Celina Mathew
Profesa Lipumba na Maalim Seif |
MWENYEKITI wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba
amesema Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad hana mamlaka ya
kuzuia ziara zake mikoani.
Kauli hiyo imekuja ikiwa imepita
takriban wiki moja tangu gazeti hili kuripoti kuhusu waraka wa Maalim Seif
uliotamka; kuwa chama hicho hakitasita kuchukua hatua dhidi ya kiongozi atakayeshirikiana
na mwanachama au kiongozi aliyefutiwa au kusimamishwa uanachama na uongozi.
Katika waraka huo kwa makatibu wa wilaya
zote wa chama hicho aliouandika Oktoba 7 na kuwafikia wahusika takriban wiki
mbili zilizopita, Maalim Seif alisema uamuzi huo una baraka zote za Baraza Kuu
la Uongozi la CUF.
“Mimi ni Mwenyekiti wa Chama hawezi
kunizuia kwenda ninakotaka maana hiki ninachokifanya sasa ni kwa ajili ya
kuijenga CUF…, hata huko Zanzibar pia nitakwenda muda ukifika, maana huko ndiko
chama kimejengeka zaidi kuliko huku (Bara),” alisema Profesa Lipumba jana
katika mahojiano na JAMBO LEO.
Lipumba ambaye Baraza hilo lilimvua uanachama
huku Ofisi ya Msajili ikiwa imetoa taarifa ya kumtambua kama Mwenyekiti halali
wa CUF, alisema licha ya mgogoro uliokikumba chama hicho, atajitahidi kukijenga
na kuhakikisha hali inakuwa shwari.
Katika maelezo yake, Profesa Lipumba
alisema: “Nitaendelea na ziara zangu wala sitasitisha na wala Maalim hana uwezo
wa kuzuia.”
Msomi huyo ambaye alitamka wazi kutotaka
ushirikiano na vyama vinavyounda Ukawa, alisema wanaosema kuwa anaungwa mkono
na wanachama wachache ndani ya CUF wanajidanganya.
“Hizo
taarifa si za kweli maana naungwa mkono na watu wengi na nimeshazunguka maeneo
mbalimbali na wote wananiunga mkono hivyo ni propaganda zao wameamua
kuzungumza,” alisema.
Katika hatua nyingine, alisema kuwa hana
tatizo na Maalim na kwamba kama anahitaji kuzungumza naye aende ofisini ili
kuendelea kukijenga chama.
Akizungumzia kesi iliyofunguliwa
mahakamani kupinga kurejea kwake, alisema suala hili lingeweza kumalizwa kwa
mazungumzo.
“Inafedhehesha
kwa kweli maana hata Rais Magufuli (John) wakati akizungumza na wanahabari,
alitupiga madongo kuwa tuliungana na sasa tumeamua kufukuzana wenyewe…, katika
hili la mahakamani tungeweza kukaa meza moja na kuyamaliza ndani ya chama,” alisema.
Alisema kwa sasa anachosubiri ni uamuzi
wa Mahakama maana hawezi kujadili suala ambalo liko mahakamani na kesi yake
inaendelea na kuwataka wanachama wa chama hicho kuwa wavumilivu.
Tangu Septemba 23, Ofisi ya Msajili
ilipotoa taarifa ya kumtambua Profesa Lipumba ambaye kitaaluma ni Mchumi kama Mwenyekiti
wa chama hicho, amefanya ziara kadhaa kwa ajili ya kuimarisha CUF, huku
akipingwa katika baadhi ya wilaya.
0 comments:
Post a Comment