* Atoa waraka mkali kwa makatibu wa wilaya
* Kambi ya Mwenyekiti yasisitiza kuendelea
Fidelis Butahe
WAKATI Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa
na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, akijiandaa
kuendelea na ziara zake za kuimarisha chama hicho leo, imebainika kuwa Katibu Mkuu
wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad amesambaza waraka kuwatahadharisha
viongozi watakaoshirikiana na masomi huyo kuwa watachukuliwa hatua kali.
“Chama hakitasita kuchukua hatua dhidi
ya kiongozi yeyote ambaye atashirikiana na mwanachama au kiongozi aliyefutiwa
au kusimamishwa uanachama na uongozi,” inaeleza sehemu ya waraka huo ambao JAMBO
LEO imeuona, ukimnukuu Katibu Mkuu huyo.
Katika waraka huo kwa makatibu wa wilaya
zote wa chama hicho aliouandika Oktoba 7 mwaka huu na kuanza kuwafikia wahusika
takribani wiki mbili zilizopita, Maalim Seif amesema uamuzi huo una baraka zote
za Baraza Kuu la Uongozi la CUF.
Tangu Septemba 23 mwaka huu, Ofisi ya
Msajili ilipotoa taarifa ya kumtambua Profesa Lipumba ambaye kitaaluma ni
mchumi kama mwenyekiti wa chama hicho, ameshafanya ziara kama hiyo inayolenga
kukiimarisha CUF katika baadhi ya wilaya mkoani Mtwara na Lindi huku ile na
Tanga akikumbana na kigingi baada ya mwenyekiti wa CUF wilaya ya Tanga, Rashid
Jumbe kutaka asipewe ushirikiano. Kesho Profesa Lipumba anatarajiwa kufanya
ziara nyingine wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Alipoulizwa kuhusu waraka huo, Kaimu
Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF, Mbarara
Maharagande alisema, “Umeona wapi hizo taarifa…, ni mambo ya ndani ya chama.
Barua hizo zimepelekwa katika wilaya kwa njia mbalimbali. Watakaokiuka
watachukuliwa hatua…, wapo watakaofukuzwa au kusimamishwa uanachama kwa kukiuka
maagizo kama Profesa Lipumba.”
Alisema wanaomuunga mkono ni baadhi ya wajumbe
wa Mkutano Mkuu, kubainisha kuwa maeneo anayotembelea kiongozi huyo anawafuata
watu wachache wanaomuunga mkono.
“Takribani wiki moja iliyopita (Lipumba)
alikwenda Bagamoyo licha ya kutoungwa mkono na viongozi, zaidi ya wanachama
wachache. Pale Mkuranga mwenyekiti, katibu wa wilaya na kamati ya utendaji wote
hawamuungi mkono. Kati ya wilaya 108 nchini, Lipumba anaungwa mkono katika wilaya
tisa tu.”
Akizungumzia ziara hiyo, Mwenyekiti wa
CUF wilaya ya Mkuranga, Ali Athuman Ubuguya alisema, “leo (jana) tumefanya
kikao cha kamati ya utendaji kujadili ziara ya Lipumba. Tumeipinga ziara yake
kwa sababu si kiongozi wa chama na tayari tumeshawajulisha polisi kwa barua.”
Profesa Lipumba alitangaza kuachana na
uongozi wa chama hicho Agosti 8 mwaka jana baada ya CUF kukubaliana na vyama
vingine vinavyounda Ukawa kumsimamisha Edward Lowassa kuwania urais.
Hata hivyo, Juni 8 mwaka huu aliandika barua
kusitisha mpango wake wa kung’atuka kwenye wadhifa huo baada ya kushawishiwa na
viongozi wa dini, chama hicho na wanachama.
Agosti 21, chama hicho kilifanya Mkutano
Mkuu kupokea taarifa ya kujiuzulu kwake na kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi
yake na nyingine za uongozi.
Hata hivyo, baada ya kupiga kura
kukubali barua ya kujiuzulu ya kiongozi huyo huku wajumbe 476 wakiridhia na 14
kupinga, mkutano huo ulivunjika kabla ya kuingia kwenye hatua ya uchaguzi wa
viongozi wapya baada ya kundi la vijana wanaoaminika kuwa wafuasi wa Profesa
Lipumba kuvamia ukumbini wakishinikiza arudishwe kwenye nafasi yake.
Wiki moja baadaye Baraza Kuu la Uongozi la
chama hicho lilimsimamisha uanachama Profesa Lipumba na kumteua Julius Mtatiro
kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya chama hicho uamuzi ambao ulipingwa na
Ofisi ya Msajili, kutangaza kumtambua Lipumba.
Baada ya vuta nikuvute, Septemba 27, baraza
hilo lilimfukuza uanachama Profesa Lipumba jambo ambalo liliendeleza mgogoro
ndani ya chama hicho na kukifanya kuwa na kambi mbili, inayomuunga mkono mchumi
huyo na ile ya Maalim Seif.
Katika waraka huo Maalim Seif ameituhumu
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi kutumika ili
kukisambaratisha CUF, kuwataka viongozi wote wa chama hicho kuwa makini.
“…, kuna mkakati mkubwa wa kumtumia
Lipumba ili aiondoe CUF kwenye ajenda zake za msingi ikiwemo suala la kupigania
haki ya Wanzanzibari katika uchaguzi mkuu uliopita na kuiondoka CUF katika
kujenga ushirikiano na vyama vingine vya upinzani kupitia Ukawa,” inaeleza
sehemu ya waraka huo.
“Mipango ikifanikiwa, CUF itahama kwenye
ajenda ya kudai haki ya ushindi wa chama Zanzibar na pia chama kitatumika kuvunja
ushirikiano wa Ukawa.”
Katika waraka huo, Maalim Seif alieleza
jinsi vyombo vya ulinzi na usalama vilivyomsaidia Profesa Lipumba kuvamia
Mkutano Mkuu wa chama hicho na ofisi za makao makuu ya CUF kwa kuvunja milango,
mara baada ya Ofisi ya Msajili kumtangaza kuwa ndiye mwenyekiti wa chama hicho.
“Baraza Kuu la Uongozi Taifa
linazielekeza wilaya zote za chama kuendelea kuwa watulivu wakati hatua
mbalimbali za kistaarabu na kisheria zikifanyika ili kurejesha ofisi hizo
katika mikono ya chama,” anaileza Maalim katika waraka huo.
Akizungumzia ziara za Profesa Lipumba,
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa chama hicho, Abdul Kambaya
alisema, “keshokutwa (kesho) profesa atakuwa na ziara ya siku moja wilayani
Mkuranga. Wiki ijayo atafanya ziara kama hiyo wilaya ya Kisarawe na baadaye
atakwenda Namtumbo. “
“Huu ni utaratibu wake tangu aliporejea
kuhakikisha kuwa anakwenda maeneo mbalimbali kwa ajili ya kukiimarisha chama.”
0 comments:
Post a Comment