Mwandishi Wetu
John Magufuli |
RAIS John Magufuli ametaka waandishi wa habari kufanya kazi
yao ya kiuchunguzi kwenye benki, ambako wanasiasa wamekopa mabilioni wa fedha,
ili waandike kwa kuwa mpaka sasa haijulikani kama wataweza kuzirudisha.
Akizungumza na wahariri katika mahojiano ya ana kwa ana
Ikulu Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema wanasiasa wamekuwa wakichangia
kufa kwa benki, kutokana na kukopa fedha nyingi na kusababisha madeni makubwa.
“Benki zilikuwa zinakopesha wanasiasa wa Ukawa na CCM,
lakini cha kushangaza hawarudishi fedha hizo na kuna benki zimefilisika, hivyo
inabidi waanikwe hadharani bila kujali itikadi zao, ili kurejesha nidhamu katika
ukopaji,” alisema Magufuli bila kutaja benki hizo.
Kauli hiyo ya Magufuli, imekuja siku chache baada ya
kufungwa kwa wiki moja kwa benki ya Twiga Bancorp, baada ya kuishiwa na mtaji
uliopungua mpaka sifuri na kwenda hasi zaidi ya 20 na kusababisha Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), kuichukua ili kulinda amana za wateja, huku benki zingine
zikilia hasara.
Mashirika ya umma
Mbali na wanasiasa, Rais Magufuli alisema hata watendaji
wakuu wa mashirika ya umma, wamekuwa wakifanya biashara na benki kwa kuchukua
fedha za umma, ambazo ni za Watanzania na kuzifanyia biashara.
Alifafanua kuwa watendaji hao wamekuwa wakiweka mabilioni
hayo ya taasisi za umma kwenye akaunti za muda maalumu kwenye benki hizo na
kupata riba ya asilimia nane, huku benki zikitumia fedha hizo hizo kukopesha Serikali
kwa riba ya asilimia 15 na kuibia wananchi katika malipo ya riba ya Serikali.
Alisema benki zipo 53 na zinawapa ahadi watendaji hao wa
mashirika ya umma, ili kupata fedha hizo na kuzifanyia biashara kwa Serikali
kwa kuikopesha kwa asilimia 15 hadi 16, lakini waliokuwa wanaumia ni wananchi
wa chini, wanaolipa kodi inayotumika kulipa riba katika benki hizo.
“Fedha ni yenu halafu benki zinaitumia kukopesha Serikali
ambayo inakuja kulipa asilimia 16, maana yake anayeumia ni wa chini na
watendaji hao wanaamua kufanya hivyo na ndiyo maana zote zimeacha biashara na
wananchi, zikawa zinategemea kufanya biashara na Serikali. Hii ni njia mbaya ya
kukua kwa uchumi," alisema.
Aliongeza kuwa hata miamala ya benki zote nchini, inaonesha
zilikuwa zikianzishwa kufanya baishara na Serikali tu, ndiyo maana amekata mrija
huo.
Alisema fedha kwenye mashirika ya umma, anazichunguza
maana si zao na kama ni za Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), zimepatikana
kwa ajili ya utalii, hivyo si zao bali za Watanzania na lazima zirudi kwao.
Kufuru
Rais Magufuli alisema watu wenye tabia kama hizo, wana
uwezo wa kuchukua nyumba zote Sinza, Dar es Salaam ili kuhakikisha kila siku wanabadilisha
mahali pa kulala kwa kuwa fedha hizo ni nyingi na hawana matumizi nazo.
Alitaja tabia nyingine ya taasisi zilizokuwa na fedha za
ziada za kuweka kwenye akaunti za muda maalumu benki, kuwa walifanya vikao nje
ya nchi na kulipa watendaji wa Bodi nzima na kuwafanya kuwa watumwa wao, kwa kuwa
wanalipwa kiasi wanachotaka.
Rais Magufuli alisema suala kama hilo halitajitokeza tena,
huku akieleza kuwa siku moja atakumbukwa kwa alichokuwa akifanya na kuongeza
kuwa hata kama hatakuwa Rais maarufu Tanzania, basi atakuwa maarufu Mbinguni
kwa kuwa ana nia njema na Watanzania.
0 comments:
Post a Comment