Joyce Kasiki, Dodoma
Hafidh Ally Tahir |
ALIYEKUWA Mbunge wa Dimani, Zanzibar,
Hafidh Ally Tahir aliyefariki dunia jana, alikuwa mmoja wa wabunge waliokuwa
wakitarajiwa kiuhudhuria maziko ya Spika mstaafu Samwel Sitta, Urambo leo.
Tahir alifariki dunia saa 9 alfajiri
usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya mkoa mjini hapa kutokana na kupatwa
na matatizo ya moyo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana
aliongoza wabunge kuaga mwili wake kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa kabla ya
kupelekwa Zanzibar kwa maziko.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri
Mkuu alitoa pole kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, familia ya marehemu na wabunge
wote.
"Tumepokea taarifa za msiba huu kwa
mshituko mkubwa. Leo tupo kwenye wakati mgumu sana. Tumeondokewa na viongozi
wengi," alisema.
Alisema wafiwa wanatakiwa kuishi kwa
upendo. "Tumwombee marehemu, tuiombee familia iwe na moyo wa utulivu
katika kipindi kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao."
Hafidh alizaliwa Oktoba 30, 1953 na kupata
kuwa Mkuu wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (1970-1978) na kuwa mbunge tangu mwaka
2005 hadi mauti yanamkuta.
Enzi ya uhai wake, alishiriki katika
masuala ya michezo; akiwa mchezaji na kisha mwamuzi wa soka mwenye beji ya FIFA
na kocha msaidiizi wa timu ya soka ya Bunge.
Hadi juzi, alishiriki shughuli
mbalimbali ikiwamo ya uchaguzi wa viongozi wa tawi la Umoja wa Wabunge
WanaYanga mjini hapa ambapo alichaguliwa
kuwa Katibu.
Spika Ndugai alisema Bunge limepata pigo
lingine la kuondokewa na Mbunge Tahir.
Mapema kabla ya kuahirishwa kwa shughuli
za Bunge kutokana na kifo hicho, wabunge walisimama kwa dakika moja kumwombea
mbunge huyo ambaye saa tatu asubuhi mwili wake ulifikishwa viwanja vya Bunge
ili wabunge watoe salamu za rambirambi na heshima za mwisho.
Alipokuwa akitangaza kifo cha Mbunge
huyo, Ndugai alisema alifariki dunia Novemba 11 wakati akipewa matibabu katika
hospitali ya mkoa.
Ndugai alisema, aliugua kwa muda mfupi,
ambapo baada ya kujisikia vibaya alikwenda hospitali mwenyewe usiku wa jana na
alipofika aligundulika na tatizo la moyo na akiwa katika matibabu alifariki dunia.
Ndugai alisema Tahir alikuwa mmoja wa
wabunge walioomba kwenda Urambo kuhudhuria
maziko ya Spika mstaafu wa Bunge la Tisa, Samwel Sitta na alikuwa mmoja wa
wabunge waliokuwa kwenye orodha ya kwenda Urambo.
Baadhi ya wabunge waliteuliwa kuusindikiza
mwili wa Tahir Zanzibar kwa maziko wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
0 comments:
Post a Comment