefariki dunia, nimeumia mno,”
alisema.
Mama Salma Kikwete, alisema Sitta
ameacha pengo katika Taifa kwani alifanya kazi nyingi zilizoonekana na bado
mchango wake ulikuwa unahitajika duniani.
Sumaye,
Warioba
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu
ya Tatu, Frederick Sumaye alisema Sitta alikuwa jasiri aliyependa kusimamia
anachokiamini bila kuogopa mtu.
“Sitta alikuwa mtu mwenye busara,
mchapakazi sana lakini sifa moja kubwa huwa akiamini jambo, lazima alifanye na
hulijengea hoja hata kama limekataliwa hadi watu waelewane,” alisema.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu
ya Pili, Jaji Joseph Warioba alisema Sitta alikuwa mtu asiyeogopa kitu,
mzalendo na alikuwa akifanya kazi kwa kujitoa na sasa ameondoka wakati Taifa
bado linamhitaji.
Serikali,
CCM
Akitoa salamu za rambirambi kutoka
serikalini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah
Kairuki alisema Sitta ni kiongozi ambaye aliandika historia wakati historia za
watu kwa kawaida huandikwa na wengine.
Alisema wapo viongozi waliojipatia sifa
lakini Sitta ameacha alama zisizoweza kufutika katika Taifa kutokana na
utendaji kazi aliokuwanao.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda alisema Sitta ndiye alimsomesha mwaka 2010, wakati alipokosa ada akiwa
Chuo cha Ushirika Moshi, baada ya kufahamiana naye kupitia Waziri wa Katiba na
Sheria, Dk Harrison Mwakyembe.
“Nitamkumbuka sana Sitta maana siku niliyokutana
naye nilimwambia sina ada, akaniambia nitakulipia kwa kadri utakavyokuwa
unasoma, akanitambulisha hadi kwa familia yake, hata kikao changu cha harusi
aliitisha yeye,” alisema.
Makonda alimshauri Rais Magufuli, kwamba
kwa kuwa Serikali inahamia Dodoma, litengwe eneo maalumu la kuzika viongozi walioacha
historia kwa nchi kwa kuwa kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakisahaulika na historia
zao kupotea.
Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka
alema Sitta ameacha historia kubwa kwa kuwa hata awamu ya Kikwete, alisimama na
kumwambia Rais kuwa amesahau kuzungumzia
suala la iliyokuwa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) jambo lililomfanya Rais
kuchukua hatua zaidi.
0 comments:
Post a Comment